Aug 05, 2024 02:28 UTC
  • Jumatatu, tarehe 5 Agosti, 2024

Leo ni Jumatatu tarehe 30 Mfunguo Nne Muharram 1446 Hijria inayosadifiana na tarehe 5 Agosti mwaka 2024.

Tarehe 5 Agosti mwaka 129 iliyopita, alifariki dunia Friedrich Engels mwanafalsafa mashuhuri wa Ujerumani.

Alikuwa rafiki na mshirika wa karibu wa mwanafalsafa mwingine wa Ujerumani yaani Karl Marx. Engels alifuatiliwa na kusakwa na vyombo vya dola kutokana na harakati zake za kisiasa na mwaka 1850 alikimbilia nchini Uingereza. Engels na Karl Marx walitayarisha Manifesto ya Ukomonisti iliyotangazwa na vyama vya kikomonisti katika mkutano wao wa kwanza mnamo mwaka 1848.

Baada ya Karl Marx, Friedrich Engels alikuwa na nafasi muhimu katika kujitokeza nadharia ya ukomonisti.   

Friedrich Engels

Siku kama ya leo miaka 64 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 5 Agosti 1960, nchi ya Burkina Faso iliyoko magharibi mwa Afrika ilipatia uhuru.

Burkina Faso ilikuwa chini ya mkoloni Mfaransa tokea katikati mwa karne ya 19. Nchi hiyo ambayo zamani ilikuwa ikijulikana kwa jina la Upper Volta, ilianza kujipatia mamlaka ya ndani mwaka 1958, lakini miaka miwili baadaye ilipatia uhuru kamili na kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa. Hata hivyo, ilipofika mwaka 1984, nchi hiyo iliamua kubadilisha jina kutoka Upper Volta na kuitwa Burkina Faso.

Nchi hiyo ya Kiafrika inapakana na nchi za Mali, Ivory Coast, Ghana, Togo, Benin na Niger.   

Katika siku kama ya leo miaka 61 iliyopita mkataba wa kuzuia majaribio ya silaha za nyuklia kati ya Marekani, Urusi ya zamani na Uingereza ulitiwa saini.

Baada ya kuanza kipindi cha Vita Baridi, ulimwengu ulikaribia kutumbukia katika vita vikubwa vya maangamizi kutokana na kuanza majaribio ya nyuklia na utengenezaji wa makombora yanayovuka mabara na yenye vichwa vya silaha za nyuklia. Suala la Cuba na kupelekwa huko makombora ya Urusi lilifikisha mgogoro huo kileleni.

Baada ya kusainiwa mkataba huo anga ya kimataifa ilitulia kidogo na kukaanza mazungumzo ya jadi kwa ajili ya kusimamisha majaribio ya silaha za nyuklia. Kuanzia Oktoba mwaka 1958 Marekani, Urusi na Uingereza zilitilia maanani suala la kusitisha majaribio ya silaha hizo japokuwa ziliendelea kufanya majaribio hayo.

Hatimaye na baada ya mazungumzo mapana, nchi hizo tatu zilifikia makubaliano ya kuzuia majaribio ya silaha za nyuklia ambayo yalitiwa saini tarehe 5 Oktoba mwaka 1963.   

Siku kama ya leo miaka 36 iliyopita, dikteta wa zamani wa Iraq, Saddam Hussein alilazimika kukubali usitishaji vita na Iran.

Baada ya Iran kukubali azimio nambari 598 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hapo tarehe 27 Tir mwaka 1367 Hijria Shamsia ambalo lilijumuisha usitishaji vita baina ya pande mbili, ilitarajiwa kuwa mapigano ya kijeshi baina ya nchi hizo mbili pia yangekomeshwa. Hata hivyo siku kadhaa baadaye Saddam Hussein alifanya mashambulizi makubwa dhidi ya ardhi ya Iran ambayo yalifeli kutokana na ushujaa wa wapiganaji wa Kiirani.

Hatimaye Saddam Hussein ambaye aliilazimisha Iran kuingia katika vita vya miaka 8 vilivyosababisha hasara kubwa ya hali na mali na hakuweza kufikia malengo yake, alikubali kusitisha mapigano katika siku kama hii ya leo na kutekeleza makubaliano hayo wiki mbili baadaye.   

Na siku kama ya leo miaka 34 iliyopita, Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC walipasisha Azimio la Haki za Binadamu za Kiislamu katika mkutano  wa 19 wa mawaziri hao uliofanyika Cairo, mji mkuu wa Misri.

Kwa mnasaba huo siku hiyo imepewa jina la 'Siku ya Haki za Binadamu za Kiislamu na Utukufu wa Mwanadamu.' Azimio hilo lina utangulizi na vipengee 25. Azimio la Haki za Binadamu za Kiislamu lilipasishwa baada ya nchi za Kiislamu kukosoa Azimio la Haki za Binadamu lililopasishwa mwaka 1948 katika Umoja wa Mataifa ambalo lilibuniwa kwa misingi ya fikra za kiliberali za nchi za Magharibi na baadhi ya vipengee vyake vinapingana na mafundisho ya Kiislamu.

Sifa kuu inayotofautisha Azimio la Haki za Binadamu za Kiislamu na lile la Umoja wa Mataifa ni kutilia maanani haki za kiroho na kimaanawi za maisha ya mwanaadamu kwa mujibu wa mafundisho ya Mwenyezi Mungu. 

 

Tags