Jan 03, 2017 10:37 UTC

Sura ya Al-Qas’as’, aya ya 70-75 (Darsa ya 698)

 

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 698, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 28 ya Al-Qas’as’. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 70 ambayo inasema:

وَهُوَ اللَّهُ لا إِلَهَ إِلاَّ هُوَ لَهُ الْحَمْدُ فِي الأُولَى وَالآخِرَةِ وَلَهُ الْحُكْمُ وَإِلَيْهِ تُرْجَعُونَ

Naye ni Mwenyezi Mungu, hapana mungu isipo kuwa Yeye. Sifa zote njema ni zake Yeye, mwanzo na mwisho. Na hukumu ni yake Yeye. Na kwake Yeye mtarejeshwa.

Katika darsa kadhaa zilizopita tulisoma aya za Qur’ani ambazo zilikana kila namna ya kumfanyia Allah SW mshirika, iwe ni mshirika katika uumbaji au mshirika katika kuabudiwa. Aya hii tuliyosoma inaashiria tauhidi ya Uola na kuhoji: ni maabudu gani ambaye anashirikiana na Mwenyezi Mungu katika kukuteremshieni neema? Neema zote za kimaada na kimaanawi zinazokufikieni zinatoka kwake Yeye Mola; kwa hivyo ni Yeye tu anayestahiki kuhimidiwa na kushukuriwa. Ni Yeye tu ndiye mfalme na mtawala wa ulimwengu huu na ulimwengu wa akhera. Ghairi ya Yeye, ni nani mwengine mwenye nguvu na uwezo wa kuuamuru na kuuendesha ulimwengu wenye adhama kama huu? Na mwishoni mwa uhai wenu marejeo yenu pia ni kwake Yeye, si kwa maabudu na miungu bandia na ya kubuni inayoabudiwa na washirikina. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba kuabudu na kunyenyekea kunamstahikia Yule tu ambaye mwanzo na mwisho wa mwanadamu pamoja na ulimwengu viko mikononi mwake. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa mamlaka ya uumbaji wa Allah wa viumbe wote wa ulimwengu na mamlaka ya upangaji sharia kwa ajili ya maisha ya wanadamu yanatokana na uumbaji wake na mamlaka yake juu ya viumbe wote.

Tunaiendeleza darsa yetu hii kwa aya ya 71, 72 na 73 ambazo zinasema:

قُلْ أَرَأَيْتُمْ إِن جَعَلَ اللَّهُ عَلَيْكُمُ اللَّيْلَ سَرْمَدًا إِلَى يَوْمِ الْقِيَامَةِ مَنْ إِلَهٌ غَيْرُ اللَّهِ يَأْتِيكُم بِضِيَاء أَفَلا تَسْمَعُونَ

Sema: Mwaonaje, Mwenyezi Mungu angeli ufanya usiku umekukalieni moja kwa moja mpaka Siku ya Kiyama, mungu gani asiye kuwa Mwenyezi Mungu atakaye kuleteeni mwangaza? Basi je, hamsikii?

قُلْ أَرَأَيْتُمْ إِن جَعَلَ اللَّهُ عَلَيْكُمُ النَّهَارَ سَرْمَدًا إِلَى يَوْمِ الْقِيَامَةِ مَنْ إِلَهٌ غَيْرُ اللَّهِ يَأْتِيكُم بِلَيْلٍ تَسْكُنُونَ فِيهِ أَفَلا تُبْصِرُونَ

Sema: Mwaonaje, Mwenyezi Mungu angeli ufanya mchana umekukalieni moja kwa moja mpaka Siku ya Kiyama, mungu gani asiye kuwa Mwenyezi Mungu ataye kuleteeni usiku mkapumzika humo? Basi je, hamwoni?

وَمِن رَّحْمَتِهِ جَعَلَ لَكُمُ اللَّيْلَ وَالنَّهَارَ لِتَسْكُنُوا فِيهِ وَلِتَبْتَغُوا مِن فَضْلِهِ وَلَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ

Na katika rehema zake amekufanyieni usiku na mchana mpate kupumzika humo na mtafute fadhila zake, na ili mpate kushukuru. 

Aya hizi zinaashiria utawala na mamlaka mutlaki ya Allah kwa ulimwengu wa maumbile na vilivyomo ndani yake na kueleza kwamba: Ikiwa Mwenyezi Mungu ataizuia sayari ya ardhi isizunguke kwa  namna ambayo kila mahala ambako hivi sasa ni mchana kuendelee kubaki kuwa mchana hadi mwisho wa dunia, na kila mahala ambako hivi sasa ni usiku kuendelee kuwa usiku hadi mwisho wa dunia, ni nani katika hao miungu wenu bandia na wa kubuni mnaowaabudu aliye mweza wa kuiendesha tena dunia na kuugawa usiku na mchana katika pembe mbalimbali za sayari ya ardhi?

Je mmejaribu kutafakari na kubaini kuwa huu mzunguko wenye mlingano wa usiku na mchana ni neema kubwa iliyoje kwenu na kwa viumbe vyote vilivyo hai? Laiti kama mwangaza na joto la jua vingekuwa haviko kwenye nusu moja ya dunia, bila ya shaka yoyote maisha na uhai katika upande huo yangekaribia kutoweka; na laiti kama nusu ya sayari ya dunia ingekuwa muda wote inapigwa na mwangaza na joto la jua viumbe vingi hai visingeweza kuhimili hali hiyo na vingekufa na kutoweka. Harakati ya sayari ya dunia ya kujizunguka yenyewe inasababisha kuwepo usiku na mchana vinavyopishana kwa nidhamu maalumu na ndani ya muda mfupi, huku kiwango cha joto kikipungua kuanzia jua linapozama na kuanza kuongezeka pale linapochomoza. Japokuwa mwangaza na joto ni vitu vya lazima kwa maisha ya mtu na viumbe vingine vyote hai lakini giza la usiku na kupungua kwa joto husaidia kuandaa mazingira ya kupumzika mtu pamoja na viumbe wengine wengi. Hii yenyewe ni neema kubwa ambayo haizingatiwi na kushukuriwa kama inavyostahiki. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kuwataka watu watalii na kutafakari juu ya mfumo unaoendesha ulimwengu, nidhamu na tadbiri inayotawala ndani yake ni miongoni mwa njia bora za kuijua tauhidi na kumjua Mwenyezi Mungu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa usiku ni kwa ajili ya utulivu na mapumziko; na mchana ni kwa ajili ya harakati na kufanya kazi. Aidha aya hizi zinatuelimisha kwamba katika kuwaongoza na kuwaelekeza watu kwenye uongofu tutumie njia ya uulizaji masuali yenye kutoa mwamko na kuwafanya wakusudiwa watafakari wao wenyewe na kubaini kuwa Uislamu ndio dini ya haki. Kadhalika tunajifunza kutokana na aya hizi kuwa kuzijua neema humfanya mtu awe mshukurivu kwa Muumba wake. Tujitahidi kuwaelimisha na kuwajulisha neema za Allah chipukizi na vijana ili waingiwe na raghba na hamu zaidi ya kumwabudu Mwenyezi Mungu.

Darsa yetu ya leo inahatimishwa na aya ya 74 na 75 ambazo zinasema:

وَيَوْمَ يُنَادِيهِمْ فَيَقُولُ أَيْنَ شُرَكَائِيَ الَّذِينَ كُنتُمْ تَزْعُمُونَ

 Na siku atakapo waita na akasema: Wako wapi hao mlio kuwa mkidai kuwa ni washirika wangu?

وَنَزَعْنَا مِن كُلِّ أُمَّةٍ شَهِيدًا فَقُلْنَا هَاتُوا بُرْهَانَكُمْ فَعَلِمُوا أَنَّ الْحَقَّ لِلَّهِ وَضَلَّ عَنْهُم مَّا كَانُوا يَفْتَرُونَ

Na tutatoa shahidi katika kila umma, na tutasema: Leteni hoja zenu! Hapo watajua kwamba haki kweli ni ya Mwenyezi Mungu, na yatawapotea yale waliyo kuwa wakiyazua.

Qur’ani tukufu inaliuliza tena suali lilelile ililouliza katika aya ya 62 ya sura hii ya Al-Qas’as kwa kusema: Wale ambao duniani, badala ya Mwenyezi Mungu waliwaendea na kuwaabudu wanadamu wenzao au viumbe wengine kwa kudhani kwamba majaaliwa yao yako mikononi mwao wao, watasimamishwa na kusailiwa mbele ya mahakama ya Siku ya Kiyama. Wakiwa mbele ya Mitume wa kila umma ambao walifanya kazi ya tablighi ya kuwalingania na kuwafikishia watu wao wito wa haki, watu hao watatakiwa watoe sababu yenye kukubalika, na kueleza kwa nini waliamua kuwaendea miungu bandia licha ya kuwepo Mtume na njia za kuweza kumjua Mola wa ulimwengu? Kisha aya zinaendelea kueleza kwamba, hapo ndipo wataelewa kuwa maabudu na miungu wao hao si lolote si chochote na wala hawana wanachoweza kufanya; na kwamba haki iko kwa Allah SW tu na Mitume wake. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kukumbushwa kuhusu mandhari ya Siku ya Kiyama ndani ya Qur’ani kunalenga kuwaonya na kuwatahadharisha waumini kuwa shirki ni hatari kubwa; na kama hawatojichunga, nao pia wanaweza kutumbukia kwenye lindi la shirki. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa Mitume na mawalii wa Allah ni miongoni mwa mashahidi katika mahakama ya Siku ya Kiyama. Kwa hivyo tutahadhari Mtume asije katika mahakama hiyo akawa mlalamikaji dhidi yetu, bali aje atushufaie na kuwa muombezi wetu. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kuwa shirki haina hoja imara wala burhani yoyote yenye mashiko. Na vilevile aya hizi zinatutaka tuelewe kuwa huko akhera viza vyote vya mghafala vitatoweka, na haki na hakika zitathibiti na kudhihiri kwa uwazi kabisa. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 698 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah aufanye mwema mwisho wetu na kuwa miongoni mwa wale ambao Siku ya Kiyama watastahiki kupata shifaa na uombezi wa Mtume wetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/