Jumanne, 24 Disemba, 2024
Leo ni Jumanne tarehe 22 Mfunguo Tisa Jamadithani 1446 Hijria mwafaka na tarehe 24 Disemba 2024.
Siku kama ya leo miaka 1055 iliyopita, alifariki dunia mtaalamu wa mashairi wa Kiislamu kwa jina la Ibn Hajjaj.
Ibn Hajjaj alizaliwa mjini Baghdad, Iraq na alijikita katika taaluma ya mashairi akiwa bado kijana na kutokea kuwa maarufu katika uwanja huo. Alitunga mashairi mengi yanayowaenzi na kuwasifu Ahlul bait wa Mtume (saw) na kuwashambulia wapiznani wa Uislamu na Mtume. Miongoni mwa athari za malenga huyo ni pamoja na diwani ya mashairi yenye juzuu kumi inayohifadhiwa katika maktaba mbalimbali duniani.

Miaka 500 iliyopita katika siku inayosadifiana na hii ya leo aliaga dunia Vasco da Gama baharia na mvumbuzi mashuhuri wa Kireno.
Vasco da Gama alizaliwa mwaka 1460. Mwaka 1498 baharia huyo mashuhuri wa Kireno alifanya kazi muhimu ya kuvumbua njia ya majini kutoka Ulaya hadi bara la Asia na India.

Miaka 175 iliyopita katika siku kama ya leo, majeshi ya Ufaransa yaliishambulia ardhi ya Guinea ya magharibi mwa Afrika.
Mashambulio hayo yalikuwa utangulizi wa Ufaransa kudhibiti ardhi hiyo iliyokuwa na utajiri wa dhahabu. Kabla ya vikosi vya Ufaransa kuishambulia ardhi ya Guinea, kulikuwa kumeanzishwa mashirika ya kibiasharaya dhahabu katika pwani ya Guinea.

Siku kama ya leo miaka 159 iliyopita, kundi la siri lililojulikana kwa jina la Ku-Klux-Klan ambalo liliitakidi kuwa watu weupe ni jamii ya watu bora na wa daraja la juu, liliasisiwa nchini Marekani kwa shabaha ya kupambana na watu wa jamii nyinginezo, hususan raia weusi.
Japokuwa kundi la Ku-Klux Klan lilipigwa marufuku miaka minne baada ya kuasisiwa kwake, lakini hadi kufikia sasa limeshafanya mauaji mengi dhidi ya raia weusi wa Marekani, kutesa, kuwaudhi, kuzusha hofu na kutoa vitisho dhidi yao.

Siku kama ya leo miaka 73 iliyopita Libya ilijipatia tena uhuru wake baada ya kupasishwa azimio la Umoja wa Mataifa na Muhamad Idriss al Mahdi kuteuliwa kuwa mfalme wa nchi hiyo.
Huko nyuma Libya ilijulikana kwa jina la Tripoli na kwa miaka kadhaa ilikuwa chini ya himaya kubwa ya nchi za kigeni. Katika karne ya 16 Miladia Libya ilivamiwa na kukaliwa kwa mabavu na jeshi la Othmania. Aidha wakati wa kukaribia Vita vya Kwanza vya Dunia, nchi hiyo ilivamiwa na Italia lakini wananchi wa Libya wakapambana vikali na wavamizi hao wa Ulaya. Katikati ya Vita vya Pili vya Dunia, Uingereza na Ufaransa zikaikalia kwa mabavu nchi hiyo, na hatimaye Libya ikajipatia uhuru wake mwaka 1951.
