Alkhamisi tarehe Mosi Disemba, 2016
Leo ni Alkhamisi tarehe Mosi Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1438 Hijria sawa na tarehe Mosi Disemba 2016.
Siku kama ya leo miaka 1438 iliyopita, Mtume Muhammad (saw) alianza Hijra yake ya kuhama Makka na kuelekea Madina, ikiwa imepita miaka 13 tokea alipobaathiwa na kupewa Utume. Mtume wa Allah alihama Makka kutokana na kushadidi vitimbi vya washirikina wa mji huo ambao walikusudia kumdhuru na kumuua wakati wa usiku akiwa amelala nyumbani kwake. Imam Ali AS alijitolea mhanga, kwa kuamua kulala kwenye kitanda cha Mtume, ili maadui wasitambue kwamba Mtume wa Allah ameondoka mjini Makka. Hijra ya Mtume (saw) na matukio ya baada yake yalikuwa na umuhimu mkubwa katika ustawi na maendeleo ya Uislamu kiasi kwamba tukio hilo lilitambuliwa kuwa mwanzo wa kalenda ya Kiislamu. Ni vyema kukumbusha hapa kuwa Mtume (saw) ndiye aliyekuwa wa kwanza kutumia hijra yake kama mwanzo wa kalenda ya Kiislamu kwani barua zote zilizoandikwa na mtukufu huyo kwa wakuu wa makabila na shakhsia maarufu alizisajili kwa kalenda hiyo.

Tarehe Mosi Rabiul Awwal miaka 1373 iliyopita, ilianza harakati ya Tawwabin kwa lengo la kulipiza kisasi cha kuuawa shahidi Imam Hussein AS pamoja na wafuasi wake watiifu. Awali, watu wa Kufa walimuomba Imam Hussein AS aelekee mjini humo kwa lengo la kuongoza harakati dhidi ya utawala wa kidhalimu wa Yazid bin Muawiya lakini alizingirwa njiani na jeshi la mtawala dhalimu, Yazid bin Muawiya, na kuuawa shahidi. Tawwabin ni kundi la watu wa Kufa ambalo lilijuta kwa kushindwa kutekeleza ahadi yake na kumuacha Imam Hussein na wafuasi wake wachache peke yao wapambane na majeshi ya Yazid. Kwa minajili hiyo watu hao walitubia makosa yao na kuamua kuanzisha harakati ya kulipiza kisasi wakiongozwa na Sulaiman bin Sorad dhidi ya jeshi la Yazid. Kundi hilo lilipigana kishujaa na jeshi la Yazid na wengi kati ya wapiganaji wake wakauawa shahidi.

Tarehe Mosi Disemba kila mwaka, nchi mbalimbali duniani huadhimisha Siku ya Kimataifa ya Ukimwi. Ukimwi ni ugonjwa wa kuambukiza ambao unatokana na kurundikana kwa virusi vya HIV mwilini ambavyo huharibu mfumo wa ulinzi wa mwili na kutayarisha mazingira ya kushambuliwa na maradhi nyemelezi. Ugonjwa huu ulibainika kwa mara ya kwanza kabisa nchini Marekani mwazoni mwa miaka ya 1980. Wakati huo baadhi ya wanaume wanaofanya mapenzi kinyume na maumbile huko New York na California waligundulika kuwa na kansa ambazo hazikukubali tiba ya aina yo yote. Japokuwa wakati huo, haikujulikana sababu ya maambukizi ya ghafla ya magonjwa hayo lakini tukio hilo limetambuliwa kuwa ndiyo mwanzo wa kujitokeza maradhi ya Ukimwi. Ugonjwa huo ambao haukuwa na jina ulienea kwa kasi kubwa katika kipindi cha mwaka mmoja na hatimaye mwaka 1982 ulipewa jina la Ukimwi.

Miaka 191 iliyopita katika siku kama hii ya leo, muungano wa kihistoria wa nchi za Ulaya au Muungano Mtakatifu ulisambaratika baada ya kujiengua utawala wa Kikaizari (Tsarist) wa Russia katika muungano huo. Muungano huo uliundwa kati ya tawala za Russia, Austria na ufalme wa Pros baada ya kuanguka kwa utawala wa Napoleon na kufanyika Congress ya Vienna, na kwa mujibu wake tawala hizo ziliafikiana kwamba nchi zilizo chini ya mamlaka ya muungano huo zifuate misingi ya dini ya Kikristo katika uhusiano wa kimataifa.

Siku kama ya leo miaka 95 iliyopita, Mirza Kuchak Khan Jangali, mwanaharakati na mpigania ukombozi wa Kiirani aliuawa shahidi na vibaraka wa Reza Khan, dikteta wa wakati huo wa Iran kwa ushirikiano wa madola ya Umoja wa Kisovieti na Uingereza. Mirza Kuchak Khan Jangali alijifunza masomo ya dini akiwa katika rika la ujana na kufanikiwa kukwea daraja za juu za kielimu. Baadaye alijiunga na safu ya wapigania uhuru hadi alipokamatwa na vibaraka wa Reza Khan na kuuawa kwa kukatwa kichwa kilichopelekwa kwa mfalme huyo kibaraka.
