Sep 26, 2023 09:18 UTC
  • Sura ya Al-Qamar, aya ya 23-32 (Darsa ya 971)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 971 na sura tunayoizungumzia kwa sasa ni ya 54 ya Al-Qamar. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 23 hadi ya 26 ya sura hiyo ambazo zinasema:

كَذَّبَتْ ثَمُودُ بِالنُّذُرِ

Thamudi waliwakanusha Waonyaji.

فَقَالُوا أَبَشَرًا مِّنَّا وَاحِدًا نَّتَّبِعُهُ إِنَّا إِذًا لَّفِي ضَلَالٍ وَسُعُرٍ

Wakasema: Ati tumfuate mtu mmoja miongoni mwetu? Basi hivyo sisi tutakuwa katika upotofu na kichaa! 

أَأُلْقِيَ الذِّكْرُ عَلَيْهِ مِن بَيْنِنَا بَلْ هُوَ كَذَّابٌ أَشِرٌ

Ameteremshiwa yeye tu huo ukumbusho baina yetu sote? Bali yeye ni mwongo mwenye kujiona!

سَيَعْلَمُونَ غَدًا مَّنِ الْكَذَّابُ الْأَشِرُ

Kesho watajua ni nani huyo mwongo mwenye kujiona. 

Katika darsa zilizopita tulizungumzia habari na hatima iliyozipata kaumu za Nuh na A’adi. Katika darsa yetu ya leo tutazungumzia habari za kaumu ya Thamudi. Watu wa kaumu hiyo walikuwa wakiishi kaskazini ya Bara Arabu na Mtume wao alikuwa Saleh AS. Kwa hakika kiburi na ghururi waliyokuwa nayo watu hao iliwafanya wasiyajali maonyo na indhari walizokuwa wakipewa na Mtume huyo wa Allah na kuamua kuendelea kufanya maasi na maovu. Watu wa kaumu ya Thamudi sio tu hawakuwa tayari kuukubali wito wa Nabii Saleh, lakini walimtuhumu pia Mtume wao huyo kuwa ni mtu mpotofu na mwendawazimu na kwamba kumfuata yeye kunawapotosha watu pia na kuwatia uwendawazimu. Lakini mbali na hayo, watu hao walikuwa na kisingizio kingine pia walichotoa kumpinga Nabii Saleh AS. Walikuwa wakisema, itawezekanaje mtu aliye kama sisi, ambaye anaishi baina yetu maisha ya kawaida tu, tena hana mamlaka, utajiri wala umati wa watu walio nyuma yake aje adai jambo kubwa kama hili la kusema kwamba ametumwa na Mwenyezi Mungu kuja kutuletea sisi uongofu? Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, katika sifa za kipekee za Mitume ni kwamba walitokana na watu wa kawaida na walikuwa wakiishi maisha ya kawaida ili wawe mfano na kigezo cha kuweza kuigwa na kufuatwa na watu wao. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, baadhi ya wakati watu huporomoka katika utu wao wakafika hadi ya kukataa katakata kuwafuata waja wema na safi kama Mitume, lakini wakati huohuo wakawa radhi kuishi maisha ya madhila chini ya watawala mataghuti au hata wakafika hadi ya kuabudu vitu visivyo na roho wala hisia yoyote! Aya hizi aidha zinatuelimisha kwamba, kuwatuhumu Mitume kuwa ni watu waongo na wenye kiburi na majivuno ni miongoni mwa silaha zinazotumiwa na wapinzani, ilhali wanaofanya hivyo, wao wenyewe ndio wenye tabia na hulka hizo.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 27 hadi ya 29 ya sura yetu ya Al-Qamar ambazo zinasema:

إِنَّا مُرْسِلُو النَّاقَةِ فِتْنَةً لَّهُمْ فَارْتَقِبْهُمْ وَاصْطَبِرْ

Hakika Sisi tutawaletea ngamia jike ili kuwajaribu, basi watazame tu na usubiri.

وَنَبِّئْهُمْ أَنَّ الْمَاءَ قِسْمَةٌ بَيْنَهُمْ ۖ كُلُّ شِرْبٍ مُّحْتَضَرٌ

Na waambie kwamba maji yatagawanywa baina yao; kila sehemu ya maji itahudhuriwa (na mwenye zamu yake).

فَنَادَوْا صَاحِبَهُمْ فَتَعَاطَىٰ فَعَقَرَ

Basi wakamwita mtu wao akaja akamchinja.

Ni jambo lililo wazi kwamba haiwezekani kumkubali mtu yeyote anayedai kuwa Mtume mpaka aonyeshe muujiza wa kuthibitisha ukweli wa madai yake. Kwa hivyo, kwa irada ya Allah SWT, jabali lilipasuka na ndani yake akatoka ngamia mwenye umbo kubwa na aliyekuwa tofauti na ngamia wengine. Kiwango cha maji ambacho alihitaji kunywa ngamia huyo kilikuwa kikubwa kiasi kwamba ilipasa maji hayo yagawanywe kwa zamu baina ya watu wa kaumu ya Thamudi na mnyama huyo. Huo tab’an ulikuwa mtihani wa Mwenyezi Mungu kwa watu hao. Kwa hivyo iliwapasa wachunge na kuheshimu mgao huo wa maji na kwenda kutumia kila ilipofika zamu yao. Wakuu wa kaumu ya Thamudi, ambao hawakuwa na uwezo wa kuukana muujiza huo, waliamua wamuue ngamia. Kwa hiyo wakamtafuta mtu wa kumpa jukumu la kuitekeleza kazi hiyo. Nabii Saleh aliwaonya na kuwapa indhari kwamba ikiwa baada ya kujionea muujiza kwa macho yao wataendelea kukadhibisha na kuikaidi haki, matokeo ya ukaidi wao yatakuwa ni kuteremkiwa na adhabu ya Mwenyezi Mungu. Pamoja na hayo, kaumu ya Thamudi iliyapuuza maonyo ya Nabii Saleh AS wakaamua kumchinja ngamia yule wa miujiza. Miongoni mwa tunayojifunza kutokana na aya hizi ni kwamba, miujiza ya Allah ni njia ya kuwatahini watu pia ili ibainike ni nani wenye nia ya dhati ya kuijua haki na ukweli na kuifuata na nani ambao kutokana na inadi, ubishi na ukaidi wamedhamiria kuipinga na kuipiga vita haki. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa Allah SWT hamwadhibu mtu wala hawateremshii watu adhabu kabla hajatimiza dhima kwa watu hao. Vilevile aya hizi zinatuonyesha kuwa wapinzani wa Mitume huwatumia watu makhabithi na wamwagaji damu ili kufikia malengo yao maovu.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 30 hadi ya 32 ya sura yetu ya Al-Qamar ambazo zinasema:

فَكَيْفَ كَانَ عَذَابِي وَنُذُرِ

Basi ilikuwaje adhabu yangu na maonyo yangu!

إِنَّا أَرْسَلْنَا عَلَيْهِمْ صَيْحَةً وَاحِدَةً فَكَانُوا كَهَشِيمِ الْمُحْتَظِرِ

Hakika Sisi tuliwapelekea ukelele mmoja tu, wakawa kama majani makavu yaliyosagika yaliyo zizini.

وَلَقَدْ يَسَّرْنَا الْقُرْآنَ لِلذِّكْرِ فَهَلْ مِن مُّدَّكِرٍ

Na bila ya shaka Sisi tumeifanya Qur'ani iwe nyepesi kuikumbuka; basi je yupo anaye kumbuka?

Baada ya kuuliwa ngamia, ambaye aliletwa na Mwenyezi Mungu ili kuthibitisha ukweli wa Utume wa Nabii Saleh AS, adhabu ya Mola iliwateremkia watu wa kaumu ya Thamudi kwa sura ya moto wa radi ambao uliwapiga watu wa kaumu hiyo ukawakausha na kuwafanya washindwe hata kutikisika. Matokeo yake wakawa ni mithili ya nyasi kavu ambazo wafugaji huzichambua na kuzivuruga ili kuzitumia kwa ajili ya chakula cha mifugo yao. Katika kuhitimisha simulizi za kaumu ya Thamudi, kwa mara nyingine tena Allah SWT anakumbusha kuwa, lengo la kuteremshwa Qur’ani ni kutoa mawaidha na maonyo ili watu wajue hatari zilizoko mbele yao na kwa hivyo wajinusuru kwa kuziepusha nafsi zao na hatari hizo ili wasije wakafikwa na adhabu ya Mola duniani na akhera. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, japokuwa muuaji wa ngamia alikuwa mtu mmoja, lakini kwa vile dhambi hiyo iliridhiwa na watu wengine kwa umoja wao, Qur’ani imekihusisha kitendo cha kumchinja ngamia huyo na wao wote na adhabu iliyoteremshwa ikawafika wote. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, hakuna mtu yeyote mwenye nguvu na uwezo wa kuizuia irada na lile alitakalo Mola. Watu wenye nguvu wa kaumu ya Thamudi walitupwa na kugaragazwa chini mithili ya matawi ya miti yaliyokauka, kisha yakakatika katika na kuvurugika chini. Wa aidha inatubainikia kutokana na aya hizi kwamba, Qur’ani si kitabu cha historia, lakini inabainisha kwa usahihi na kulingana na uhalisia wake historia ya baadhi ya kaumu zilizopita ili itoe ibra na mazingatio kwa watu wote. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 971 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah aijaalie Qur’ani iwe kilainishi na ponyo la nyoyo zetu, na iwe kinawirishi na pambo la macho yetu na Siku ya Kiyama ije iwe sahibu na muombezi wetu. Wassaalamu Alaykum Warahamatullahi Wabarakatuh…/

 

 

Tags