Utafiti: Idadi ya Wakristo inazidi kupungua nchini Australia
Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Takwimu ya Australia umefichua kuwa, Ukristo unazidi kuporomoka nchini humo, huku aghalabu ya raia wa nchi hiyo hakijiarifisha kama watu wasio na dini.
Takwimu za ABS zimeeleza kuwa, Wakristo hivi sasa ni miongoni mwa wafuasi wa dini za walio wachache nchini humo, huku wimbi hilo la kupungua idadi ya wafuasi wa dini hiyo likishuhudiwa pia katika nchi karibu zote za Ulaya Magharibi.
Sensa iliyofanywa mwaka jana nchini humo inaonesha kuwa, kati ya Waaustralia milioni 25, asilimia 43 tu ndio wanaojitambulisha kama Wakristo, kutoka asilimia 52 mwaka 2016, na asilimia 61 mwaka 2011.
Wananchi wa Australia wanaojitambua kuwa hawana dini ni asilimia 39, kutoka asilimia 30 mwaka 2016. Hii ni katika ambayo, sensa hiyo bila ya kuuashiria Uislamu, imesema kuwa idadi ya wafuasi wa dini 'nyinginezo' inaongezeka kwa kasi nchini humo.
Inaarifiwa kuwa, kashfa za kimaadili za viongozi wa Kikristo zimedhoofisha mno imani za Wakristo nchini humo na kuwafanya wapuuze kwenda Makanisani.

Huku hayo yakijiri, dini ya Uislamu imeendelea kukumbatiwa nchini Australia hususan na tabaka la vijana, licha ya wimbi la chuki dhidi ya dini ya Uislamu kuzidi kuongezeka nchini humo.
Wimbi la chuki dhidi ya Uislamu nchini Australia na New Zealand limeshtadi katika miaka ya hivi karibuni ambapo pia kumeshuhudiwa ongezeko la matukio ya mauaji dhidi ya wafuasi wa dini hiyo ya mbinguni katika nchi mbili hizo. Aidha wanawake na wasichana wanaojisitiri kwa vazi la hijabu ndio walengwa wakuu wa wimbi hilo la chuki.