UN yajitenga na mpango wa kuwahamishia wakimbizi wa UK nchini Rwanda
https://parstoday.ir/sw/news/world-i84626-un_yajitenga_na_mpango_wa_kuwahamishia_wakimbizi_wa_uk_nchini_rwanda
Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limejiweka mbali na madai kuwa linaunga mkono mpango wa kuwahamishia Rwanda wakimbizi na watu wanaotafuta hifadhi nchini Uingereza.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 11, 2022 05:50 UTC
  • UN yajitenga na mpango wa kuwahamishia wakimbizi wa UK nchini Rwanda

Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limejiweka mbali na madai kuwa linaunga mkono mpango wa kuwahamishia Rwanda wakimbizi na watu wanaotafuta hifadhi nchini Uingereza.

Laura Dubinsky, wakili wa UNHCR ameituhumu serikali ya London kuwa kidhabi kwa kudai kuwa taasisi hiyo ya Umoja wa Mataifa inaunga mkono mpango huo wa Uingereza kuwapeleka wakimbizi Rwanda.

Wakili huo wa UNHCR aliiambia Mahakama Kuu ya Uingereza jana Ijumaa kuwa, "Hatujawahi kuunga mkono mpango huo wa Rwanda na Uingereza. UNHCR haijahusika kivyovyote na mpango huo licha ya Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza,  Priti Patel kudai kinyume chake."

Hapo jana Jaji wa Mahakama Kuu ya Uingereza, Jonathan Swift aliubariki mpango huo wa serikali ya London wa kuanza kuwahamishia nchini Rwanda wakimbizi wanaoomba hifadhi nchini Uingereza kuanzia Jumanne ijayo.

Wakimbizi wanaopinga kufurushwa UK nje ya Mahakama Kuu

Makubaliano hayo yenye utata baina ya nchi mbili za Rwanda na Uingereza yamelalamikiwa vikali na wabunge wa Uingereza hasa wa chama cha upinzani cha Labour ambao wamesema hautekelezeki na ni kinyume na maadili. 

Makubaliano hayo yamefikiwa baina ya serikali za Kigali na London baada ya Uingereza kushindwa kufikia makubaliano kama hayo na nchi za Kenya, Ghana na Albania. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, serikali ya Rwanda itapewa dola milioni 158 na serikali ya Uingereza katika kile ambacho London inakiita ni ushirikiano mpana wa uhamiaji na maendeleo ya uchumi.