Onyo jipya la kijeshi la Marekani kwa China
(last modified Mon, 25 Apr 2022 02:18:21 GMT )
Apr 25, 2022 02:18 UTC
  • Onyo jipya la kijeshi la Marekani kwa China

Mashindano ya kijeshi na kiusalama baina ya Marekani na China katika eneo la Indo-Pasifiki yamechukua muelekeo mpya kutokana na jitihada za pande mbili za kujiimarisha kijeshi katika eneo hilo muhimu kistratijia.

Kuhusiana na nukta hiyo, Ikulu ya White House imetoa onyo kuhusu uwepo kijeshi wa China katika Visiwa vya Suleiman na imesema itatoa jibu kwa hatua hiyo. Visiwa vya Suleiman au Visiwa vya Solomon ni nchi ya visiwani ya Melanesia katika Bahari ya Pasifiki iliyoko mashariki kwa Papua Guinea Mpya. Eneo lake ni visiwa karibu 1000. Baada ya Mapatano ya Marekani na Visiwa vya Suleiman kuhusu kuanza mazungumzo katika ngazi za juu, Ikulu ya White House imetoa taarifa na kusema: "Iwapo kutachukuliwa hatua za kujenga kituo cha kijeshi cha kudumu cha China katika visiwa hivi, Washington itatoa jibu kwa hatua hiyo.  Katika kipindi hiki hasasi, Marekani imeafikiana na Visiwa vya Suleiman kuhusu kufanya mazungumzo ya ngazi za juu ya kistratijia chini ya usimamizi wa Ikulu ya White House na Wizara ya Mambo ya Nje ya visiwa hivyo.''

Siku ya Jumanne, China ilitangaza kuwa imetia saini mapatano ya usalama na Visiwa vya Suleiman. Hatua hii inayotajwa kuwa ya aina yake imekabiliwa na radiamali hasi ya Marekani.

 

Hatua ya China kimsingi inamaanisha kuwa kwa mara ya kwanza baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia, China itaweza kuweka wanajeshi wake katika eneo ambalo limekuwa ngome ya kijitanua kijeshi Marekani.

Hatua hiyo imeibua wasiwasi mkubwa Marekani na pia miongoni mwa waitifaki wake katika Bahari ya Pasifiki Kusini yaani Australia na New Zealand. Madola hayo matatu yana wasiwasi mkubwa kuuhusu kuenea satwa na ushawishi wa China katika eneo hilo. Pamoja na hayo viongozi wa Visiwa vya Suleiman wana mtazamo tafauti na Marekani na washirika wake.

Manasseh Sogavare Waziri Mkuu wa Visiwa vya Suleiman ameliambia bunge la nchi hiyo kuwa: "Uamuzi wa viongozi wa Visiwa vya Suleiman wa kutia saini mapatano ya usalama na China hautadhuru, kuvuruga au kudhoofisha amani katika eneo."

Pamoja na kuwepo msimamo huu wa serikali ya Visiwa vya Suleiman, lakini Marekani imepinga mapatano hayo ya usalama na imesema ina wasiwasi kuwa uhusiano na ushirikiano wa karibu wa China na Visiwa vya Suleman ni jambo ambalo linaandaa ushawishi zaidi wa China katika eneo la Indo-Pasifiki.

 Adrian Watson Msemaji wa Baraza la Usalama wa Taifa Marekani amesema wakuu wa Marekani, Japan, Australia na New Zealand wana wasiwasi kuhusu mapatano ya usalama ya China na Visiwa vya Suleiman na kudai kuwa mapatano hayo yanaweza kuwa ni hatari kubwa kwa usalama wa Bahari ya Hindi na Bahari ya Pasifiki.

Hatua ya China kueneza ushawishi wake wa kijeshi katika eneo la Indo-Pasikifi ni jibu kwa taharuki za Marekani katika eneo hilo. 

Katika zama za utawala wa Joe Biden, kwa kisingizio cha kukabiliana na tishio la China, Marekani imelekeza sera zake za kigeni katika eneo la kistratijia la Indo-Pasifiki na imekuwa ikiunda muungano wa kijeshi dhidi ya China katika eneo hilo. Moja ya hatua za kichochezi ambazo Marekani imechukua dhidi ya China ni kuunda muungano wa kiusalama wa pande nne ujulikanao kama QSD ambao unajumuisha Marekani, Australia, Japan na India. Aidha, Marekani imeunda muungano mwingne wa kiusalama katika eneo hilo ujulikanao kama AUKUS  ambao unajumuisha Marekani, Uingereza na Australia. Miungano hii ya kijeshi inayoongozwa na Marekani imezidisha taharauki katika eneo la Indo-Pasifiki.

Kile kinachodhihirika wazi ni kuwa, Marekani iko tayari  kutoa madai yasiyo na msingi na kutumia nguvu zake zote kukabiliana na China kiuchumi, kibiashara, kiusalama, kijeshi, kisiasa na kiiintaneti.

Mawaziri wa mambo ya nje wa China na Visiwa via Solomon 

 

Jibu la China kwa uchochezi huo wa Marekani limekuwa ni kujiimarisha kijeshi. Kati ya hatua ambazo China imechukua ni kuimarisha uhusiano wa kistratijia na Russia ikiwa ni pamoja na kufanya mazoezi ya pamoja ya kijeshi na nchi hiyo. Hatua ya hivi karibuni ya China kujibu uchochezi wa Marekani ni kuimarisha uwepo wake katika eneo la Indo-Pasikifi kwa kutia saini mapatano ya kijeshi na kiusalama na chi za eneo vikiwemo Visiwa vya Suleiman.