Dec 09, 2025 02:38 UTC
  • Jumanne, tarehe 9 Disemba, 2025

Jumanne tarehe 18 Jamadithani 1447 Hijria sawa na Disemba 9 mwaka 2025.

Siku kama ya leo miaka 428 iliyopita aliuawa shahidi Kadhi Sayyid Nurullah Shushtari, faqihi, mwanatheolojia na alimu mkubwa.

Alizaliwa mwaka 956 Hijiria katika familia bora na ya kielimu huko Shushtar, kusini magharibi mwa Iran. Sayyid Nurullah Shushtari alijifunza masomo ya awali ya kidini kwa baba yake na kisha akaelekea Mash’had, kaskazini mashariki mwa Iran na kustafidi na elimu kutoka kwa maulama wakubwa wa mji huo.

Mwaka 993, Kadhi Sayyid Nurullah Shushtari alielekea India kwa ajili ya kulingania dini ambapo wakati huo nchi hiyo ilikuwa chini ya utawala wa Mfalme Akbar Shah katika silsila ya Mongolia. Hadhi yake kubwa, elimu na uadilifu wa Sayyid Shushtari vilimfanya ateuliwe kuwa kadhi wa mji wa Lahore nchini humo. Baada ya kufariki dunia Mfalme Akbar Shah, wapinzani wa mwanazuoni huyo walimwendea mfalme aliyechukua uongozi kwa jina la Jahangir Shah na kumwambia maneno ya uongo na ya uchonganishi, na hatimaye liuawa shahidi katika siku kama ya leo kwa kutumia kisingizio cha madhehebu ya Shia ya alimu huyo mkubwa.

Sayyid Nurullah Shushtari ameandika vitabu kadhaa miongoni kama ‘Majaalisu-Mu’minina’ ‘Ihqaaqul-Haqqi’ na ‘Tuhfatul-Uquul.’ 

Siku kama ya leo miaka 283 iliyopita Carl Wilhelm Scheele mwanakemia mashuhuri wa Sweden na mmoja kati ya waasisi wa elimu ya kemia ya leo alizaliwa huko Stockholm mji mkuu wa nchi hiyo.

Mwanakemia huyo aliendelea na masomo yake kutokana na jitihada na hamu yake kubwa aliyokuwanayo licha ya familia yake kuwa duni.

Carl Wilhelm ambae aliishi katika zama za kuchanua kwa elimu ya kemikali, mwezi Oktoba mwaka 1772 alifanikiwa kugundua gesi ya chlorine baada ya juhudi za miaka mitano. Gesi hiyo ni moja kati ya mada muhimu za kemikali na inatumika sana viwandani. Mbali na hayo mwanakemia huyo aligundua pia manganese na Glicerine. 

Miaka 267 iliyopita katika siku kama hii ya leo vilianza vita vya miezi 13 vya Madras. Vita hivyo vinahesabiwa kuwa mojawapo ya vita vikali zaidi vya kikoloni kati ya Uingereza na Ufaransa huko India.

Vita hivyo vilianza baada ya Ufaransa kuishambulia bandari ya Madras huko kusini mwa India, ambayo ilikuwa ikidhibitiwa na Waingereza. Ufaransa ilipigana ikiwa na wanajeshi elfu tatu dhidi ya Uingereza iliyokuwa na wapiganaji elfu 22.

Mwezi Januari mwaka 1761, Ufaransa ilisalimu amri mbele ya Uingereza baada ya kikosi cha dhiba kushindwa kufika vitani. 

Tarehe 18 Jumadithani miaka 166 iliyopita aliaga dunia faqihi na msomi mkubwa wa Kiislamu, Sheikh Murtadha Ansari katika mji mtakatifu wa Najaf huko Iraq.

Alizaliwa mwaka 1214 Hijria Shamsia katika mji wa Dezful nchini Iran na baada ya kupata elimu ya msingi kwa baba yake alielekea katika miji mitakatifu ya Karbala na Najaf huko Iraq kwa ajili ya elimu ya juu. Miaka kadhaa baadaye Sheikh Ansari alitambuliwa kuwa miongoni mwa wanazuoni na walimu mashuhuri wa zama hizo.

Msomi huyo wa Kiislamu ameandika vitabu vingi vikiwemo vile vya Rasaail na Makaasib ambavyo vingali vinatumiwa hadi sasa kufundishia katika vyuo vikuu vya kidini.

Miaka 64 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani tarehe 9 Disemba mwaka 1961 ardhi ya Tanganyika ambayo hii leo ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ilijikomboa na kupata uhuru.

Tanganyika ilianza kukoloniwa na Ujerumani mwaka 1880 hadi mwaka 1919 wakati ilipoanza kukoloniwa na Uingereza na kuendelea kuwa chini ya udhibiti wa mkoloni huyo hadi ilipopata uhuru na kujitawala katika siku kama ya leo. Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa Tanganyika na baadaye akachaguliwa kuwa Rais wa kwanza wa Tanganyika.

Mwaka 1964 Tanganyika iliungana na Zanzibar na kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. ***

Siku kama hii ya leo miaka 39 iliyopita, yalianza mapambano yasiyo na kikomo ya wananchi wa Palestina dhidi ya utawala ghasibu wa Israel katika Ukingo wa Magharibi mwa Mto Jordan na Ukanda wa Ghaza.

Mapambano hayo ya ukombozi ambayo ni mashuhuri kwa jina la "Intifadha ya Kwanza" yalianzishwa baada ya kushadidi mauaji na ukandamizaji wa Israel dhidi ya Wapalestina na pia kuendelea kukaliwa kwa mabavu ardhi zao na utawala huo ghasibu.

Hayo yalijiri baada ya wananchi Waislamu wa Palestina kukatishwa tamaa na hatua zilizokuwa zikichukuliwa na nchi za Kiarabu na taasisi nyingi za Palestina kwa ajili ya kurejeshewa haki zao.

Miaka 34 iliyopita katika siku kama hii ya leo, Umoja wa Mataifa ulitoa ripoti na kuutangaza utawala wa Baath wa Iraq kuwa ndio ulioanzisha vita vya miaka minane dhidi ya Iran.

Katika siku hiyo, Javier Perez de Cuellar Katibu Mkuu wa wakati huo wa Umoja wa Mataifa alitangaza katika ripoti yake kuwa Iraq iliivamia Iran tarehe 22 Septemba mwaka 1980.

Miji na vijiji vingi vya mpakani mwa Iran vilitekwa na kukaliwa kwa mabavu huku wanawake, watoto na wanaume wengi wakiwa wahanga wa vita hivyo vikubwa katika uvamizi huo ambao uliungwa mkono kwa hali na mali na nchi za Magharibi.

Siku kama ya leo miaka 32 iliyopita, Ayatullahil Udhma Sayyid Muhammad Ridha Golpayegani, alimu, fakihi mkubwa na mmoja wa marajii wakubwa wa Kiislamu ulimwenguni alifariki dunia.

Alizaliwa mjini Golpayegan moja ya miji ya Iran na kusoma masomo ya dini kwa maustadhi stadi na waliokuwa wametabahari kielimu katika zama hizo akiwemo Ayatullah Hairi.

Ayatullah Golpayegani alianza kufundisha katika Chuo Kikuu cha Kidini (Hawza) cha mjini Qum-Iran baada ya kuasisiwa kwake. Mwanazuoni huyo mkubwa ameandika vitabu vingi katika nyuga mbalimbali. 

Na tarehe 9 Disemba ni Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Ufisadi (rushwa).

Siku hii huadhimishwa kila mwaka tarehe 9 Desemba ili kuongeza uelewa wa umma kuhusu ufisadi na njia za kuupambana nao.

Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Rushwa ilianzishwa kufuatia kupitishwa kwa Mkataba wa Umoja wa Mataifa dhidi ya Rushwa mwaka wa 2003. Mkataba huo unautambua ufisadi kama tishio kubwa kwa utulivu wa jamii, maadili ya demokrasia, maendeleo endelevu na utawala wa sheria, na unasisitiza ushirikiano wa kimataifa ili kuzuia na kupambana nao. ****