Suratul Qas'as 83-85 (701)
Sura ya Al-Qas’as’, aya ya 83-85 (Darsa ya 701)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 701, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 28 ya Al-Qas’as’. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 83 ambayo inasema:
تِلْكَ الدَّارُ الآخِرَةُ نَجْعَلُهَا لِلَّذِينَ لا يُرِيدُونَ عُلُوًّا فِي الأَرْضِ وَلا فَسَادًا وَالْعَاقِبَةُ لِلْمُتَّقِينَ
Hayo ndiyo makaazi ya Akhera, tumewafanyia wale wasio taka kujitukuza duniani wala ufisadi. Na mwisho mwema ni wa wachamngu.
Katika darsa iliyopita tulizungumzia hatima ya Qarun na kuangamizwa kwake kwa sababu ya kuasi na kuleweshwa na mali na utajiri wake. Aya hii tuliyosoma inatoa hitimisho jumla juu ya tukio hilo na kueleza kwamba: Watu wanaojitukuza na kujiona bora kuliko wenzao na kutaka wawe juu ya wanadamu wenzao wajue kwamba makazi yao huko Akhera hayatokuwa peponi kwa sababu Pepo ni makao ya waja safi na wachaMungu.
Kiburi na uistikbari ambazo ni sifa chafu za matajiri na wenye madaraka wapenda dunia, huwa sababu ya kufisidika wao wenyewe; na pia utajiri wao na madaraka yao husababisha kuenea ufisadi katika jamii. Imeelezwa katika historia kwamba wakati Imam Ali (AS) alipokuwa kiongozi wa utawala wa Kiislamu alikuwa akiwaambia watu: “Kama ambavyo mimi sijayafanya madaraka wenzo wa kujikwezea na kujiona bora kuliko watu wengine, matajiri nao wasiufanye uwezo wa mali walionao wenzo wa kuwatawala watu wengine.” Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba kuwa na mali na utajiri na nguvu za madaraka tu, peke yake havisababishi ufisadi kwa mtu. Kinachosababisha kujitokeza na kuenea ufisadi ni kujikweza na kutaka kuwa juu ya wengine kwa sababu ya mali na madaraka. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa mchaMungu wa kweli ni mtu aliye mnyenyekevu asiye na majigambo wala kutaka kujikweza juu ya wengine.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 84 ambayo inasema:
مَن جَاءَ بِالْحَسَنَةِ فَلَهُ خَيْرٌ مِّنْهَا وَمَن جَاءَ بِالسَّيِّئَةِ فَلا يُجْزَى الَّذِينَ عَمِلُوا السَّيِّئَاتِ إِلاَّ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ
Atakaye tenda wema atapata malipo bora kuliko huo wema alio utenda. Na atakaye tenda uovu, hawalipwi watendao uovu ila waliyo kuwa wakiyatenda.
Baada ya maelezo ya aya iliyotangulia, aya hii inaashiria kaida na kununi kuu ya utoaji malipo ya adhabu na thawabu kwa waja huko akhera na kueleza kwamba: Wakati Allah SW anapolipa thawabu huangalia uraufu na fadhila zake kwa waja wake, si uzito na thamani halisi ya amali zao. Kwa sababu hiyo thamani ya malipo ya thawabu mara zote huwa makubwa na ya juu zaidi kulinganisha na thamani ya amali zenyewe njema za watu. Baadhi ya wakati hulipa mara kumi zaidi ya malipo halisi, wakati mwengine mara mia zaidi, wakati mwengine mara mia saba, na mara nyengine kwa kiwango na idadi isiyohesabika.
Ni wazi kuwa uraufu, rehma na fadhila za Allah hutegemea pia ikhlasi na usafi wa nia ya mtu; hivyo amali hazitokuwa na malipo sawa, bali zitakuwa na thawabu tofauti kulingana na ikhlasi na nia tofauti za watu.
Ama kuhusu madhambi na matendo maovu, Allah SW hutumia uadilifu wake katika kuwalipa waja wake. Kwa hivyo adhabu ya kila dhambi hulipwa kulingana na athari za ubaya wa amali ovu yenyewe. Athari ambazo, baadhi ya wakati yamkini zikaendelea kubaki kwa miaka na karne baada ya kufa mtu na kusababisha kuenea ufisadi, maovu na madhambi katika jamii.
Nukta ya kutaamali ni kwamba aya hii haielezi kuwa Mwenyezi Mungu atawaadhibu watenda madhambi, bali inasema: Adhabu yao itakuwa ni yaleyale waliyofanya wao wenyewe. Yaani yale waliyoyatenda watu yatajidhihirisha na kujionesha Siku ya Kiyama katika sura na umbo linalolingana na matendo yenyewe. Na kimsingi ni hizo amali zao wenyewe watu ndizo zitakazowaletea maudhi na machungu siku hiyo.
Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba amali njema, ikifanywa na mtu yeyote yule inapendeza na ina malipo. Ima duniani au akhera! Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa kufanya amali na tendo jema tu hakutoshi; muhimu zaidi ni kuifikisha salama amali hiyo Siku ya malipo na hesabu. Kwani si hasha kufanya dhambi, kusimbulia, kutosheka mtu na mema yake, ghururi na ria vikaifanya amali njema ya mtu ipotee wala isifike kwenye uwanja wa malipo Siku ya Kiyama. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba Mwenyezi Mungu hulipa thawabu za amali njema kulingana na fadhila zake; lakini malipo ya adhabu ya wafanya madhambi anayalipa kulingana na uadilifu wake.
Darsa ya 701 ya Qur'ani inahatimishwa na aya ya 85 ambayo inasema:
إِنَّ الَّذِي فَرَضَ عَلَيْكَ الْقُرْآنَ لَرَادُّكَ إِلَى مَعَادٍ قُل رَّبِّي أَعْلَمُ مَن جَاءَ بِالْهُدَى وَمَنْ هُوَ فِي ضَلالٍ مُّبِينٍ
Hakika aliye kufaradhishia kuifuata Qur'ani hapana shaka atakurudisha pahala pa marejeo. Sema: Mola wangu Mlezi ndiye anaye mjua zaidi mwenye kuja na uwongofu, na aliyemo katika upotofu ulio dhaahiri.
Aya hii na nyengine tatu zinazofuatia ambazo ni aya za mwisho za sura hii ya Al- Qas'as' zinamhutubu Bwana Mtume Muhammad SAW kwamba kwa amri ya Allah SW anapaswa kuhajiri kwa kuhama Makka na kuhamia Madina. Washirikina wa Kikureishi, ambao walikuwa na mali na nguvu kubwa za mamlaka hawakuwaruhusu watu wamwamini na kumfuata Bwana Mtume SAW; na kila aliyeukubali wito wa haki wa Nabii huyo wa rehma walimwandama kwa anuai za mateso na maudhi. Mpaka ikafika hadi wakawasusia na kuwawekea mzingiro wa kiuchumi na kijamii kwa muda wa miaka mitatu, hata hao Waislamu wachache waliomwamini Bwana Mtume Muhammad SAW na kuwafanya wawe katika hali ngumu kabisa. Lakini baada ya washirikina hao kuvunjika moyo kwa kuona hawakupata walilolitaka la kuizima nuru ya Uislamu, waliazimia kumuua Bwana Mtume SAW. Ni kutokana na kufikia hatua hiyo ndipo Mwenyezi Mungu SW akamwamuru Mtume wake ahame Makka na kuhamia Yathrib.
Kwa upande mmoja Bwana Mtume SAW alikuwa akitaka kubakia Makka kwa sababu ndiko alikozaliwa na ndipo ilipokuwepo Nyumba ya Allah ya Al-Ka’ba. Na kwa upande mwengine ilimbidi auhame mji huo ili kuweza kuutangaza na kuueneza wito wake wa haki kwa uhuru. Katika aya hii tuliyosoma, Qur'ani tukufu inamuelekea Bwana Mtume na kumwambia: Mwenyezi Mungu ambaye, amekuteremshia wewe Qur'ani na kukuamuru uhajiri, anakupa ahadi kuwa atakurudisha kwenu Makka ulikozaliwa; tena katika wakati ambapo, badala ya washirikina, wewe na waliokuamini mtakuwa ndio wenye mamlaka na madaraka.
Kisha aya inaendelea kumueleza Bwana Mtume kwamba: Waambie hao wanaoukanusha ujumbe wako na wanashupalia kufru na ukadhibishaji wao kwamba: Japokuwa nyinyi mnaukufuru ujumbe wangu, lakini Mwenyezi Mungu anajua zaidi ni nani aliyetumwa na Yeye kuja kuwaongoza watu na kuwafikisha kwenye nuru ya haki na uongofu; na nani aliye kwenye dhalala na upotofu, asiye tayari kuukubali uongofu wa Mola.
Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba kuteremshwa aya za Qur'ani na kufikishwa kwa watu kulikabiliwa na upinzani wa makafiri na hatimaye kumfanya Bwana Mtume SAW ahajiri Makka na kuhamia Madina; lakini Mola wa Qur'ani akampa ahadi Mtume wake kuwa atamrejesha Makka akiwa na izza na heshima. Na naam, ahadi hiyo ikathibiti na mtukufu huyo akarudi Makka. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa kutekeleza faradhi si kusali na kufunga tu, bali kusoma na kuitangaza Qur'ani na kuwalingania watu kukifuata Kitabu hicho cha mbinguni pia ni faradhi na wajibu kwa muumini. Wapenzi wasikilizaji, darsa yetu ya leo ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah aupe nusra na ushindi Uislamu na Waislamu na awadhalilishe maadui wote wa dini yake ya haki. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/