EU yataja masharti ya kuwa na mawasiliano na Taliban
Mkuu wa Sera za Kigeni za Umoja wa Ulaya amedai kuwa EU haitalitambua rasmi kundi la Taliban, na badala yake amelipa kundi hilo masharti matano ya kuweza kuwa na mawasiliano nalo, eti kwa maslahi ya wananchi wa Afghanistan.
Josep Borrell alitaja masharti hayo yatakayoiwezesha EU kuwa na eti 'mawasiliano ya kioperesheni' na Taliban jana Ijumaa katika kikao na waandishi wa habari mjini Brdo, Slovenia baada ya kufanyika mkutano usio rasmi wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya.
Amebainisha kuwa: Mustakabali wa Afghanistan linasalia kuwa suala nyeti kwetu. (Mustakabali huo) unatuathiri sisi, eneo na uthabiti wa dunia, kama ambavyo una mfungamano wa moja kwa moja na usalama wa Ulaya.
Baadhi ya masharti hayo ya EU kwa Taliban yanasema; Mosi, EU inataka hakikisho la serikali ya Afghanistan kwamba nchi hiyo hatageuka kuwa kitovu cha 'ugaidi wa kimataifa; na pia itafuatilia kuona iwapo utawala mpya nchini humo unaheshimu utawala wa sheria na haki za binadamu hususan haki za wanawake.
Aidha EU inaitaka Taliban iunde serikali jumuishi, mbali na kuruhusu misaada ya kibinadamu kuingizwa nchini humo; na vile vile kuheshimu ahadi yake ya kuruhusu raia wa kigeni na Waafghani walio katika hatari wanaondoka nchini humo.
Marekani na waitifaki wake wamelazimika kukimbia Afghanistan baada ya uvamizi wao wa miaka 20 kutozaa matunda yoyote isipokuwa kupata nguvu ugaidi, vita, ukatili, machafuko, ukosefu wa amani na utulivu pamoja na mauaji ya mamia ya maelfu ya wananchi wa Afghanistan.