Rais Putin wa Russia naye atabiri kuwa Marekani inaelekea kusambaratika
https://parstoday.ir/sw/news/world-i71008-rais_putin_wa_russia_naye_atabiri_kuwa_marekani_inaelekea_kusambaratika
Rais Vladimir Putin wa Russia katika kikao chake cha hivi karibuni na waandishi habari pembizoni mwa Kongamano la Kimataifa la Uchumi mjini St. Petersburg alisema kuwa Marekani inakumbwa na matatizo ambayo madola makubwa hukumbana nayo. Amebaini kuwa matatizo ambayo Marekani inakabiliana nayo yanatokana na nguvu ilizonazo na sasa imeshindwa kutatua matatizo hayo na hali hiyo ndiyo ile ile liliyokumbana nayo Shirikisho la Sovieti.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 07, 2021 08:53 UTC
  •  Vladimir Putin
    Vladimir Putin

Rais Vladimir Putin wa Russia katika kikao chake cha hivi karibuni na waandishi habari pembizoni mwa Kongamano la Kimataifa la Uchumi mjini St. Petersburg alisema kuwa Marekani inakumbwa na matatizo ambayo madola makubwa hukumbana nayo. Amebaini kuwa matatizo ambayo Marekani inakabiliana nayo yanatokana na nguvu ilizonazo na sasa imeshindwa kutatua matatizo hayo na hali hiyo ndiyo ile ile liliyokumbana nayo Shirikisho la Sovieti.

Putin ameongeza kuwa, watawala wa Marekani wanadhani kuwa kutokana na kuwa nchi yao ina uwezo mkubwa wa kisiasa, kiuchumi na kijeshi basi inaweza kukabiliana na matatizo ya aina zote. Rais wa Russia amesema tatizo la jamii kama hiyo ni kuwa hudhani ina nguvu za kutosha na iwapo itakosea haitapata madhara.

Rais Putin ameendelea kuashiria matatizo makubwa ambayo Marekani inakumbana nayo na sera zake zilizfeli za kutumia mabavu na kusema, hivi sasa matatizo ya nchi hiyo yanazidi kuongezeka na itafika wakati ambao haitaweza kuyatatua. Kwa msingi hiyo kwa yakini Marekani imeingia ule ule mkondo ambao ulichukuliwa na Shirikisho la Sovieti. Kwa kuzingatia hali ya hivi sasa ya Marekani, Rais wa Russia amesema nchi hiyo iko katika ule mkondo ambao ulikuwa umechukuliwa na Shirikisho la Sovieti baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia na ni mkondo ambao hatimaye ulipelekea shirikisho hilo kusambaratika.

Putina halikadhalika amekosoa sera za maamuzi ya upande mmoa na utumiaji mabavu ambazo zinashuhudiwa Marekani hata baada ya kuondoka madarakani Donald Trump. Amesema kinyume na anavyodai, Rais Joe Biden wa Marekani anatekeleza sera za utumiaji mabavu na kutoa vitisho kwa nchi zingine na anatumia vikwazo kama silaha ya kuwashinikiza wengine.

Kuhusiana na nukta hiyo, Putin ameashiria vikwazo vya hivi karibuni vya Marekani dhidi ya Russia na kusema Marekani inakosea inapodhani kuwa ina nguvu za kukabiliana na tishio kutoka nchi zingine.

Rais Biden wa Marekani akijaribu kuvaa barakoa

Ni wazi kuwa Marekani ingali inaamini ndio dola lenye uwezo mkubwa duniani na hivyo inapinga sera za maamuzi ya pande kadhaa yaani multilateralism na kwa msingi huo inalenga kueneza satwa yake kimataifa kwa kutumia ubabe, mabavu na kuzilazimisha nchi zingine zitii matakwa yake. Mwaka 2019 Putin aliashiria sera za Marekani wakati wa Trump na kukumbusha kuwa muundo wa Vita Baridi ulikuwa umeshatoweka duniani huku akiongeza kuwa, sera za Marekani zinavuruga amani na kuhatarisha usalama wa dunia. Alisema mashinikizo ya kiuchumi na kisiasa ya Marekani dhidi ya nchi zingine ni kinyume cha sheria za kimataifa.

Nukta nyingine muhimu katika matamshi ya Putin ni kuwa,  hii ni  mara ya kwanza kwa Rais wa Russia kuonya kuwa mwelekeo ambao Marekani imechukua unashabihiana na ule wa Shirikisho la Sovieti na hivyo ni wazi kuwa iwapo Washington itaendeleza sera zake za sasa, basi hatima yake ni kuangamia.

Shirikisho la Sovieti lilisambaratika mwaka 1991 baada ya miaka sabini ya uhai wake na huo ukawa mwisho wa Vita Baridi duniani.

Muadhui ya kuanza kudhoofika Marekani hatua kwa hatua imekuwa ikijadiliwa kwa miaka kadhaa sasa na wasomi pamoja na weledi wa masuala ya kisiasa katika uga wa kimataifa. Maudhui hii haitajwi tu na nchi zinazohasimiana na Markani bali hata taasisi za kielimu na kisiasa katika nchi za Magharibi zimekuwa zikijadili kadhia hii kwa muda mrefu sasa.

Wanamgambo watiifu kwa rais wa zamani wa Marekani Donald Trump wakiwa wamejizatiti kwa silaha

Moustafa Khoshcheshm mtaalamu wa masuala ya Marekani anasema kusambaratika Marekani si nadharia bali ni mchakato ambao ulianza muda mrefu.

Wahakiki wanasema uwezo wa Marekani unazidi kudhoofika na kudidimia ndani na nchi na pia nje ya nchi hiyo. Kwa mfano ndani ya Marekani kuna migogoro mikubwa ya  kiuchumi na kijamii na hata kiusalama kutokana na kuenea ugaidi wa ndani ya nchi huku kukiwa kumeibuka ufa mkubwa wa hitilafu za kirangi baina ya Wazungu na wasiokuwa wazungu, na pia hitilafu za kitabaka nazo zimeshadidi.

Katika uga wa kimataifa pia tunashuhudia kupungua nguvu na uwezo wa Marekani katika sekta za nguvu za kijeshi na pia  kiuchumi. 

Hivi sasa kwa kuzingatia kufeli sera na mikakati ya Marekani, Putin ametabiri kuwa, Marekani hatimaye itakumbwa na hatima sawa na ile ya Shirikisho la Sovieti, yaani kusambaratika kikamilifu.