Jun 27, 2024 02:27 UTC
  • Alkhamisi, Juni 27, 2024

Leo ni Alkhamisi tarehe 20 Mfunguo Tatu Dhulhija 1445 Hijria sawa na tarehe 27 Juni mwaka 2024 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 1317 iliyopita alizaliwa Imam  Mussa al-Kadhim (as) ambaye ni mmoja kati ya wajukuu watukufu wa Bwana wetu Muhammad (saw).

Alilelewa na baba yake Imam Ja'far Swadiq (as) na kupata elimu na maarifa ya Kiislamu kutoka kwa mtukufu huyo kwa kipindi cha miaka 20. Baada ya kuuawa shahidi baba yake, Imam Kadhim (as) alishika hatamu za Uimamu na uongozi wa Umma wa Kiislamu kwa kipindi cha miaka 35 na kukabiliana na mashaka mengi. Imam Kadhim (as) alipitisha kipindi kikubwa cha umri wake katika kuwazindua na kuwaelimisha Waislamu maarifa asili ya dini.

Suala hili liliwatia hofu kubwa watawala wa Bani Abbas ambao walimkamata na kumfunga jela ili kumuweka mbali na Waislamu waliokuwa na kiu ya maarifa halisi ya dini yao. Imam Kadhim (as) alisifika kwa ukarimu mkubwa, uvumilivu na usamehevu. Tunatoa mkono wa baraka kwa Waislamu wote kwa mnasaba wa kuadhimisha siku hii muhimu ya kuzaliwa mtukufu huyo. 

Siku kama ya leo miaka 47 iliyopita inayosadifiana na 27 Juni 1977, nchi ya Djibouti iliyoko karibu na eneo la Pembe ya Afrika ilipatia uhuru kutoka kwa mkoloni Mfaransa baada ya kupita miaka kadhaa ya harakati ya kupigania uhuru.

Tokea mwaka 1896 nchi hiyo ilikuwa ikijulikana kwa jina la Somalia Ufaransa na kuwa chini ya himaya ya Ufaransa, lakini baada ya kupita miongo minane, hatimaye nchi hiyo ilipata uhuru.

Djibouti ilikuwa nchi ya mwisho kujiunga na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na inahesabiwa kuwa nchi muhimu katika eneo la kiistratijia kwa kuwa inapakana na Bahari Nyekundu na Bahari ya Hindi, kwenye eneo la lango bahari la 'Bab Mandab'. 

Katika siku kama ya leo miaka 43 iliyopita mwafaka na tarehe 7 mwezi wa Tir mwaka 1360 Hijria Shamsiya, Ayatullah Dakta Muhammad Beheshti aliuawa shahidi akiwa pamoja na watu wengine 72 waliokuwa miongoni mwa shakhsiya bora wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran baada ya kuripuliwa kwa bomu ofisi kuu ya chama cha Jamhuri ya Kiislamu.

Ayatullah Beheshti pia alikuwa miongoni mwa shakhsiya wa awali waliotoa mchango mkubwa katika Mapinduzi ya Kiislamu. Dakta Beheshti pia alikuwa mmoja kati ya wasaidizi wakuu wa Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu.

Mlipuko huo wa bomu uliwaua shahidi Dakta Beheshti na wasaidizi 72 wa Imam Khomeini wakiwemo mawaziri na wabunge kadhaa.

Ayatullah Dakta Muhammad Beheshti

Tarehe 27 Juni 1993, Marekani ilirusha makombora 23 huko Baghdad mji mkuu wa Iraq na pambizoni mwa mji huo.

Shambulio hilo lilifanyika kwa kisingizo kwamba viongozi wa utawala wa zamani wa Iraq walitaka kumuuwa George Bush 'baba', Rais wa zamani wa Marekani wakati alipokuwa safarini nchini Kuwait mwezi April mwaka huo huo. Shambulio hilo lilipelekea watu sita kuuawa na jengo la makao makuu ya Taasisi ya Usalama ya Iraq liliharibiwa kabisa.   ****

Miaka 37 iliyopita katika siku kama ya leo mji wa Sardasht huko magharibi mwa Iran ulishambuliwa kwa mabomu ya kemikali na ndege za kivita za utawala wa zamani wa Iraq.

Raia wasio na ulinzi 110 wa Iran wakazi wa mji huo waliuawa shahidi na wengine 530 kujeruhiwa katika mashambulizi hayo ya utawala wa zamani wa Saddam Hussein.

Utawala wa Saddam ambao ulikuwa umekata tamaa ya kupata ushindi katika medani za vita dhidi ya Iran ulikuwa ukidhani kwamba kwa kufanya mashambulizi hayo ya kemikali dhidi ya raia wa mji wa Sardasht ungeweza kulitwisha taifa la Iran matakwa yake.

Taasisi muhimu za kimataifa na madola makubwa duniani hata hivyo hazikuchukua hatua yoyote ya jadi ya kuuzuia utawala wa Saddam kutumia silaha za kemikali wala hata kulaani jinai hizo ulizozifanya dhidi ya raia wasio na hatia wa Iran.

Shambulizi la kemikali dhidi ya watu wa Sardasht

Na siku kama ya leo miaka 29 iliyopita Sheikh Hamad bin Khalifa Aal Thani aliyekuwa mrithi wa Amir wa Qatar alifanya mapinduzi dhidi ya baba yake.

Sheikh Hamad alimuondoa madarakani baba yake, Sheikh Khalifa bin Hamad Aal Thani wakati Amiri huyo wa zamani wa Qatar alipokuwa safarini nchini Uswisi. Sheikh Khalifa ambaye alikuwa kiongozi wa Qatar tangu mwaka 1972 alifanya jitihada kubwa za kurejea madarakani lakini hakufanikiwa.

Nchi ndogo ya Qatar iko kusini mwa Ghuba ya Uajemi na inapakana na Saudi Arabia. Nchi hiyo ina utajiri mkubwa wa mafuta na gesi.   

Sheikh Hamad bin Khalifa Aal Thani