China yaitaka Uingereza iachane na fikra za kikoloni
https://parstoday.ir/sw/news/world-i82070-china_yaitaka_uingereza_iachane_na_fikra_za_kikoloni
Serikali ya China imelaani vikali uingiliaji wa Uingereza katika masuala ya ndani ya mji wa Hong Kong na kusisitiza kuwa, nchi hiyo ya Ulaya inapaswa kuachana na fikra zake za kikoloni.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Apr 02, 2022 22:11 UTC
  • China yaitaka Uingereza iachane na fikra za kikoloni

Serikali ya China imelaani vikali uingiliaji wa Uingereza katika masuala ya ndani ya mji wa Hong Kong na kusisitiza kuwa, nchi hiyo ya Ulaya inapaswa kuachana na fikra zake za kikoloni.

Zhao Lijian, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China amesema serikali ya Beijing inapinga vikali ripoti ya kichochezi na kichokozi iliyotolewa hivi karibuni na Uingereza kuhusu hali ya mambo katika mji wa Hong Kong.

Lijian ameeleza bayana kuwa, kadhia ya Hong Kong ni ya ndani ya China na hivyo Uingereza haipaswi kujiingiza katika suala hilo. Amesema London haina mamlaka, uwezo na haki ya kisheria ya 'kusimamia' masuala ya Hong Kong.

Matamshi ya Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya China ni jibu kwa ripoti hiyo ya UK, ambayo hutolewa kila baada ya miezi sita, ikikosoa eti sera za China mkabala wa Hong Kong.

Zhao Lijian, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China

Wizara ya Mambo ya Nje ya China inasema uingiliaji wa mara kwa mara wa Marekani na Uingereza kwenye masuala ya Hong Kong utakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa watu wote wa China ikiwa ni pamoja na wale wa Hong Kong.

China imesisitiza mara kadhaa kuwa, kamwe serikali ya nchi hiyo haitovumilia harakati za kujitenga eneo la Hong Kong.

Wamagharibi wamekuwa wakitumia maandamano na malalamiko ya wakazi wa Hong Kong kama wenzo wa kuzidisha mashinikizo dhidi ya China kwa kuihumu kuwa inafumbia macho matakwa ya wakazi wa jiji hilo na kudhoofika mwenendo wa kidemokrasia nchini humo.