Hadithi ya Uongofu (121)
Assalaamu alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi cha Hadithi ya Uongofu, kipindi ambacho hujadili maudhui mbalimbali za kimaadili, kijamii na kadhalika na kukunukulieni hadithi kutoka kwa Bwana Mtume saw na Maimamu watoharifu (as) kuhusiana na maudhui hizo
Kipindi chetu kilichopita kilijadili na kuzungumzia suala la utani na mzaha. Tulibainisha faida za kufanya mzaha na utani na kueleza jinsi mzaha na utani unavyopaswa kuwa na mipaka. Aidha tulieleza umuhimu wa kutia furaha katika moyo wa muumini aliye na ghamu na majonzi. Kadhalika tulisema kwamba, Mtume saw anakitaja kitendo hicho kwamba, ni mithili ya kumfurahisha Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Mbora huyo wa viumbe amenukuliwa akisema: Kila atayemfurahisha muumini, amenifurahisha mimi, na mwenye kunifurahisha mimi amemfurahisha Mwenyezi Mungu. Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 121 ya mfululizo huu, kitazungumzia moja ya tabia nyingine mbaya nayo ni ya kujipendekeza au kujikomba. Ni matumaini yangu kuwa, mtakuwa pamoja name katika dakika hizi chache ili mtegee sikio kile nilichokuandalieni kwa leo. Karibuni.
Katika fasili na maana ya lugha, kujipendekeza ni kuwa na uhusiano wa kinafiki na mtu au kumpa sifa za uwongo au kumsaidia kazi kwa lengo la kupata upendeleo fulani ambapo kuna maana ya kujikomba pia. Kwa hakika kujikomba na kujipendekeza ni katika dhambi za ulimi. Mtu mwenye kujikomba si tu kwamba, huwa amekumbwa na tabia hii mbaya ya kimaadili bali hutumbukia katika tabia nyingine mbaya kama za kusema uongo, ria na kujionyesha na kujikweza ambazo zote hizi ni katika sifa na tabia mbaya za kimaadili. Baya zaidi ni kwamba, kumsifia mtu kwa sifa asizonazo kwa nia ya kujikomba na kujipendekeza, humzuia mtu mwenye tabia isiyofaa kujidiriki na kutambua aibu zake na hivyo kukosa fursa yenye thamani ya kujirekebisha. Imam Ali bin Abi Twalib as anaitambua tabia ya kujipendekeza kuwa miongoni mwa tabia chafu na mbaya za kimaadili na anawataka watu wasifanye urafiki na mtu mwenye tabia hii. Anasema: Usifanye urafiki na mtu mwenye tabia ya kujikomba na kujipendekeza, atakuhadaa na kukufanya ukumbwe na mghafala kwa kutumia ulimi wake wa kujipendekeza, jambo ambalo ni baya analionyesha na kulifanya kuwa zuri na hupenda wewe uwe kama yeye.
Kwa hakika kuwasifia kupita kiasi watu ambao hawana ustahiki na uwezo wa kusikia sifa wanazopatiwa ni kujipendekeza. Hapana shaka kuwa, kujikomba ni katika ishara za unafiki, nifaki na undumakuwili. Ukweli wa mambo ni kuwa, mtu mwenye kujipendekeza kwa wengine kwa ajili ya maslahi kama kupatiwa upendeleo au kujikweza daima si mwenye kusema na kubainisha haki na ukweli, bali anachokitanguliza yeye ni maslahi yake binafsi ambayo ndio ambayo humsukuma kuwasifia watu wengine. Na ndio maana kama itatokea kwamba, mazingira yakabadilika na akaona kuwa maslahi yake yapo hatarini kwa yule yule mtu aliyekuwa akimpamba na kumsifia kwa sifa kemkemu, basi hugeuka na kumuandama mtu yule kwa sifa mbaya na chafu.
Ni kutokana na ukweli huo ndio maana Imam Ali bin Abi Twalib as anaeleza kuwa moja ya vigezo vya urafiki wa kweli baina ya marafiki wawili ni kujiepusha na kujikomba na kujipendekeza. Kwa maana kwamba, rafiki wa kweli ni yule ambaye hajikombi na kujipendekleza kwa ajili ya maslahi yake.
Kwa hakika, tabia ya kujikomba na kujipendekeza hufuatiwa na kiburi kwa aliyesifiwa na kujiona kiasi kwamba, huwa kipofu na kutoona udhaifu na mapungufu yake au sifa hizo humlevya na kusahau nakisi na mapungufu aliyonayo. Mtu huyu baada ya kulewa sifa hizo, huhalalisha na kuyaona kuwa sahihi matendo mabaya na yasiyofaa.
Kwa msingi huo, nukta muhimu tunayojifunza ni hii kwamba, kujikomba na kujipendekeza mbali na kuzuia na kufunga mlango wa mabadiliko ya kimaadili na kitabia huwafanya watu wenye vifua vidogo vya kustahamili mambo kubadilika na kupata ujasiri wa kufanya mambo yasiyostahiki ambayo kimsingi yanakinzana na akili na sheria.
Kwa muktadha huo tunaweza kusema kuwa, mtu mwenye kujikomba na kujipendekeza ambaye amemsifia mtu fulani na kumfanya awe na ujasiri wa kufanya mambo mabaya na kushindwa kudiriki udhaifu na mapungufu hayo kutokana na kulewa sifa, ni mshirika wa dhambi, dhulma, kutokea ufisadi na uhalifu wa mtu huyo kwani amekuwa na nafasi katika kumshajiisha pasipo pa mahala pake. Ni kwa kuzingatia ukweli huo, ndio maana Bwana Mtume saw anasema: Wakati mwovu anaposifiwa arshi ya Mwenyezi Mungu hutetemeka na hilo humkasirisha Mwenyezi Mungu. Aidha amenukuliwa akisema: Usiwasifie watu wengine kwa sifa nzuri ambazo hawana kwa sababu tu ya kutaka kujipendekeza.
Hapana shaka kuwa, kila kitendo na sifa mbaya na isiyofaa ina matokeo yake. Kujipendekeza na kujikomba pia nako kuna athari mbaya na haribifu katika maisha ya mtu ambapo athari kuu ni kuhadaika. Tukirejea katika vitabu vya hadithi tunapata riwaya nyingi zinazoonyesha kuhadaika watu kutokana na kusifiwa na watu wengine.
Kwa mujibu wa hadithi hizo maneno ya mtu mwenye kujikomba na kujipendekeza huwa chimbuko la mtu kughafilika na kuhadaika. Wakati mtu anapojiona kuwa mbora kupitia uwongo wa wengine na kujihisi kimakosa kwamba, kwa upande wa elimu, amali na mtaji wa kimaada na kimaanawi ni mbora kuliko wengine kwa hakika huwa ameingia katika hatua hatari mno.
Ndio maana Imam Ali bin Abi Twalib as anazungumzia suala hilo akiashiria umuhimu wa kulindwa mipaka ya Mwenyezi Mungu na kutotoka katika hali ya uwiano na kati na kati na kusema: Msizungumze na mimi kama mnavyozungumza na wafalme waovu, msijitenge na kuwa mbali na mimi kama mnavyofanya kwa watu wenye hasira na msiamiliane nami kidhahiri.
Viongozi wa dini walikuwa wakiwachukia watu wote wenye kujikomba na kujipendekeza. Hali hii ya chuki ilikuwa kubwa kiasi kwamba, Mtume saw anasema: Wamwagieni udongo wa uso wenye kujipendekeza na kuwasifia watu wengine (kwa sifa wasizonazo).
Wapenzi wasikilizaji hadithi zote tulizotangulia kukunukulieni na ambazo zinakataza na kuwataka watu wajitenge mbali na sifa na tabia mbaya ya kujikomba na kujipendekeza lengo lake ni kuzuia kuenea tabia hii mbaya ya kimaadili katika jamii.
Nukta nyingine ya kuashiria ni kwamba, mtu anayesifiwa pia anapaswa kuwa makini na kutoruhusu hilo kwani kufanya hivyo hatua kwa hatua humfanya aghafilike na kulewa sifa kiasi cha kuona kwamba yote anayosifiwa ni sifa alizonazo. Matokeo yake ni kutoweza kudiriki mapungufu yake. Imam Ali bin Abi Twalib as na ambaye aliondokea kufahamika kwa sifa zote njema za ukamilifu wa mwanadamu katu hakuwa akiruhusu mtu amsifie mbele yake. Na ikitokea mtu amefanya hivyo basi alikuwa akisema: Ewe Mola wangu! Wewe wananijua zaidi kuliko ninavyojijua na mimi ninajijua zaidi kuliko wanavyonijua wao, Ewe Mola wangu! Usiniadhibu kwa kile alichokisema kunihusu mimi ambacho sina, na unifanye mbora kuliko wanavyonidhania.
Wapenzi waskilizaji muda wa kipindi chetu kwa leo umefikia tamati hivyuo sina budi kukomea hapa kwa leo.
Ninakushukuruni kwa kunitegea sikio na kwaherini…