Ilhan Omar: Uamuzi wa Marekani kuiuzia silaha Saudi Arabia haukubaliki
(last modified Fri, 12 Nov 2021 02:23:10 GMT )
Nov 12, 2021 02:23 UTC
  • Ilhan Omar: Uamuzi wa Marekani kuiuzia silaha Saudi Arabia haukubaliki

Mbunge wa chama cha Democratic katika Baraza la Wawakilishi la Marekani amesema, hatua ya nchi hiyo kuiuzia silaha Saudi Arabia haikubaliki kutokana na silaha hizo kutumika kuulia raia wa Yemen.

Akizungumzia misimamo ya ukosoaji dhidi ya uamuzi wa serikali ya Joe Biden wa kuidhinisha mauzo mapya ya silaha kwa Saudia zenye thamani ya dola milioni 650 wakati nchi hiyo inaendelea kuua raia wa Yemen, Ilhan Omar amesema, kuiuzia silaha Saudi Arabia ilhali inaendelea kuua raia wa Yemen hakukubaliki.

Mbunge huyo wa chama tawala cha Democratic ameongezea kwa kusema: "kama kweli tunaitakidi kwamba haki za binadamu ni kipaumbele katika sera zetu za nje hatuwezi kuwapatia silaha wakiukaji wa haki za binadamu."

Maafa yanayosababishwa na vita vya Saudi Arabia dhidi ya Yemen

 

Hivi karibuni, wizara ya mambo ya nje ya Marekani ilitangaza kuwa imeafiki kuiuzia Saudi Arabia makombora ya anga kwa anga yenye thamani ya dola milioni 650 pamoja na zana zinazohusika nazo. Washington imedai kuwa, uuzaji wa makombora hayo kwa Saudia utaisaidia kujilinda na ndege zisizo na rubani za nje ya mipaka ambazo zimehatarisha maisha ya wafanyakazi wa kijeshi wa Saudia na Marekani.

Hatua ya Marekani ya kuidhinisha mauzo hayo mapya ya silaha kwa Saudi Arabia inakinzana na ahadi aliyokuwa ametoa rais Joe Biden ya kuhitimisha vita dhidi ya Yemen na kuzuia Saudia kupatiwa silaha za mashambulio.../

Tags