Mvutano katika uhusiano wa Algeria na Ufaransa
https://parstoday.ir/sw/news/world-i75352-mvutano_katika_uhusiano_wa_algeria_na_ufaransa
Usiku wa Jumamosi iliyopita serikali ya Algeria ilimwita nyumbani balozi wake nchini Ufaransa kwa ajili ya mashauriano ikilalamikia matamshi yaliyotolewa na Rais Emmanuel Macron dhidi ya nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 03, 2021 13:43 UTC
  • Mvutano katika uhusiano wa Algeria na Ufaransa

Usiku wa Jumamosi iliyopita serikali ya Algeria ilimwita nyumbani balozi wake nchini Ufaransa kwa ajili ya mashauriano ikilalamikia matamshi yaliyotolewa na Rais Emmanuel Macron dhidi ya nchi hiyo.

Katika matamshi yake ya karibuni, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa alikosoa historia rasmi ya Algeria na kusema inahitajia kuandikwa upya.

Macron alihoji kuwa, je, kabla ya ukoloni wa Ufaransa kulikuwepo taifa linalojulikana kama Algeria? Vilevile alidai kuwa Rais wa Algeria Abdelmadjid Tebboune anaathiriwa na watu wa kandokando yake. Macron pia alitahadharisha kuhusu athari mbaya za kueneza chuki dhidi ya Ufaransa nchini Algeria.

Gazeti la Ufaransa la Le Monde lilimnukuu Emmanuel Macron akidai kwamba, historia ya Algeria haijajengeka katika msingi wa ukweli na uhakika bali kwa misingi wa fikra za chuki dhidi ya Ufaransa.

Matamshi hayo ya Rais wa Ufaransa yamezusha mwangwi mkubwa sana nchini Algeria. Kwa sababu hiyo Algiers imemwita nyumbani balozi wake nchini Ufaransa na wakati huo huo Ofisi ya Rais wa Algeria imelaani vikali matamshi hayo ya Macron. Vilevile Rais Abdelmadjid Tebboune wa Algeria amepiga marufuku ndege za kivita za Ufaransa zinazoshiriki katika Operesheni Barkhane katika eneo la Sahil barani Afrika, kutumia anga ya nchi hiyo. 

Mvutano baina ya Ufaransa na Algeria una historia ndefu. Katika kipindi kirefu cha kuwepo kwao nchini Algeria, Wafaransa walipora mali na utajiri wa nchi hiyo sambamba na kufanya jinai za kutisha ikiwa pamoja na mauaji ya halaiki dhidi ya raia wa Algeria. Kifichuliwa na kuwekwa wazi jinai na ukatili uliofanywa na Wafaransa nchini Algeria katika miezi ya karibuni kumewafedhehesha maafisa wa serikali ya Paris kiasi kwamba, mwezi uliopita Rais Emmanuel Macron alilazimika kuomba rasmi kutokana na jinai na uhalifu uliofanywa na nchi yake huko Algeria.

Waalgeria wasiopungua milioni 1.5 waliuawa wakati wa ukoloni wa Ufaransa

Takwimu zilizotolewa karibuni zinaonesha kuwa, zaidi ya Waalgeria milioni moja na nusu waliuawa katika kipindi cha ukoloni wa Ufaransa na wakati wa vita vya ukombozi wa nchi yao. Vilevile kufichuliwa jinai za Wafaransa wakati wa majaribio ya silaha za nyuklia yaliyofanyika katika maeneo ya jangwani nchini Algeria na kusababisha maafa makubwa ambayo yangali yanaendelea hadi hii leo, kumezidisha ghadhabu na hasira ya Waalgeria dhidi ya mkoloni huyo wa zamani. Katika mojawapo ya majaribio hayo ya nyuklia, Wafaransa waliwatumia raia 150 wa Algeria kama mapanya wa maabara ili kupima taathira za mionzi ya nyuklia kwa mwili wa mwanadamu. Mkuu wa kundi la Watetezi wa Wahanga wa Nyuklia nchini Algeria Abdul Rahman Tumi anasema: "Magonjwa yanayosababishwa na mionzi ya nyuklia ya majaribio ya Wafaransa nchini Algeria yanaendelea kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kizazi kingine."

Rais wa Algeria walitumiwa na Wafaransa kama 'panya wa maabara' katika majaribio ya nyuklia

Hata hivyo Ufaransa imekuwa ikishughulikia kadhia hiyo kwa siasa zake makhsusi. Katika miaka ya nyuma maafisa wa serikali ya Paris walikuwa wakikana uhalifu na jinai hiyo. Lakini miaka ya karibuni na baada ya kuwekwa wazi nyaraka za kihistoria za jinai na uhalifu huo wa Ufaransa nchini Algeria, Rais Emmanuel Macron na kwa shabaha ya kulinda hadhi ya nchi hiyo mbele ya fikra za walimwengu, amelazimika kuungama na kukiri kwamba nchi yake ilifanya uhalifu nchini Algeria. Wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka 2017 pia Macron alisema: "Majaribio ya nyuklia ya Ufaransa nchini Algeria yalikuwa jinai dhidi ya binadamu na ukatili halisi. Hii ni sehemu ya historia yetu tunayopaswa kuiangalia na kuwaomba radhi wale tuliowafanyia ukatili huo."

Pamoja na hayo katika kipindi chote cha miaka minne ya utawala wake huko Ufaransa, Macron amekuwa na misimamo tofauti na ya kigeugeu. Kwa sasa ambapo Ufaransa inakaribia uchaguzi wa rais na kwa kutilia maanani kupungua kwa umaarufu wake yeye na chama chake baina ya Wafaransa, Macron anafanya mikakati ya kupata ridhaa na uungaji mkono wa vyama na makundi ya kisiasa kupitia njia ya kufunika, kuficha au hata kupotosha ukweli wa kihistoria na dhulma za ukoloni wa nchi yake dhidi ya mataifa ya Afrika ikiwemo Algeria. Suala hili yumkini likavuruga uhusiano wa Paris na nchi nyingine.