Interpol yakamata makumi ya wafanya magendo ya binadamu
Polisi ya Kimataifa (Intepol) imesema imewatia mbaroni wafanya magendo ya binadamu zaidi ya 80, na wasafirishaji haramu wa wahajiri wapatao 63 katika opersheni iliyofanyika katika nchi 24 duniani.
Interpol imesema operesheni hiyo ilifanyika baina ya Machi 28 na Aprili 2 mwaka huu katika nchi 24 duniani zikiwemo Kenya, Brazil na Ufaransa, ambapo wafanya magendo ya binadamu 88 wamekamatwa.
Polisi ya Kimataifa imefanikiwa kuwaokoa pia watu wasiopungua 500, wahanga wa biashara hizo haramu. Taarifa ya Interpol imesema taasisi hiyo imewanusuru wahajiri kadhaa waliokuwa wakitumikishwa kama wajenzi huko Congo DR.
Imesema raia hao wa Lebanon, Syria na Jordan walikuwa wakifanyishwa kazi za sulubu bila mshahara wowote, wasijue cha kufanya na kwa kukimbilia kwa kuwa wafanya magendo wamezuia pasi zao za kusafiri.
Juergen Stock, Katibu Mkuu wa Interpol amesema miongoni mwa watu iliowanusuru ni binti wa miaka 15 raia Jamhuri ya Kidemokraia ya Kongo, ambaye amekuwa akidhallishwa kingono na wafanya magendo ya binadamu.
Inaarifiwa kuwa, binti huyo Mkongamani alijikuta mikononi mwa wafanya magendo ya binadamu akitoroka ndoa ya kulazimishwa.
Polisi ya Kimataifa imesema biashara ya magendo ya binadamu na kuuzwa wahajiri kama watumwa imeongezeka kwa kiasi kikubwa hususan katika kipindi hiki cha jang la Corona, kwa kuwa aghalabu ya watu wanaojikuta mikononi mwa walaghai hao ni wanaojaribu kukimbia dhiki za maisha zilizochangiwa na janga hilo linaloendelea kuisimbua dunia.