Amnesty International: Ukandamizaji umeongezeka sana nchini Saudi Arabia
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limetangaza kuwa, Saudi Arabia imezidisha ukandamiza dhidi ya raia baada ya kumalizika muda wa uenyekiti wake katika kundi la G20.
Taarifa iliyotolewa leo na Amnesty International imesema baada ya kupungua ukandamizaji wa raia kukikoandamana na Saudi Arabia kuwa mwenyekiti wa kundi la G20 hapo mwaka 2020, kuanzia mwanzoni mwaka huu Riyadh imezidisha tena ukandamizaji na unyanyasaji wa wapinzani na watetezi wa haki za binadamu.
Naibu Mkurugenzi wa Amnesty international kanda ya Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika, lynn Maalouf amesema kuwa, baada tu ya kumalizika kipindi cha uenyekiti wa Saudi katika G20, maafisa wa serikali ya Riyadh walianza kutekeleza mienendo yao ya kikatili dhidi ya watu waliofanya ujasiri wa kutoa maoni huru au kukosoa utawala wa kifalme wa nchi hiyo.
Amnesty international imeongeza kuwa, japokuwa hukumu za kifo zilipungua kwa asilimia 85 mwaka jana nchini Saudia lakini watu wasiopungua 40 walinyongwa nchini humo katika kipindi cha baina ya Januari na Julai mwaka huu wa 2021 na kiwango hicho peke yake ni kikubwa zaidi ikilinganishwa na mwaka mzima wa kabla yake.
Mashirika mengi ya kutetea haki za binadamu likiwemo la Human Rights Watch yamekuwa yakipinga na kukosoa ukandamizaji wa uhuru wa kujieleza na adhabu za kunyongwa na kuswekwa jela wapinzani wa serikali na watetezi wa haki za binadamu nchini Saudi Arabia.
Mashirika hayo yanasisitiza kuwa Saudi Arabia ni miongoni mwa tawala zinazoongoza duniani kwa ukandamizaji na ukiukaji wa haki za binadamu.