Feb 20, 2022 08:01 UTC
  • Familia yalaani hukumu 'laini' dhidi ya polisi mzungu aliyeua kijana mweusi US

Wanasheria na familia ya kijana mwenye asili ya Afrika aliyeuawa na polisi mzungu nchini Marekani mwaka jana wamelaani vikali kitendo cha kuhukumiwa kifungo cha miaka miwili pekee askari huyo muuaji katika mji Minneapolis.

Inaelezwa kwamba afisa huyo wa zamani wa polisi anayefahamika kama Kim Potter alitenda jinai hiyo Aprili 11 mwaka jana, katika hali ambayo kijana huyo mweusi aliyemuua kwa jina la Daunte Wright alikuwa hana silaha yoyote wakati wa tukio hilo.

Afisa huyo wa Kituo cha Polisi cha Brooklyn katika jiji la Minneapolis jimboni Minnesota alimpiga risasi kijana huyo baada ya kusimamisha gari lake, eti kwa kosa la kutumia leseni ambayo imepitwa na wakati, na pia kwa kuning'iniza kikopo cha manukato kwenye kioo cha gari hilo.

Afisa huyo anadai kuwa alitoa bastola kimakosa, akidhani ni kifaa chake cha kuwapiga shoti washukiwa (taser) wanaoleta usumbufu wakati wa kukamatwa.

Hata hivyo, Ben Crump, wakili wa familia ya kijana huyo mweusi amesema, kilichoshuhudiwa katika utoaji wa hukumu hiyo, kinadhihirisha wazi uozo wa ubaguzi katika mfumo wa sheria na idara ya mahakama nchini Marekani.

Maandamano ya kupinga ubaguzi na ukatili dhidi ya watu weusi Marekani

Mmano Machi 2019, maandamano makubwa yalifanyika katika jimbo la Pennsylvania baada ya kamati ya usawa ya mahakama ya mji wa Pittsburgh katika jimbo hilo kumfutia mashitaka afisa wa zamani wa polisi kwa jina la Michael Rosfeld, aliyemuua bila ya hatia kijana mwenye asili ya Kiafrika aliyetambuliwa kwa jina la Antwon Rose. Kabla ya hapo, mwendesha mashtaka wa jimbo la California aliwaachia huru polisi wawili waliohusika kumuua kijana mwingine mwenye asili ya Afrika katika mji wa Sacramento jimboni hapo.

Mienendo hiyo isiyo ya kiuadilifu ya polisi na vyombo vya mahkama nchini Marekani dhidi ya jamii Wamarekani weusi, imekuwa ikilalamikiwa vikali katika maeneo tofauti ya nchi hiyo inayojidai kuwa mtetezi wa haki za binaadamu duniani.

Tags