Jan 03, 2017 10:49 UTC

Sura ya Al-Qas’as’, aya ya 86-88 (Darsa ya 702)

 

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 702, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 28 ya Al-Qas’as’. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 86 ambayo inasema:

وَمَا كُنتَ تَرْجُو أَن يُلْقَى إِلَيْكَ الْكِتَابُ إِلاَّ رَحْمَةً مِّن رَّبِّكَ فَلا تَكُونَنَّ ظَهِيرًا لِّلْكَافِرِينَ

Nawe hukuwa unataraji kuletewa Kitabu; lakini ni rehema tu ya Mola wako Mlezi. Basi usiwe msaidizi wa makafiri.

Katika aya ya 85 ya sura hii ambayo tuliisoma katika darsa iliyopita, Mwenyezi Mungu Mtukufu amempa ahadi Mtume wake, Nabii Muhammad SAW kwamba baada ya kuhajiri kuelekea Madina atamrejesha tena Makka na atamwezesha kuwashinda makafiri. Madhumuni ya aya tuliyosoma ni kwamba, kama ambavyo ewe Nabii Muhammad hukuwa ukitarajia kwamba utarudi tena Makka ukiwa na nguvu na mwenye izza, lakini Allah SW akataka iwe hivyo na ikawa, hukuwa pia ukijitarajia nafsi yako kwamba utabaathiwa kwa kupewa Utume na kuteremshiwa Kitabu cha mbinguni, lakini kwa hekima yake, Mwenyezi Mungu SW amekurehemu kwa rehma zake maalumu na kukufanya Mtume.  Kutokana na hayo usikubali katu kusalimu amri na kuridhia matakwa yasiyostahiki ya washirikina na makafiri kwa sababu hiyo ni namna fulani ya kuwasaidia wao; kwa hivyo waoneshe na watangazie waziwazi na kwa mkato kabisa kwamba unachukizwa na wanayoyafanya.

Katika aya zilizopita za sura hii hii ya al-Qas'as' tulisoma kuwa Nabii Musa (AS) alikwenda mlima Turi kwa madhumuni ya kutafuta kijinga cha moto ili aweze kuota moto na kupata joto yeye mwenyewe pamoja na ahli zake, lakini alipofika huko akabaathiwa na kupewa Utume. Kuhusu Bwana Mtume Muhammad SAW, mapokezi ya historia yanaeleza kuwa mtukufu huyo alikuwa akienda kwenye mlima Nuru katika pango la Hira kwa ajili ya kufanya ibada na kudhihirisha uja wake kwa Mola na ndipo akateremkiwa na Jibril na kumpa bishara njema ya kubaathiwa na kupewa Utume. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba moja ya visingizio walivyokuwa wakitoa makafiri vya kutoiamini haki ni kwamba kwa nini wao pia hawateremshiwi wahyi? Qur'ani inasema: Mitume, ambao ni waja wenye nyoyo safi, na ambao waliiishi maisha yao kwa utoharifu na utakasifu wa nafsi hawakuwa wakitarajia kupewa neema hiyo na Allah itakuwa nyinyi makafiri!? Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa katika chuo cha mafundisho ya Mitume ni marufuku kufanya jambo lolote litakalowaimarisha na kuwapa nguvu makafiri na madhalimu.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 87 ambayo inasema:

وَلا يَصُدُّنَّكَ عَنْ آيَاتِ اللَّهِ بَعْدَ إِذْ أُنزِلَتْ إِلَيْكَ وَادْعُ إِلَى رَبِّكَ وَلا تَكُونَنَّ مِنَ الْمُشْرِكِينَ

Wala wasikuzuie kuzifuata Aya za Mwenyezi Mungu baada ya kuteremshiwa wewe. Na lingania kwa Mola wako Mlezi, wala usiwe kabisa miongoni mwa washirikina.

Aya hii inataja moja ya vielelezo vya mifano hai iliyoashiriwa katika aya iliyotangulia ambayo ilisema: 'usiwe msaidizi kwa makafiri.' Na sababu ni kwamba kuacha tablighi ya kutangaza aya za kitabu cha Allah na kuzembea katika kuwalingania watu wito wa tauhidi huifanya kufru na shirki zipate nguvu. Imeelezwa katika historia kwamba kila Bwana Mtume Muhammad SAW alipokuwa akiwasomea watu aya za Qur'ani na kuwaita wasikilize maneno hayo ya Allah, washirikina na wapinzani wa haki walikuwa wakimtuhumu mtukufu huyo kuwa ni mshairi, kuhani na msemaji maneno ya khurafa na uzushi. Aya tuliyosoma inasema: Ewe Mtume usirudi nyuma katika kutekeleza jukumu lako; kwani kama utafanya hivyo nawe pia utakuwa miongoni mwa washirikina na hutokuwa na tofauti yoyote na wao mbele ya Allah. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba maadui wa dini wana mipango na njama wanazopanga hata dhidi ya Mitume wa Allah na wala hawazembei katika kushamirisha na kueneza kufru na shirki. Kwa sababu hiyo tunapaswa kuwa na bidii na idili katika kuilinda dini yetu na kutokuwa walegevu na wazembe katika kuwalingania watu dini tukufu ya Uislamu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa Mitume wanalelewa chini ya uangalizi wa Allah SW; na Yeye Mola ndiye anayewakumbusha kwa maamrisho na makatazo yake ili kuhakikisha wanaitekeleza kwa usahihi kazi ya kufikisha ujumbe wake kwa watu. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba Mitume walikuwa wakiwalingania watu wito wa Mwenyezi Mungu, si wito wao wao; na kupambana na kufru na shirki ilikuwa ndio maudhui kuu ya kazi yao.

Darsa ya 702 ya Qur'ani inahatimishwa na aya ya 88 ambayo inasema:

وَلا تَدْعُ مَعَ اللَّهِ إِلَهًا آخَرَ لا إِلَهَ إِلاَّ هُوَ كُلُّ شَيْءٍ هَالِكٌ إِلاَّ وَجْهَهُ لَهُ الْحُكْمُ وَإِلَيْهِ تُرْجَعُونَ

Na wala usimwombe pamoja na Mwenyezi Mungu mungu mwenginewe. Hapana mungu ila Yeye. Kila kitu kitaangamia isipo kuwa Dhati Yake. Hukumu iko kwake, na kwake mtarejeshwa.

Katika aya zilizotangulia tumeona jinsi Mwenyezi Mungu mtukufu alivyomtahadharisha Mtume wake na kufanya ajizi na kuzembea katika kuwalingania watu na kufikisha aya za kitabu cha haki cha Qur'ani. Aya hii ya 88 inaendeleza maudhui hiyo na kueleza kwamba kila mtu mwenye maarifa ya tauhidi na ya kumjua Mwenyezi Mungu hamfanyi yeyote kuwa mshirika katika kumwabudu Allah, kwa sababu anajua, ghairi ya Yeye Mola, vingine vyote ni vyenye kumalizika na kutoweka. Ni Yeye Allah pekee ndiye anayebakia milele; kwa hivyo amali yoyote inayofanywa kwa ajili ya Allah ifanywe kwa ikhlasi. Isitoshe ni kwamba utawala na mamlaka mutlaki juu ya ulimwengu wa maumbile ni ya Mwenyezi Mungu tu SW na ni jambo lisilokuwa na maana kumwabudu mwengine yeyote ghairi ya Yeye. Katika aya hii viumbe vyote vya ulimwengu vimetajwa kuwa ni  'faanin' yaani 'vitowekaji', kwa sababu iwe ni sasa au baadaye vitatoweka na kuangamia. Aidha ni vitowekaji kwa sababu hata katika muda huu wa kuwepo kwao huo ujudi wao hautokani na wao wenyewe, na endapo Allah SW ataondoa na kusitisha rehma zake kwao kwa lahadha ndogo tu, viumbe vyote vitaangamia.

Baada ya aya iliyotangulia iliyogusia shirki, aya hii imetoa tafsiri na maana ya shirki kwa kueleza kuwa ni kumwomba na kumfanya mwengine kuwa Mungu. Kinyume na Mawahabi ambao wanakuchukulia kutawasali kwa Mtume na mawalii wa Allah kuwa ni shirki, kutawasali kwa watukufu hao si shirki. Kwa sababu hakuna mtu yeyote anayemchukulia Bwana Mtume SAW au Imam Ali (AS) au mawalii wengine watoharifu wa Allah kuwa na mamlaka wenyewe kama wao tu bila ya kuwa na utegemezi kwa Mola; bali wao wanawahutubu wao kwa sura ya kuwa ni waja wakubwa na wateule waliojitolea na kufanya jithada isiyo na mfano katika kueneza dini ya tauhidi. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba mfuasi halisi wa tauhidi na mpwekeshaji wa kweli wa Allah ni yule aliyejivua pingu za maabudu wote ghairi ya Mola na akasimama imara kukabiliana na mataghuti na wale wanaojifanya watawala wa dunia wakataka wakaazi wote wa sayari hii ya dunia wafuate amri na maamuzi yao. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa dunia na vilivyomo ndani yake vinatoweka, na mkabala na hilo, Allah na vile vyenye rangi ya ilhamu ya Allah vinabakia. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba maana ya mauti si kutoweka na kumalizika bali ni kurejea kwenye asili na kianzio cha ulimwengu. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 702 ya Qur'ani imefikia tamati. Na darsa hii imekamilisha tarjumi na maelezo ya sura ya 28 ya Al-Qas'as'.Tunamwomba Allah atuwafikishe kuyafanyia kazi yote tuliyojifunza katika sura hii. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/