Feb 16, 2021 07:59 UTC
  • Mkuu mpya wa WTO ataka usawa katika ugavi wa chanjo za Corona

Mkuu mpya wa Shirika la Biashara Duniani (WTO) ametahadharisha dhidi ya 'utaifa' katika ugawaji wa chanjo za kukabiliana na ugonjwa wa Covid-19 na kusisitiza kuwa, janga la Corona linaweza kudumaza ukuaji wa uchumi wa nchi zote duniani, maskini na hata tajiri.

Ngozi Okonjo-Iweala amesema kipaumbele chake cha kwanza atakapoingia ofisini mwezi ujao ni kuhakikisha kuwa WTO inachukua hatua za ziada za kupambana na janga la Corona, na kwamba ataziasa nchi wanachama ziondoe vizuizi vya kusafirishwa nje dawa na suhula mbalimbali za matibabu.

Amesisitizia udharura wa kuwepo uadilifu katika ugawaji wa chanjo za Corona kati ya nchi tajiri na maskini duniani na kueleza bayana kuwa, ujio wa spishi na aina kadhaa mpya za virusi vya maradhi hayo hauwezi kukabiliwa iwapo nchi zenye uwezo mkubwa zitaendelea kujirundukia chanjo huku zile za kipato cha chini zikikosa kabisa au zikipata chache.

Makao makuu ya WTO mjini Geneva, Uswisi

Amesema jukumu lake la kwanza atakapochukua hatamu za uongozi ndani ya WTO ni kupambana na mgogoro wa ugawaji usio na usawa wa chanjo za ugonjwa wa Covid-19.

Waziri huyo wa zamani wa Fedha wa Nigeria na mkurugenzi wa ngazi ya juu wa Benki ya Dunia aliteuliwa jana Jumatatu kwa kishindo kuwa Mkurugenzi Mkuu mpya wa WTO, na anatazamiwa kuanza kazi Machi Mosi.

Hii ni mara ya kwanza kwa shirika la WTO kuongozwa na mwanamke tena wa Kiafrika.

Tags