Apr 25, 2021 06:12 UTC
  • Nusu ya chanjo bilioni 1 za corona imetolewa katika nchi tatu pekee duniani

Zaidi ya dozi bilioni moja za chanjo za kukabiliana na ugonjwa wa Covid-19 zimekwishapeanwa katika maeneo mbalimbali ya dunia kufikia sasa, lakini zaidi ya asilimia 50 ya chanjo hizo zimetolewa katika nchi tatu pekee.

Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, hadi kufikia jana jioni, kwa akali dozi 1,002,938,540 za corona zilikuwa zimetolewa katika nchi na maeneo 207 ya dunia, chini ya miezi mitano baada ya kampeni ya kwanza kabisa ya utoaji chanjo kwa umma kuanza.

Hata hivyo cha kusikitisha ni kuwa, asilimia 58 ya chanjo hizo zimetolewa katika nchi tatu pekee za Marekani (dozi milioni 225.6), China (milioni 216.1) na India (milioni 138.4).

Hivi karibuni pia, Waziri wa Afya wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alifichua kuwa, karibu asilimia 80 ya chanjo za virusi vya corona imetolewa katika nchi 10 tu tajiri duniani na kwamba, hadi sasa nchi 18 zenye kipato cha chini hadi kati hazijapokea chanjo yoyote.

Mpango wa kimataifa wa COVAX umeshindwa kuleta uwiano katika ugawaji wa chanjo za corona duniani

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, nchi 12 duniani hazijaanza utoaji wa chanjo ya corona; ambapo saba ni za Kiafrika  (Tanzania, Madagascar, Burkina Faso, Chad, Burundi, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Eritrea); tatu za eneo la Oceania (Vanuatu, Samoa na Kiribati); nchi moja ya Asia (Korea Kaskazini); na moja ya eneo la Caribbean (Haiti).

Shirika la Afya Duniani (WHO) na Umoja wa Mataifa (UN) zimekosoa mara kadhaa ugawaji usio wa kiadilifu wa chanjo za Corona duniani. WHO na UN zinasisitiza kuwa, mgogoro unaoikabili dunia hivi sasa unahitajia jibu la kimataifa, na kwamba ufumbuzi wa suala la ugavi wa chanjo unahitaji umoja na ushirikiano wa nchi mbalimbali duniani. 

 

Tags