Mwenendo unaoongezeka wa vitisho dhidi ya Waislamu nchini Ufaransa
https://parstoday.ir/sw/news/world-i98882-mwenendo_unaoongezeka_wa_vitisho_dhidi_ya_waislamu_nchini_ufaransa
Katika miaka ya karibuni, wanasiasa wa Ufaransa wamekuwa wakiwawekea vikwazo Waislamu na kuchochea chuki dhidi ya Uislamu katika nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 17, 2023 04:28 UTC
  • Mwenendo unaoongezeka wa vitisho dhidi ya Waislamu nchini Ufaransa

Katika miaka ya karibuni, wanasiasa wa Ufaransa wamekuwa wakiwawekea vikwazo Waislamu na kuchochea chuki dhidi ya Uislamu katika nchi hiyo.

Ingawa Ufaransa ina idadi kubwa zaidi ya Waislamu barani Ulaya, lakini Waislamu wa nchi hiyo wanakabiliwa na vikwazo, vitisho na mashinikizo mbalimbali.

Wizara ya Elimu ya Ufaransa jana Ijumaa iliamuru uchunguzi wa kiidara ufanyike kufuatia kitendo cha wanafunzi wa Kiislamu wa shule tatu za mji wa Nice kusini-mashariki mwa Ufaransa kuswali hadharani katika uwanja wa shule hizo.

Akizungumzia kitendo hicho, meya wa manispaa ya Nice amesema kuwa kitendo hicho cha wanafunzi Waislamu kuswali kwenye uwanja wa shule hakivumiliki.

Waziri wa Elimu wa Ufaransa ametangaza katika taarifa ya pamoja na meya huyo kwamba wanafunzi kadhaa waliswali swala hizo wakati wa mapumziko. Amesisitiza kuwa atachukua hatua zozote zinazohitajika ili kuhakikisha kuwa sheria za kilaiki zisizozingatia dini zinafuatwa kikamilifu katika shule za nchi hiyo.

Katika barua iliyotumwa kwa Waziri wa Elimu wa Ufaransa, Christian Strosi, Meya wa Nice, amelaani vikali kitendo cha wanafunzi Waislamu kuswali katika uwanja wa shule na kukaa kwao kimya kwa dakika moja kama ishara ya heshima kwa Mtume Muhammad (saw).

Wakati huo huo, hivi karibuni video moja imesambazwa mitandaoni ikionyesha mabinti wa Kiislamu katika shule moja nchini Ufaransa wakilazimishwa kuvua hijabu kabla ya kuruhusiwa kuingia shuleni.

Utendaji wa viongozi wa shule hiyo umechochea hasira ya watumiaji mitandao ya kijamii huko Kifaransa.

Hivi karibuni Kamati ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa ilitangaza kwamba Ufaransa imekiuka mkataba wa kimataifa wa haki za binadamu kwa kuwazuia wanawake na wasichana wa Kiislamu waliovaa hijabu kushiriki masomo katika shule za nchi hiyo.