Jun 07, 2023 10:04 UTC
  • Sisitizo la Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia kuwa Marekani inaunga mkono magaidi wa Daesh na Al Qaeda

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergey Lavrov amesema Marekani inaunga mkono makundi ya kigaidi nchini Afghanistan kwa lengo la kuliyumbisha eneo.

Akizungumza wakati wa ziara yake katika kambi ya kijeshi ya Russia huko Tajikistan siku ya Jumatatu, Lavrov amesema,  "inajulikana kuwa Marekani inawaunga mkono kikamilifu magaidi wa Daesh (ISIS) waliosalia nchini Afghanistan na al-Qaeda na makundi mengine ya kigaidi yenye mafungamano nayo. Lengo na uungaji mkono huo ni kuhakikisha hakuna utulivu nchini Afghanistan."

"Ni kwa manufaa ya Marekani kuona hakuna uthabiti katika nchi hiyo," amesema Lavrov. Pia amepuuzilia mbali kauli za uongo zilizotolewa na balozi wa Marekani nchini Tajikistan Manuel Micaller ambapo alikanusha uungaji mkono wa Marekani kwa makundi ya kigaidi yanayopinga Taliban.

Russia imetangaza mara kwa mara kwamba Marekani iliunga mkono moja kwa moja magaidi wakufurishaji wa ISIS wakati ilipokuwepo kijeshi nchini Afghanistan na baada ya hapo, na kukosoa vikali sera hiyo ya Washington.

Kwa mtazamo wa Moscow, lengo la Marekani katika kuunga mkono magaidi ni kuendeleza ukosefu wa utulivu nchini Afghanistan na kuimarisha makundi ya kigaidi katika nchi hiyo, yakiwemo makundi ya Daesh na Al-Qaeda.

Kuhusiana na hilo, Lavrov ameashiria hatua kama hiyo ya Marekani katika eneo la Caucasus Kusini mwishoni mwa muongo uliopita na kusisitiza kwamba lengo ni kuvuruga utulivu wa Afghanistan. Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia anaamini kuwa ni kwa manufaa ya Marekani utulivu uvurugwe mara kwa mara katika nchi hiyo.

Ushahidi wa uhakika unaonyesha kuwa Marekani ilikuwa na nafasi kubwa katika kuasisiwa na kuliendeleza kundi la kigaidi la kitakfiri la Daesh kwa ajili ya kukabiliana na mhimili wa muqawama (mapambano) na imefanya juhudi za kuendelea kupanua harakati za kundi hilo la kigaidi huko Iraq na Syria na kisha Afghanistan. Kuna ushahidi wa kina unaothibitisha kwamba Marekani imehusika katika mipango maalumu ya kueneza ugaidi duniani na hasa eneo la Asia Magharibi. Marekani haiwezi kuficha jukumu lake katika uundaji wa Daesh. Marekani ikiwa kinara wa nchi za Magharibi pamoja na washirika wake katika baadhi ya nchi za Kiarabu wameunga mkongo magaidi wakufurishaji wakiwemo wa ISIS na inayatazama makundi hayo ya kigaidi kama njia ya kufikia malengo yake haramu.

 

Magaidi watenda jinai wa ISIS

Baada ya kushindwa vibaya magaidi wa Daesh huko Syria na Iraq, Washington imemarisha kundi hilo la kigaidi nchini Afghanistan ili kuvuruga usalama katika nchi jirani za Afghanistan. Kuhusu Afghanistan, Washington ilifuata utaratibu huo huo kabla ya kujiondoa katika nchi hiyo kwa kuwaunga mkono magaidi wa ISIS kushambulia nchi inazohasimiana nazo na nchi jirani ya Afghanistan.

Zamir Kabulov, mwakilishi wa Rais wa Russia katika masuala ya Afghanistan, alisema mwishoni mwa mwezi Agosti 2021 kwamba: Vikosi vya Marekani na washirika wa nchi hiyo huko Afghanistan waliwasiliana na kundi la kigaidi la ISIS na kushirikiana nalo. Sasa, kwa kuendelea kuunga mkono ISIS na al-Qaeda, Marekani inakusudia hasa kutoa pigo kwa Russia, nchi za Asia ya Kati na Iran kwa kuyumbisha na kuongeza ukosefu wa usalama nchini Afghanistan.

Suala muhimu ni kwamba wanasiasa waandamizi wa Marekani wamekiri nafasi ya Washington katika uundaji na upanuzi wa kundi la kigaidi la Daesh. Kuhusiana na hilo, Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump amenukuliwa akisema kuwa rais aliyemtangulia Barack Obama na Waziri wa Mambo ya Nje wa zamani wa Marekani Hillary Clinton walihusika moja kwa moja katika kuunda kundi la kigaidi la ISIS. Katika hotuba yake ya kampeni za uchaguzi Januari 2016, Trump alisema: Wao (Obama na Clinton), ni watu wasio waaminifu kwani walianzisha ISIS. Hillary Clinton pamoja na Obama waliunda ISIS.

Pia, "Robert F. Kennedy Jr.", mwanasiasa wa Marekani mwenye umri wa miaka 69 ambaye ametangaza kushiriki katika uchaguzi wa urais mwaka ujao akiwa mpinzani wa Rais Joe Biden katika Chama cha Democratic, amekiri kwamba Marekani ilianzisha kundi la kigaidi la ISIS. Robert Kennedy Jr. Amesema: Tuliunda ISIS. Tulituma wakimbizi milioni mbili Ulaya na kusababisha kuyumba kwa demokrasia huko ambako kulisababisha Brexit.

Kauli za Trump na Robert F. Kennedy Junior kwa hakika ni uthibitisho wa shutuma ambazo zimetolewa mara nyingi na wakuu wa baadhi ya nchi duniani, kama vile Rais Vladimir Putin wa Russia, kuhusu kuhusika moja kwa moja Ikulu ya White House katika uundaji kundi la ISIS na vitendo vyake vya kigaidi.

Tags