Biden: Lilikuwa kosa kubwa sana kujitoa katika JCPOA
Rais Joe Biden wa Marekani amesema kujitoa nchi yake katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA lilikuwa kosa kubwa sana na akadai kwamba "inapasa turudi tena kwenye JCPOA".
Mazungumzo ya Vienna ya uondoaji vikwazo yalipiga hatua nzuri kutokana na ubunifu uliofanywa na ujumbe wa Iran katika mazungumzo hayo, lakini ucheleweshaji uliofanywa na upande wa Magharibi na hasa serikali ya Biden wa kufidia hatua zilizochukuliwa kinyume cha sheria na serikali iliyotangulia ya Marekani na kuendeleza sera mbovu ya mashinikizo ya juu kabisa dhidi ya Iran viliibua shaka kubwa kuhusu madai ya Washington ya kuwa na nia ya dhati ya kurudi kwenye makubaliano ya JCPOA na hivyo kupelekea kurefuka zaidi mwenendo wa mazungumzo hayo.
Rais wa Marekani ambaye yuko ziarani Palestina inayokaliwa kwa mabavu ameiambia chaneli ya 12 ya televisheni ya utawala wa Kizayuni kuwa, hatua ya mtangulizi wake Donald Trump ya kujitoa kwenye makubaliano ya nyuklia ya Iran lilikuwa kosa kubwa sana na akasema angali anaamini kuwa Washington inapaswa irudi kwenye JCPOA.

Pamoja na hayo, na pasi na kuashiria msimamo wa nchi yake wa kujivutia zaidi upande wake, Biden ameitupia mpira Iran na kudai kwamba, uamuzi wa kufanikisha mapatano hayo uko mikononi mwa Iran.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesisitiza mara kadhaa kuwa endapo itaondolewa vikwazo vyote haramu ilivyowekewa; na pande zingine husika katika JCPOA zikatekeleza ahadi na majukumu yao katika makubaliano hayo, kwa namna ya kuiwezesha kupata manufaa yaliyoainishwa katika JCPOA itarudi tena kutekeleza kikamilifu mapatano hayo ya nyuklia.../