Waafghani waandamana kulaani wizi wa mabilioni uliofanywa na Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i80314-waafghani_waandamana_kulaani_wizi_wa_mabilioni_uliofanywa_na_marekani
Wananchi wa Afghanistan wamefanya maandamano katika mji mkuu wa nchi hiyo, Kabul, kulalamikia kitendo cha hatua ya Marekani ya kupora mabilioni ya dola za Afghanistan na kuzitumia kuwalipa wanaodai fidia kutokana na mashambulizi ya Septamba 11 mwaka 2001.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Feb 13, 2022 12:45 UTC
  • Waafghani waandamana kulaani wizi wa mabilioni uliofanywa na Marekani

Wananchi wa Afghanistan wamefanya maandamano katika mji mkuu wa nchi hiyo, Kabul, kulalamikia kitendo cha hatua ya Marekani ya kupora mabilioni ya dola za Afghanistan na kuzitumia kuwalipa wanaodai fidia kutokana na mashambulizi ya Septamba 11 mwaka 2001.

Waandamanaji hao waliokusanyika nje ya Msikiti wa Jamia wa Eid Gah jijini Kabul, wameutaka utawala wa Washington kutoa fidia kwa makumi ya maelfu ya Waafghani waliouawa katika uvamizi na vita vya Marekani nchini Afghanistan katika kipindi cha miaka 20 iliyopita.

Baadhi ya mabango yaliyokuwa yamebebwa na wananchi hao wa Afghanistan yalikuwa na jumbe zinazoutaka utawala wa Rais Joe Biden wa Marekani kulirejeshea fedha zake taifa hilo linalokabiliwa na mgogoro mkubwa wa kiuchumi.

Siku ya Ijumaa Ikulu ya White House ilitangaza kuwa utawala wa Joe Biden unapanga kuchukua kwa mabavu nusu ya dola bilioni saba fedha za Afghanistan zinazoshikiliwa katika benki za Marekani na kuzigawa kwa familia za walioathirika na mashambulizi ya 9/11.

Maandamano ya Waafghani mjini Kabul

Hii ni katika hali ambayo miongoni mwa waliotekeleza mashambulizi ya Septemba 11 hapakuwa hata raia mmoja wa Afghanistan. Serikali ya Taliban nchini Afghansitan imelaani vikali hatua hiyo ikisisitiza kuwa, wizi huo ni dalili ya kuporomoka maadili ya Marekani.

Suhail Shaheen aliyeteuliwa kuwa mwakilishi wa serikali ya Taliban katika Umoja wa Mataifa amekosoa uamuzi huo wa Marekani na kusema fedha hizo zote zinapaswa kuachiliwa na kukabidhiwa Benki Kuu ya Afghanistan kwani ni mali ya Waafghani.