Feb 16, 2017 04:08 UTC
  • Alkhamisi 16 Februari, 2017

Leo ni Alkhamisi tarehe 18 Jamadil Awwal 1438 sawa na tarehe 16 Februari 2017.

Siku kama ya leo miaka 25 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 16 Februari 1992 aliuawa shahidi Sayyid Abbas Musawi, Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya nchini Lebanon katika shambulio lililofanywa na ndege za utawala wa Kizayuni wa Israel huko kusini mwa nchi hiyo. Shambulio hilo lilipelekea kuuawa pia watu kadhaa waliokuwa wameandamana naye akiwemo mke na mwanawe mdogo, pamoja na wasaidizi wake watatu. Shambulio hilo lilitokea wakati Sayyid Abbas Musawi alipokuwa akirejea nyumbani kutoka kwenye kumbukumbu za kuuawa shahidi Sheikh Raghib Harb aliyeuliwa na maafisa wa utawala huo miaka michache iliyopita kabla ya hapo. Sheikh Raghib Harb alikuwa mwasisi wa harakati za mapambano huko kusini mwa Lebanon. Hujuma hiyo ilizusha hasira kubwa za Waislamu kote ulimwenguni dhidi ya Israel. Hata hivyo madola ya Magharibi yanayodai kutetea haki za binadamu, si tu hayakulaani jinai hiyo bali pia yalijaribu kuihalalisha. Baada ya kuuawa shahidi Sayyid Abbas Musawi, Sayyid Hassan Nasrullah alichukua jukumu la kuwa Katibu Mkuu wa Hizbullah, na kutoa pigo kwa Israel mwaka 2000, baada ya kuyafukuza kwa madhila majeshi ya utawala huo katika ardhi za kusini mwa Lebanon.

Sayyid Abbas Musawi

Siku kama leo miaka 71 iliyopita, inayosadifiana na 16 Februari 1946 kwa mara ya kwanza kura ya veto ilitumiwa na mjumbe wa Urusi ya Zamani katika Umoja wa Mataifa. Siku hiyo mwakilishi wa Urusi, alipinga moja ya mapendekezo ya Baraza la Usalama na kutumia kwa mara ya kwanza haki ya veto. Haki ya kura ya veto inayolalamikiwa na mataifa mengine duniani zimepewa nchi tano tu wanachama wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambazo ni Marekani, Uingereza, Ufaransa, China na Russia. Mpango wa kutumia veto ulipasishwa na Marekani, Uingereza na Urusi ya Zamani katika mkutano wa Yalta wa mwaka 1945. Tangu wakati huo kumekuwa na malalamiko ya kupinga kupewa nchi hizo tu kura hiyo ya veto, hasa kwa kuzingatia kuwa, baadhi ya nchi hizo zimekuwa zikiitumia haki hiyo kwa malengo ya kisiasa.

Katika siku kama ya leo miaka 988 iliyopita, Abu al-Abbas Ahmad bin Ali maarufu kwa lakabu ya Najashi aliaga dunia huko Samarra Iraq akiwa na umri wa miaka 78. Najashi alikuwa alimu na msomi mashuhuri katika karne ya tano Hijria na alikuwa amebobea na kutabahari katika elimu ya hadithi na wapokezi wa hadithi.

ابوالعباس احمد بن علی نجاشی

Katika siku kama ya leo miaka 1110 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria alifariki dunia Ahmad bin Muhammad mashuhuri kwa jina la Ibn Abdu Rabbuh mshairi na mwandishi mahiri wa Kiarabu. Abdu Rabbuh alibobea mno katika mashairi. Athari yake mashuhuri inaitwa Aqd al-Farid ambayo inahusiana na historia, lugha na mashairi. Malenga huyo pia ameandika mashairi mengi.

احمد بن محمد (ابن عبد ربه)