Marine Le Pen ashambulia tena Uislamu na vazi la hijabu
https://parstoday.ir/sw/news/world-i80450-marine_le_pen_ashambulia_tena_uislamu_na_vazi_la_hijabu
Mgombea uraisi wa Ufaransa wa chama cha kitaifa cha Rassemblement chenye siasa kali za mrengo wa kulia kwa mara nyingine ameeleza upinzani wake dhidi ya vazi la hijabu la wanawake wa Kiislamu.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Feb 17, 2022 08:04 UTC
  • Marine Le Pen
    Marine Le Pen

Mgombea uraisi wa Ufaransa wa chama cha kitaifa cha Rassemblement chenye siasa kali za mrengo wa kulia kwa mara nyingine ameeleza upinzani wake dhidi ya vazi la hijabu la wanawake wa Kiislamu.

Marine Le Pen amesema katika mahojiano yake ya leo Alkhamisi na televisheni ya LSE kwamba "tunapaswa kupinga vazi la hijabu hadharani."

Le Pen ambaye ni mashuhuri kwa kupiga vita Uislamu, ameongeza kuwa hijabu sio tu ishara ya wazi la kidini bali pia ni aina ya sare.

Mgombea huyo wa urais wa Ufaransa amedai kuwa vazi la hijabu linakiuka uhuru, na kusema baadhi ya wasichana wamemwambia kuwa wamechagua vazi la hijabu kwa uhuru na hiari yao, lakini hadhani kwamba mtu anaweza kuweka kando uhuru kwa hiari yake.

Hujuma dhidi ya Uislamu na Waislamu zimepamba moto nchini Ufaransa katika siku hizi za kukaribia uchaguzi wa rais nchini humo. 

Uwezekano wa kushinda wagombea wenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia katika uchaguzi ujao wa rais wa Ufaransa umeibua wasiwasi kuhusu kushadidi siasa za chuki dhidi ya Uislamu nchini humo.

Siku chache zilizopita mgombea mwingine wa kiti cha urais nchini Ufaransa mwenye siasa kali za mrengo wa kulia alitangaza tena ajenda na mipango yake kuhusu dini ya Kiislamu, ambayo amesema ataitekeleza iwapo ataingia Ikulu ya Elysee.

Éric Zemmour

Éric Zemmour, ambaye amekuwa maarufu kwa jina la 'Trump wa Ufaransa' amesisitiza kwa mara nyingine tena kwamba, miongoni mwa mipango atakayoitekeleza ikiwa atashinda kiti cha urais ni kufunga misikiti na kupiga marufuku vazi la hijabu.

Duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais wa Ufaransa itafanyika Aprili 10, mwaka huu wa 2022 na duru ya pili kati ya wagombea wawili wa juu itafanyika Aprili 24.