Ufaransa yataka kuondolewa mivutano katika uhusiano wake na Algeria
https://parstoday.ir/sw/news/world-i75432-ufaransa_yataka_kuondolewa_mivutano_katika_uhusiano_wake_na_algeria
Rais wa Ufaransa ametoa wito wa kuondolewa mivutano katika uhusiano wa nchi hiyo na Algeria.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Oct 05, 2021 23:36 UTC
  • Emmanuel Macron
    Emmanuel Macron

Rais wa Ufaransa ametoa wito wa kuondolewa mivutano katika uhusiano wa nchi hiyo na Algeria.

Emmanuel Macron ambaye alikuwa akizungumza na Redio ya Taifa ya Ufaransa ameeleza matumaini ya kupungua mivutano iliyopo katika uhusiano wa Paris na Algiers na kusema, kuna hitilafu za kimitazamo baina ya pande mbili lakini zinaweza kutatuliwa kupitia njia ya mazungumzo. 

Hitilafu baina ya pande hizo mbili zilipamba moto zaidi siku kadhaa zilizopita baada ya Rais huyo wa Ufaransa kushambulia historia rasmi ya Algeria na kusema inahitaji kuandikwa upya.

Macron alihoji kuwa, je, kabla ya ukoloni wa Ufaransa kulikuwepo taifa linalojulikana kama Algeria? Vilevile alidai kuwa Rais wa Algeria Abdelmadjid Tebboune anaathiriwa na watu wa kandokando yake. 

Emmanuel Macron pia alidai kwamba, historia ya Algeria imejengeka katika msingi wa fikra za chuki dhidi ya Ufaransa na si msingi ukweli na uhakika.

Ofisi ya Rais wa Algeria imetoa taarifa ikijibu matamshi hayo na kusema kuwa maneno ya Macron ni dharau dhidi ya mamilioni ya Waalgeria. 

Rais Abdelmadjid Tebboune wa Algeria

Algiers pia imemwita nyumbani balozi wake nchini Ufaransa kwa ajili ya mashauriano. Vilevile Rais Abdelmadjid Tebboune wa Algeria amepiga marufuku ndege za kivita za Ufaransa zinazoshiriki katika Operesheni Barkhane katika eneo la Sahil barani Afrika, kutumia anga ya nchi hiyo.