Sep 30, 2017 04:40 UTC
  • Jumamosi, Septemba 30, 2017

Leo ni Jumamosi tarehe 9 Mfunguo Nne Muharram 1439 Hijria mwafaka na tarehe 30 Septemba mwaka 2017 Miladia.

Siku kama ya leo inasadifiana na tarehe 9 Muharram mwaka 61 Hijria. Katika siku hii majeshi ya Yazid yalikuwa yamejiandaa kikamilifu kumshambulia Imam Hussein AS na masahaba zake katika ardhi ya Karbala, Imam alimtuma ndugu yake aliyesifika kwa ushujaa mkubwa yaani Abul Fadhl Abbas akawaombe maadui hao wampe fursa aupitishe usiku huo kwa Swala na kunong'ona na Mola wake. Usiku huo Imam Hussein aliwakusanya wafuasi wake na baada ya kumhimidi Mwenyezi Mungu na kumsalia Mtume, aliwaambia: ''Kila anayetaka, aitumie fursa iliyobakia ya giza la usiku kwa ajili ya kuyanusuru maisha yake, kwani hakuna atakayebaki hai hapo kesho tutakapokabiliana na jeshi la Yazid.'' Hata hivyo masahaba na wafuasi waaminifu na waumini wa kweli wa mtukufu huyo walikuwa wameshakata shauri kujitolea mhanga kwa ajili ya Mwenyezi Mungu hadi tone la mwisho la damu zao. Usiku huo wa kuamkia Ashura yaani tarehe 10 Muharram, uwanja wa Karbala ulikuwa medani ya ibada kwa mashujaa ambao licha ya kuwa wachache kwa idadi lakini walisimama imara kama mlima na hawakumuacha Imam na kiongozi wao hata kwa dakika moja.***

Siku ya Tasua

Siku kama ya leo kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, aliaga dunia Maulana Jalaluddin Balkhi maarufu kwa jina la Moulavi mmoja wa malenga na washairi mahiri wa Iran.  Moulavi alikuwa mshairi mkubwa na mwenye uwezo na kipaji kikubwa katika karne ya 7 Hijria. Alizaliwa mwaka 604 Hijria katika mji wa Balkhi kaskazini mwa Afghanistan ya leo. Miongoni mwa athari kubwa za Maulana au Jalaluddin Balkhi ni kitabu cha mashairi cha Masnavi Manavi.***

Maulana Jalaluddin Balkhi maarufu kwa jina la Moulavi 

Miaka 79 iliyopita katika siku kama ya leo, kulifayika mkutano wa kihistoria wa Munich nchini Ujerumani. Mkutano huo ulihudhuriwa na Adolph Hitler na Benito Mussolini viongozi wa Ujerumani na Italia na pia Neville Chamberlain na Edouard Daladier, Mawaziri Wakuu wa wakati huo wa Ufaransa na Uingereza. Mkutano wa Munich ulifanyika kwa shabaha ya kutafuta njia ya kumaliza hitilafu kati ya Ujerumani na Czechoslovakia. Mkutano huo ulimalizika kwa kufikiwa makubaliano ya kuiunganisha sehemu moja ya ardhi ya Czechoslovakia na Ujerumani.***

Viongozi walioshiriki katika mkutano wa kihistoria wa Munich nchini Ujerumani.

Miaka 51 iliyopita katika siku kama hii ya leo yaani tarehe 30 mwezi Septemba mwaka 1966, nchi ya Botswana ilijipatia uhuru kutoka kwa mkoloni Muingereza. Botswana ilianza kukoloniwa na Uingereza mwaka 1885 Miladia. Harakati za wananchi wa Botswana za kuikomboa nchi yao zilishtadi tangu mwaka 1920 na kupelekea kupatikana uhuru wa nchi hiyo mwaka 1966. Nchi ya Bostwana iko kusini mwa bara la Afrika ikipakana na Afrika Kusini, Zimbabwe na Namibia. ***

Botswana

Katika siku kama ya leo miaka 32 iliyopita, alifariki dunia mvumbuzi wa kipimo kinachotumiwa kupimia nguvu ya mitetemeko ya ardhi Charles Richter. Akishirikiana na mhakiki mwingine, Richter alipima mitetemeko hiyo kwa mujibu wa nishati inayotokana na mawimbi ya mitetemeko ya ardhi toka daraja moja hadi 9 na kusajili kipimo cha Rishta. Kabla ya hapo wataalamu walikuwa wakipima mitetemeko ya ardhi kwa mujibu wa athari ya nje ya kipimo ambacho hakikuwa cha kuaminika. ***

Charles Richter.

Na leo tarehe 30 Septemba ni Siku ya Kimataifa ya Viziwi. Lengo la siku hii kupewa jina la Siku ya Kimataifa ya Viziwi ni kutaka kuimarisha utamaduni wa kuwa na mawasiliano na watu wenye ulemavu huo, kustawisha maarifa ya lugha ya ishara na kuwazindua wanasiasa na watu wa kawaida kuhusu matatizo ya watu wa tabaka hilo.

Siku ya Kimataifa ya Viziwi

 

 

Tags