Mar 25, 2018 05:23 UTC
  • Jumapili, Machi 25, 2018

Leo ni Jumapili tarehe saba Rajab 1439 Hijiria inayosadifiana na tarehe 25 Machi mwaka 2013 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1134 iliyopita, alizaliwa Ibn Twarrar, msomi mkubwa wa hadithi na fasihi wa ulimwengu wa Kiislamuu. Abul-Fat'hi Muafi Ibn Zakaria Ibn Yahya, maarufu kwa jina la Ibn Twarrar, ni miongoni mwa walimu wakubwa na maulama wa madhehebu ya Shaafi ambaye pia alibobea katika elimu ya fiqhi, fasihi, hadithi, nahw na lugha. Msomi huyo wa Kiislamu, aliandika vitabu mbalimbali katika fani ya fiqhi. Miongoni mwa athari za Ibn Twarrar ni pamoja na kitabu cha 'al-Jalis wal-Anis'. Kitabu hicho kinajumuisha juzuu 100 ambazo baadhi yake zimezungumzia hadithi za Mtume Muhammad (saw) pamoja na hekaya mbalimbali. Ibn Twarrar alifariki dunia mjini Baghdad, Iraq mwaka 390 Hijiria akiwa na umri wa miaka 85.

Ibn Twarrar

Siku kama ya leo miaka 61 iliyopita, mkataba wa kuasisi Jumuiya ya Kiuchumi ya Ulaya au kwa jina jingine Soko la Pamoja la Ulaya ulisainiwa huko Roma mji mkuu wa Italia kati ya wawakilishi wa nchi mbalimbali za bara hilo. Jumuiya hiyo iliundwa kwa lengo la kuasisi umoja wa forodha kati ya nchi wanachama ili kufuta ushuru wa bidhaa na baada ya hapo, ubadilishanaji wa bidhaa, nguvu kazi, vitega uchumi na huduma nyinginezo pia ukawa huru kati ya nchi wanachama. Jumuiya hiyo ilikuwa utangulizi wa kuundwa Umoja wa Ulaya mwaka 1992.

Bendera za Umoja wa Ulaya

Siku kama ya leo miaka 43 iliyopita, Mfalme wa wakati huo wa Saudi Arabia, Faisal bin Abdulaziz, aliuawa na mwana wa ndugu yake mwenyewe, Faisal bin Saaid bin Abdulaziz. Faisal bin Saaid alifanya mauaji hayo akilalamikia kupunguzwa kwa mshahara wake. Japokuwa hitilafu katika kizazi cha wafalme wa Saudi Arabia zimekuwepo siku zote na zimekuwa zikipamba moto mara kwa mara lakini mauaji ya Mfalme Faisal yalikuwa ya kwanza ya mfalme wa nchi hiyo kutokana na hitilafu kama hizo. Muuaji wa Mfalme Faisal pia alikatwa kichwa mbele ya umati wa watu tarehe 18 Juni mwaka 1975. Baada ya Faisal, Khalid mwana mwingine wa Abdulaziz alishika kiti cha ufalme wa Saudi Arabia.

Faisal bin Saaid bin Abdulaziz

Siku kama ya leo miaka 23 iliyopita, vikosi vamizi vya Marekani ambavyo mwezi Disemba 1992 viliwasili nchini Somalia kwa kisingizio cha kukomesha uasi nchini humo, hatimaye vililazimika kuondoka katika nchi hiyo baada ya kushindwa vibaya na bila ya kutarajia. Mwaka 1991 makundi mbalimbali ya Somalia yalimpindua dikteta wa nchi hiyo Muhammad Siad Barre. Hata hivyo makundi hayo yalishindwa kufikia makubaliano ya kuunda serikali ya mseto na mkwamo huo wa kisiasa ukapelekea kuzuka vita vya ndani nchini humo. Marekani ilituma wanajeshi wake huko Somalia katika fremu ya kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa ili kulinda maslahi yake nchini humo, kutokana na nafasi muhimu ya Somalia katika eneo la Pembe ya Afrika. Askari wa Marekani walikabiliwa na mapambano makali ya Wasomali na kupoteza askari karibu 100.

Ramani ya Somalia