Oct 22, 2022 12:19 UTC
  • Nyaraka nyeti zinazohusiana na Iran zimekutwa kwenye makazi ya Trump Florida

Gazeti la Washington Post limeripoti kuwa nyaraka nyeti zinazohusiana na Iran zimekutwa nyumbani kwa rais wa zamani wa Marekani Donald Trump.

Tarehe 8 Agosti, maafisa ya Polisi ya Upelelezi ya Marekani FBI walivamia makazi ya Trump ya Mar- a-lago mjini Florida na kunasa maboksi 33 ya nyaraka, yakiwemo 11 yenye nyaraka nyeti za siri. Imeelezwa kuwa rais huyo wa zamani wa Marekani aliondoka Ikulu ya White House na nyaraka zisizopungua 300 za siri na kwenda nazo kwenye makazi yake ya Mar-a-laga.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, gazeti la Washington Post limeripoti kuwa, kati ya nyaraka ambazo maafisa wa FBI walizikuta kwenye makazi ya rais wa zamani wa Marekani huko Mar-a-lago Florida walipokwenda kufanya upekuzi miezi michache iliyopita, ni pamoja na nyaraka kadhaa nyeti  zinazohusiana na Iran na China.

Kwa mujibuu wa gazeti hilo la Marekani, kwa uchache, moja ya nyaraka zilizopatikana nyumbani kwa Trump inahusu mpango wa makombora wa Iran na nyaraka nyingine ni ya taarifa za siri kubwa kuhusiana na China.

Msemaji wa Trump hakuwa tayari kujibu wala kueleza chochote kuhusiana na ripoti hiyo iliyotolewa na Washington Post .

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Marekani, Polisi ya Upelelezi ya Marekani FBI inafanya uchunguzi dhidi ya Trump kwa sababu ya kuteketeza nyaraka, kuweka vizuizi vya kukwamisha uchunguzi na kukiuka sheria ya ujasusi ya nchi hiyo.../

Tags