Sep 09, 2018 11:32 UTC
  • Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu (67)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi la Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu. Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipitia hivi sasa umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya 67.

Kwa wale wasikilizaji wetu mnaofuatilia kwa karibu kipindi hiki bila shaka mngali mnakumbuka kuwa katika vipindi kadhaa vilivyopita tumezungumzia na kuchambua mabadiliko ya kisiasa na kimapinduzi yanayojulikana kama Mwamko wa Kiislamu nchini Yemen na uvamizi na mashambulio ya kijeshi ya Saudi Arabia na waungaji mkono wale dhidi ya nchi hiyo kwa lengo la kuiangusha serikali ya kimapinduzi ya harakati ya Ansarullah yenye uungaji mkono wa wananchi. Aidha tukaeleza kwamba hatua hiyo ya Saudia, mbali na kukiuka sheria za kimataifa imeshadidisha pia mivutano, mpasuko na hali ya utengano katika Ulimwengu wa Kiislamu. Kipindi chetu cha leo kitatupia jicho matukio ya Bahrain na kufanya uchambuzi kuona vipi mgogoro wa nchi hiyo pia umechangia kuleta umoja na mshikamano au utengano na mfarakano katika Ulimwengu wa Kiislamu.

Bahrain ni nchi ndogo zaidi iliyoko kwenye eneo la Ghuba ya Uajemi, inayoundwa na mjumuiko wa visiwa 33. Mji mkuu wa nchi hiyo ni Manama. Japokuwa lugha rasmi ya nchi hiyo ni Kiarabu, lakini lugha za Kifarsi, Kiurdu na Kiingereza zina watumiaji wengi pia nchini humo. Tangu zama za utawala wa Wasasani, yaani zaidi ya miaka 2000 iliyopita, Bahrain ilikuwa sehemu ya ardhi ya Iran, lakini kuna kipindi cha kuanzia mwaka 1522 hadi 1602 nchi hiyo ilikuwa chini ya utawala wa Wareno. Mnamo mwaka 1602, na baada ya Wareno kutimuliwa katika Ghuba ya Uajemi, Bahrain ilirejea tena kuwa sehemu ya ardhi ya Iran na mamlaka ya Iran katika kisiwa hicho yakaendelea hadi mwaka 1971 ambapo kwa upatanishi wa Umoja wa Mataifa na kwa ridhaa ya serikali ya Iran, Bahrain, ambayo hadi wakati huo ilikuwa mkoa wa 14 wa Iran, iligeuka kuwa nchi nyingine huru katika eneo la Ghuba ya Uajemi inayojitawala yenyewe. Bahrain ina ukubwa wa eneo la kilomitamraba 706 na idadi ya watu wapatao milioni moja, ambao asilimia 70 kati yao ni Waislamu wa madhehebu ya Shia na asilimia 30 iliyosalia inaundwa na Waislamu wa Kisuni, Wakristo, Wayahudi na wafuasi wa dini nyinginezo. Mfalme wa Bahrain ni Sheikh Hamad bin Issa Aal Khalifa, ambaye ndiye anayeitawala nchi hiyo tangu mwaka 1999 hadi hivi sasa. Kuna vyama karibu 15 vya siasa vinavyoendesha harakati zao nchini Bahrain vikiwemo vya kidini, vya kiliberali, vya mrengo wa kushoto na vile vya Kibaathi.

Mashia wa Bahrain wamegawika makundi mawili: Mashia Waarabu na wasio Waarabu. Asilimia isiyopungua 20 ya Wabahraini ni watu wenye asili ya Iran na watu wasio Waarabu, ambao ni wakazi wa Bahrain kabla ya uhuru wa nchi hiyo. Kuhusu kuhajiri kwa Wairani kuelekea Bahrain si rahisi kubainisha ni lini hasa watu hao walihamia nchini humo kwa sababu kumbukumbu zinaonyesha kuwa Wairani wamekuwepo nchini Bahrain katika kipindi chote cha historia. Kinyume na nchi mbili za Kuwait na Umoja wa Falme za Kiarabu, yaani Imarati, ambapo Wairani wengi wanaoishi huko walihajiri kuelekea nchi hizo katika kipindi maalumu cha kabla na baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1979 hapa nchini Iran, kwa upande wa Bahrain, Wairani wamekuwa siku zote ni sehemu ya wakazi wa asili wa ardhi ya nchi hiyo. Licha ya kupita miaka na miaka, lugha ya Kifarsi, utamaduni na mila na desturi za Wairani wa Bahrain zimeendelea kubaki kuwa za Kiirani. Kifarsi ndiyo lugha ya asili na lugha wanayozungumza watu hao majumbani mwao; na lugha ya Kiarabu inahesabiwa kuwa lugha ya pili ya watu hao. Jamii nyengine ya Wabahraini ni ya Mashia Waarabu ambao wamekuwa na uhusiano mkubwa na wa tangu na tangu na Iran. Asili ya uhusiano huo inarejea kwenye kipindi cha karibu 500 nyuma, yaani wakati wa enzi za utawala wa Wasafawiyyah nchini Iran ambapo wakati huo Ushia ulifanywa kuwa madhehebu rasmi ya Kiislamu nchini Iran. Kuanzia kipindi hicho na kuendelea, Mashia na maulamaa wa Kishia kutoka Bahrain walikuwa ndio kiungo cha mawasiliano baina ya Iran na Ulimwengu wa Waarabu, wakawa wanafanya safari za kuja Iran kwa ajili ya kufanya tablighi ya kutangaza madhehebu ya Shia.

 

Muundo wa idadi ya watu nchini Bahrain ni ya mchanganyiko; lakini kwa upande wa kidini akthari ya Wabahraini ni Waislamu wa madhehebu ya Shia, wakati mfumo wa utawala wa nchi hiyo uko mikononi mwa wasio Mashia. Katika muundo wa kisiasa Masuni walio wachache wa ukoo wa Aal Khalifa ndio walioshika hatamu za utawala wa nchi, huku Mashia wakishirikishwa kwenye sehemu chache tu za muundo wa madaraka.  Utawala wa kifalme wa Aal Khalifa ni tegemezi mno kwa Saudi Arabia na unahisi ni hatari na tishio kwake ikiwa Mashia watashika hatamu za madaraka nchini Bahrain. Kwa sababu hiyo, ili kubadilisha demografia na muundo wa idadi ya watu, katika kipindi cha miaka kadhaa sasa serikali ya Bahrain imekuwa ikitekeleza sera mpya ya kuwaandalia mazingira watu na raia wa kigeni wasio wazalendo wa Bahrain kutoka nchi za Jordan, Palestina, Lebanon, Saudi Arabia na Misri kuhamia nchini humo ili kubadilisha muundo wa idadi ya watu kwa madhara ya Waislamu wa Kishia. Lakini pamoja na kutekelezwa sera hiyo Mashia wangali wanaunda idadi kubwa ya raia wa Bahrain. Hatua hiyo ya utawala wa Aal Khalifa, sambamba na kuwanyima wananchi hao haki na uhuru wao wa kiraia uliobainishwa wazi ndani ya katiba zimezusha malalamiko na upinzani mkubwa wa Mashia. Manung’uniko na upinzani huo na kutotekeleza utawala wa Aal Khalifa ahadi zake za kuleta mageuzi vimekuwaa kila mara vikisababisha mivutano na mikwaruzano ndani ya jamii ya Bahrain, lakini kuanza wimbi la mwamko mwanzoni mwa muongo wa mwanzo wa karne hii ya 21 tunaweza kukutaja kama nukta muhimu zaidi katika historia ya Bahrain.

Vuguvugu la Mwamko wa Kiislamu nchini Bahrain lilianza rasmi tarehe 14 Februari mwaka 2011 kutokana na kuathiriwa na matukio na mabadiliko yaliyojiri katika nchi nyingine za Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika ikiwemo Tunisia, Misri, Libya na Yemen. Tangu wakati huo hadi sasa, nchi hiyo inashuhudia maandamano ya wananchi ya kupinga utawala wa Aal Khalifa. Katika muda wote wa vuguvugu hilo la mapinduzi ya wananchi, utawala wa Aal Khalifa umekuwa ukitumia njia za kikatili na za ukandamizaji kukabiliana na wapinzani wanaoandamana kwa amani. Lakini mbali na ukandamizaji wa raia unaofanywa na utawala wa Aal Khalifa, mnamo mwezi Machi mwaka 2011, wanajeshi vamizi wa Saudi Arabia waliopata baraka kamili za Aal Khalifa na serikali ya Marekani, na kwa kutumia mwavuli wa vikosi vya Ngao ya Kisiwa, waliingia nchini Bahrain na kuendeleza kazi iliyoanzishwa na askari wa utawala wa Aal Khalifa ya kuwakandamiza wananchi wa Bahrain.

 Wapenzi wasikilizaji, kutokana na kumalizika muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki sina budi kuishia hapa nikitumai kuwa mumenufaika na yale mliyoyasikia katika kipindi chetu cha leo. Basi hadi tutakapokutana tena wiki ijayo inshaallah, katika siku na saa kama ya leo katika sehemu ya 68 ya mfululizo huu nakuageni, huku nikikutakieni usikilizaji mwema wa sehemu iliyosalia ya matangazo yetu.

Tags