Tamasha la sanaa Ufaransa lafutiwa ruzuku kwa mchoro wa hijabu
https://parstoday.ir/sw/news/world-i79780-tamasha_la_sanaa_ufaransa_lafutiwa_ruzuku_kwa_mchoro_wa_hijabu
Serikali ya jimbo la Auvergne-Rhone-Alpes nchini Ufaransa imelisimamishia ruzuku kundi moja la wasanii wanaoandaa tamasha la sanaa mjini Grenoble, kwa kujumuisha mchoro wa mwanamke aliyevaa hijabu katika kazi zao.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 30, 2022 04:31 UTC
  • Tamasha la sanaa Ufaransa lafutiwa ruzuku kwa mchoro wa hijabu

Serikali ya jimbo la Auvergne-Rhone-Alpes nchini Ufaransa imelisimamishia ruzuku kundi moja la wasanii wanaoandaa tamasha la sanaa mjini Grenoble, kwa kujumuisha mchoro wa mwanamke aliyevaa hijabu katika kazi zao.

Taarifa ya serikali ya jimbo hilo la kusini mashariki mwa Ufaransa imedai kuwa, mchoro huo wa mwanamke aliyevaa vazi la stara linalovaliwa na wanawake Waislamu ni wa kichochezi na usiokubalika.

Imesema tamasha hilo la sanaa halitapewa ruzuku ya Yuro 10,000 kama ilivyokuwa imepangwa kutokana na mchoro huo, ikisisitiza kuwa picha ya mwanamke huyo aliyevaa hijabu haina umuhimu wowote isipokuwa kuwafaidi wenye misimamo ya chuki, na kuchochea chuki na ghasia. 

Haya yanajiri siku kadhaa baada ya Baraza la Seneti la Ufaransa kupiga kura na kuidhinisha sheria inayopiga marufuku wanawake Waislamu kuvaa vazi la stara na heshima la hijabu katika mashindano ya michezo. 

Katika miezi ya hivi karibuni Ufaransa imeshadidisha mbinyo dhidi ya Waislamu nchini humo ambapo hata maduka ya Waislamu yanafungwa kwa visingizio mbali mbali.

Mwezi Julai mwaka jana 2021, Bunge la nchi hiyo ya Ulaya lilipasisha sheria tata ambayo inawakandamiza Waislamu na kubana sheria kuhusu ufadhili wa misikiti na jumuiya za Waislamu.