Hofu ya Baraza la Usalama ya kuenea ugaidi barani Afrika
Nchi wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa zimeleeza wasi wasi wao juu ya kuenea harakati za makundi ya kigaidi katika nchi za Afrika.
Vladimir Voronkov, Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Ofisi ya Kupambana na Ugaidi ya Umoja wa Mataifa (UNOCT) amesema kundi la kigaidi la ISIS/Daesh limepanua satua yake katika nchi za Afrika kuanzia Mali, Burkina Faso, Niger, Nigeria, Chad hadi Cameroon huko Magharibi mwa Afrika.
Amesema wanachama wa kundi hilo wamejipenyeza na kuendeleza harakati zao pia katika nchi za Msumbiji, kusini mwa Afrika na Tanzania, huko mashariki mwa bara hilo.
Katika taarifa, Baraza la Usalama la UN limesema, kuongezeka harakati za kundi hilo katika nchi za Afrika kutakuwa na matokeo mabaya kwa amani, uthabiti na usalama wa eneo.
Vladimir Voronkov, Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Ofisi ya Kupambana na Ugaidi ya Umoja wa Mataifa ameeleza bayana kuwa, ISIS ni tishio kuu kwa amani na usalama wa dunia, na kwa msingi huo jamii ya kimataifa inapaswa kutoa 'jibu la kimataifa' dhidi ya kundi hilo.
Mwezi uliopita, wataalamu wa Umoja wa Mataifa walisema katika ripoti yao mpy kuwa, bara la Afrika limekuwa muhanga mkuu wa ugaidi katika nusu ya kwanza ya mwaka huu wa 2021 kutokana na kuenea makundi ya kigaidi kama Daesh na al-Qaida, na kwamba magenge hayo yana uwezo mkubwa wa kujidhaminia fedha na kutumia silaha za kisasa ikiwa ni pamoja na ndege zisizo na rubani kwa ajili ya kufikia malengo yao ya kigaidi.