Alkhamisi, Aprili 10, 2025
Leo ni Alkhamisi tarehe 11 Mfunguo Mosi Shawwal 1446 Hijria inayosadifiana na tarehe 10 Aprili 2025 Milaadia.
Siku kama ya leo miaka 1449 iliyopita, Mtume Muhammad (saw) alikwenda eneo la “Taif” kwa ajili ya kueneza dini ya Uislamu. Safari hiyo na kulingania dini katika eneo la Taif, karibu na Makka, ilifanyika muda mfupi baada ya kuaga dunia Abu Twalib aliyekuwa msaidizi mkuu na mlinzi wa Mtume, na kwa sababu hiyo, waabudu masanamu wa Kiquraishi walikuwa wamezidisha mateso yao dhidi ya mtukufu huyo na masahaba zake.
Kwa msingi huo, kama watu wa Taif wangesilimu, mji huo ungekuwa kituo na mahali salama kwa Waislamu waliokuwa wakikandamizwa na kudhulumiwa huko Makka. Hata hivyo viongozi wa kabila la Thaqif huko Taif, sio tu kwamba hawakumwamini Mungu Mmoja na Mtume wake, Muhammad (SAW), bali pia waliwachochea baadhi ya wajinga waliomuudhi Mtume (saw) na kumjeruhi.

Siku kama ya leo miaka 212 iliyopita, alifariki dunia Joseph-Louis Lagrange, mwanahisabati maarufu wa Ufaransa. Lagrange alizaliwa mwaka 1736 huko mjini Turin, Italia. Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri ni pamoja na kitabu cha 'Uchunguzi wa Umekanika' ambacho alikiandika kwa kipindi cha miaka 25.

Katika siku kama ya leo miaka 106 iliyopita, aliuawa Emiliano Zapata mwanamapinduzi mashuhuri wa nchini Mexico kupitia njama maalumu dhidi yake. Wahindi Wekundu wa Mexico wanamfahamu Zapata kama mrekebishaji wa jamii na mwokozi wao. Tangu mwishoni mwa mwaka 1910 sanjari na kutoa nara za kupigania uhuru, alibeba pia silaha na kuwaongoza Wahindi Wekundu katika kupambana na wavamizi na kufanikiwa kuzikomboa ardhi za nchi hiyo zilizokuwa zimeporwa.

Siku kama ya leo miaka 79 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 10 Aprili 1946, kundi la mwisho la wanajeshi wa Ufaransa liliondoka huko Lebanon.
Ufaransa ilizikalia kwa mabavu Lebanon na Syria wakati wa Vita vya Pili vya Dunia. Lebanon ilipata uhuru mwaka 1945 na mwaka huo huo ikatia saini makubaliano ya kuondoka askari wa Uingereza na Ufaransa katika ardhi ya nchi hiyo ambayo yalianza kutekelezwa Aprili 1946.

Siku kama ya leo miaka 52 iliyopita yaani sawa na tarehe 10 Aprili 1973, makachero wa Shirika la Ujasusi la utawala haramu wa Israel MOSSAD waliwaua maafisa watatu wa Palestina huko Beirut, mji mkuu wa Lebanon.
Katika kuendeleza jinai zake dhidi ya Wapalestina, miaka kumi baadaye utawala wa Kizayuni wa Israel yaani tarehe 10 Aprili 1983, ulimuuwa huko Ureno, Isam Sartawi aliyekuwa mshauri wa Yassir Arafat kiongozi wa zamani wa Harakati ya Ukombozi ya Palestina (PLO).
Utawala wa Kizayuni wa Israel umekuwa ukitumia mauaji ya kigaidi dhidi ya viongozi wa mapambano ya ukombozi wa Palestina kwa ajili ya kuendelea kujipanua na kuzima mapambano ya wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina.
