Waliouawa katika ghasia za Kazakhstan wapindukia 160
(last modified Sun, 09 Jan 2022 13:31:00 GMT )
Jan 09, 2022 13:31 UTC
  • Waliouawa katika ghasia za Kazakhstan wapindukia 160

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Kazakhstan imetangaza kuwa, watu 160 wakiwemo maafisa usalama wameuawa tangu kuanza kwa machafuko katika nchi hiyo ya Asia ya Kati wiki moja iliyopita.

Watu hao wameuawa katika makabiliano ya siku kadhaa baina ya waandamanaji na maafisa usalama. Wananchi wa Kazakhstan walianzisha maandamano ya ghasia ya kulalamikia hatua ya serikali ya kupandisha bei ya mafuta.

Wizara hiyo imesema watu zaidi ya elfu tano wametiwa mbaroni kwa kufanya maandamano ya fujo kinyume cha sheria, kuwashambulia maafisa usalama, na kuharibu mali za umma.

Taarifa ya wizara hiyo imesema ghasia hizo zimelisababishia taifa hilo hasara ya takriban dola milioni 200, kushambuliwa na kuibiwa benki na maeneo ya biashara, mbali na kuchomwa moto magari zaidi ya 400.

Sehemu ya athari za maandamano ya fujo mjini Almaty, Kazakhstan

Wizara ya Afya ya nchi hiyo imenukuliwa ikisema kuwa, watu 164 wakiwemo watoto wadogo wawili na maafisa usalama zaidi ya 20 wameuawa kwenye fujo hizo.

Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Ndani wa nchi hiyo, Erlan Turgumbayev amesema hali ya utulivu, nidhamu na utawala wa kikatiba imerejeshwa katika maeneo karibu yote ya nchi hiyo, lakini operesheni za kupambana na 'ugaidi' zingali zinaendelea.