UN yakaribisha usitishaji vita uliotekelezwa na Russia Ukraine
Jan 07, 2023 04:05 UTC
Martin Griffiths, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na Masuala ya Kibinadamu, amesema usitishaji mapigano wa upande mmoja uliotekelezwa na Russia ni fursa ya kutuma misaada ya kibinadamu kwa watu katika maeneo yaliyoathiriwa na vita.
Griffiths ameeleza katika ujumbe wa Twitter: "usitishaji huu wa mapigano unatoa fursa ya kutuma misaada muhimu kwa watu ambao hatujaweza kuwafikia kutokana na mapigano makali."
Vikosi vya ulinzi vya Russia vimetangaza usitishaji vita wa upande mmoja katika maeneo yote ya vita kuanzia saa sita mchana Januari 6 hadi usiku wa manane wa tarehe 7 Januari.
Hata hivyo Ukraine imetupilia mbali pendekezo hilo lililotolewa na Rais Vladimir Putin wa Russia la kusitisha mapigano kwa masaa 36 wakati wa Krismasi ya Kiorthodoksi na kusema kuwa haitasitisha mapigano hadi pale Russia itakapoondoa majeshi yake katika maeneo inayoyakalia.
Wakati huo huo, Dmitry Medvedev, Naibu Mkuu wa Baraza la Usalama wa Taifa la Russia amesema kuhusiana na uamuzi wa Ukraine wa kukataa kusitisha mapigano: "wakati wa mapumziko ya Krismasi, mkono wa upendo wa Kristo umenyooshwa kwa Ukraine, lakini viongozi wa Ukraine wameukataa".
Naye Dmitry Polyansky, naibu balozi wa Russia katika Umoja wa Mataifa, amezungumzia msimamo wa serikali ya Ukraine wa kukataa pendekezo la usitishaji vita lililotolewa na Moscow katika masiku ya Krismasi, akisema: "Kiev iko tayari kuwatoa kafara watu wa Ukraine kwa malengo ya kijiografia na kisiasa ya Magharibi".../
Tags