Mar 31, 2021 03:02 UTC
  • Wakili wa Floyd awakosoa Wamarekani kwa kupuuza uhalifu na ubaguzi dhidi ya watu weusi

Wakili wa familia ya George Floyd amewakosoa Wamarekani kwa kupuuza jinai na uhalifu unaofanywa kwa makusudi dhidi ya jamii ya watu weusi nchini humo.

Jeff Storms ambaye anawakilishi familia ya George Floyd mahakamani amewataka Wamarekani wasipuuze tena na kunyamazia kimya uhalifu na jinai zinazofanywa dhidi ya Wamarekani weusi.

Storms ameongeza kuwa: "Wengi wetu tunapuuza kwa makusudi na kufumbua jicho jinai na uhalifu unaofanywa dhidi ya dada na kaka zetu wenye asili ya Afrika, lakini hii leo ni kipindi cha kihistoria cha kuonyesha kwamba, hatutapuuza tena chuki dhidi ya watu weusi." Amesema Wamarekani wanapaswa kushikamana na familia zilizopatwa na masaibu kwa ajili ya kung'oa kabisa chuki katika jamii.

George Floyd

Kesi ya afisa wa zamani wa polisi ya Marekani, Derek Chauvin aliyemuua kwa damu baridi, Mmarekani mwenye asili ya Afrika, George Floyd ilianza jana, miezi kumi baada ya mauaji hayo ya kinyama. Matokeo ya kesi hiyo yanatarajiwa kuwa na athari kubwa na muhimu katika mahusiano ya kimbari baina ya Wamarekani. 

Mkanda wa video ulirushwa sana katika mitandao ya kijamii, ulimuonesha afisa huyo mzungu wa polisi ya Marekani akimkandamiza kwa goti hadi kumuua Mmarekani huyo mwenye asili ya Afrika, mchana kweupe mbele ya kadamnasi ya watu, huku muhanga wa ukatili huo akilalamika kuwa hawezi kupumua hadi alipokata roho. Ukatili huo ulifanyika tarehe 25 Mei katika mji wa Minneapolis huko Minnesota.

Muda mchache kabla ya kukata roho, George Floyd mbali na kusikika akilalamika kuwa hawezi kupumua, alisikika pia akiomba maji na kumbembeleza mzungu huyo katili asimuue, lakini yote hayakusaidia kitu.  

Tags