Jumatatu 26 Juni, 2017
Jumatatu tarehe Mosi Shawwal 1438 Hijria sawa na Juni 26, 2017
Leo ni Jutatu tarehe Mosi Shawwal inayosadifiana na Idi tukufu ya al-Fitr. Idul Fitri ni miongoni mwa sikukuu kubwa katika dini tukufu ya Kiislamu. Baada ya kukamilisha ibada ya funga, kuomba na kujipinda kwa ibada katika mwezi mtukufu wa Ramadhani, Waislamu hufanya sherehe katika siku hii kubwa wakimshukuru Mola manani kwa kuwawezesha kukamilisha ibada huyo. Idi al Fitr ni kuuaga mwezi mtukufu wa Ramadhani ambao ni mwezi wa ibada na kujisafisha. Katika siku hii ya leo ni haramu kufunga saumu yoyote na Waislamu baada ya juhudi za mwezi mzima za kupambana na nafsi na kuchuma matunda ya ucha-Mungu hukusanyika pamoja na kusali Swala ya Idul Fitr. Kuhusiana na utukufu wa siku hii Mtukufu Mtume (saw) anasema: "Mtu yeyote atakayemuasi Mwenyezi Mungu katika siku ya Idi, basi ni kama mtu aliyemuasi Mwenyezi Mungu siku ya miadi- yaani Siku ya Kiama." Kwa mnasaba wa siku hii adhimu, Redio Tehran inatoa mkono wa pongezi, heri na fanaka kwa Waislamu wote duniani.

Siku kama ya leo miaka 1185 iliyopita yaani tarehe Mosi Shawwal mwaka 256 Hijria Qamariya mpokezi mashuhuri wa hadithi wa Ahlusunna, Imam Bukhari aliaga dunia. Abu Abdullah Muhammad Ismail aliyekuwa mashuhuri kwa jina la Imam Bukhari ni miongoni mwa wanazuoni wakubwa wa hadithi wanaoaminiwa na Ahlusunna. Alisafiri sana kwa ajili ya kutafuta hadithi za Mtume (saw). Kitabu mashuhuri zaidi cha mwanazuoni huyo ni kile cha Jamius Swahih maarufu kama Sahihi Bukhari. Vitabu vingine mashuhuri vya mwanazuoni huyo ni: Al Adabul Mufrad, Tarikhul Ausat na As Sunan.

Tarehe Mosi Shawwal miaka 869 iliyopita Said Bin Mubarak maarufu kwa jina la Ibn Dahhan, mfasiri, mwanafasihi na malenga wa Kiislamu alifariki dunia. Alizaliwa mjini Baghdad na baada ya kumaliza masomo yake ya awali, alianza kusoma lugha sambamba na kupokea hadithi kutoka kwa wanazuoni wakubwa wa zama zake. Mtaalamu huyo mkubwa wa lugha alitilia maanani taaluma ya fasihi hususan katika kusoma mashairi na hivyo kuwa mfano wa kuigwa na wanafunzi wake katika usomaji mashairi.

Siku kama ya leo miaka 72 iliyopita sawa na tarehe 26 Juni 1945, mkutano wa kimataifa wa San Fransisco ulimaliza shughuli zake katika mji unaojulikana kwa jina hilo huko Marekani kwa kupasishwa hati ya Umoja wa Mataifa. Mkutano huo ambao ulikuwa wa kwanza wa kimataifa kuwahi kufanyika baada ya Vita vya Pili vya Dunia, ulihudhuriwa na wawakilishi wa nchi 50 waitifaki katika vita hivyo.

Siku kama ya leo miaka 57 iliyopita kisiwa cha Madagascar kilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mfaransa. Uingereza na Ufaransa zilianzisha ushindani wa kuidhibiti nchi hiyo ya Kiafrika katika karne ya 18. Mwishoni mwa karne ya 19 Ufaransa ilifanikiwa kukidhibiti kikamilifu kisiwa cha Madagascar. Hata hivyo wananchi wa Madagascar waliendesha mapambano mengi ya ukombozi dhidi ya wakoloni wa Kifaransa, miongoni mwake ni yale ya mwaka 1947 ambapo karibu watu elfu 80 waliuawa.

Miaka 832 iliyopita, sawa na tarehe Mosi Shawwal mwaka 606 Hijria, alifariki dunia Fakhruddin Razi, faqihi na msomi mkubwa wa Kiirani katika mji wa Herat akiwa na umri wa miaka 62. Razi alizaliwa mwaka 544 katika mji wa Rey ulioko kandokando mwa jiji la Tehran. Msomi huyo ameandika na kutarjumi vitabu vingi na miongoni mwa vitabu vyake ni tafsiri ya Qur'ani Tukufu ijulikanayo kwa jina la 'Tafsir Kabiir' na Nihayatul U'quul.

Miaka 181 iliyopita katika siku inayosadifiana na hii ya leo, aliaga dunia Rouget de Lisle, malenga na mtunzi wa nyimbo za kimapinduzi wa Ufaransa. Rouget alihudumu pia jeshini, na alikuwa akiimba mashairi ya kuwahamasisha wanamapinduzi wa Ufaransa na kutunga pia nyimbo za hamasa na kusisimua. Rouget de Lisle alitunga wimbo wa kimapinduzi kwa jina "La Marseillaise" ambao baadaye ulikuwa wimbo rasmi wa taifa.
