Jul 19, 2017 02:26 UTC
  • Jumatano, Julai 19, 2017

Leo ni Jumatano tarehe 24 Mfunguo Mosi Shawwal 1438 Hijria sawa na Julai 19, 2017 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 689 iliyopita alifariki dunia Ibnu Labban faqihi, mpokeaji hadithi, mfasiri wa Qur'ani na mwandishi wa Kiislamu. Alizaliwa mwaka 679 Hijria katika mji wa Damascus na kupitisha kipindi cha ujana wake katika mji huo. Ibnu Labban alipata elimu za fiqih, usul-fiqih na hadithi kutoka kwa walimu na maulamaa wakubwa wa zama hizo. Mbali na masomo hayo, Ibnu Labban alikuwa mahiri pia katika kutunga mashairi. Msomi huyo wa Kiislamu alijishughulisha vilevile na kufundisha, kutoa waadhi na kufasiri Qur'an Tukufu. Kitabu pekee kilichochapishwa cha mwanazuoni huyo ni tafsiri ya Qur'ani Tukufu.

Miaka 124 iliyopita katika siku kama hii ya leo alizaliwa malenga wa Russia kwa jina la Vladimir Mayakovsky. Mashairi ya Mayakovsky yalikuwa na nafasi kuu wakati wa mapinduzi ya Kikomonisti ya Urusi ya zamani mwaka 1917. Vladimir Mayakovsky alikuwa akiamini kuwa fasihi inapasa kuwa lugha ya watu wengi na inayobainisha maisha yao ya kijamii. 

Vladimir Mayakovsky

Miaka 63 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia msomi mashuhuri wa Kiislamu Muhammad Hussein Kashiful Ghitaa. Ayatullah Kashiful Ghitaa alizaliwa katika mji mtakatifu wa Najaf katika familia ya wasomi na wachamungu na kuanza kutafuta elimu akiwa bado kijana mdogo. Baada ya kukamilisha elimu ya msingi na ya kati, Ayatullah Kashiful Ghitaa alihudhuria darsa za maulamaa wakubwa wa zama hizo na kukwea daraja za juu za elimu katika kipindi kifupi. Alifanikiwa kulea wasomi na maulamaa wakubwa na kufanya safari katika nchi nyingi za Kiislamu kwa ajili ya kueneza elimu na maarifa. Mwanazuoni huyo mkubwa wa Kiislamu pia alikutambua kushiriki katika masuala ya kisiasa na kutilia maanani masuala ya serikali na utawala kuwa ni katika mambo ya wajibu na alikuwa na mchango mkubwa katika kuanzisha Harakati ya Kitaifa ya Iraq. Ayatullah Kashiful Ghitaa alishiriki vilivyo katika mapigano ya jihadi ya wananchi wa Iraq wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia dhidi ya jeshi vamizi la Uingereza. Mwanazuoni huyo wa Kiislamu ameandika vitabu vingi katika nyanja mbalimbali.

Muhammad Hussein Kashiful Ghitaa

Miaka 38 iliyopita katika siku kama ya leo mapinduzi ya wananchi wa Nicaragua yalipata ushindi dhidi ya dikteta Anastasio Somoza wa nchi hiyo na muitifaki wake mkubwa yaani Marekani. Dikteta huyo kibaraka wa Marekani alichukua hatamu za uongozi wa Nicaragua mwaka 1967 na tangu wakati huo wimbi kubwa la upinzani lilianza kuenea nchini kote na katika America ya Kati dhidi ya kiongozi huyo. Mapambano ya silaha ya wapiganaji wa msituni ya Harakati ya Ukombozi wa Kitaifa ya Sandinista (FSLN) yaliyoanza mwaka 1963 yalipamba moto zaidi katikati ya muongo wa 1970 na kuungwa mkono na wananchi. Hatimaye Somoza alilazimika kukimbia nchi baada ya jeshi la Sandinista kuingia Managua mji mkuu wa Nicaragua katika siku kama ya leo. Karibu watu elfu 40 waliuawa katika mapinduzi ya Nicaragua.

Mapinduzi ya watu wa Nocaragua

 

Tags