Sep 27, 2018 02:47 UTC
  • Alkhamisi, 27 Septemba,  2018

Leo ni Alkhamisi tarehe 17 Muharram 1440 Hijria sawa na Septemba 27, mwaka 2018.

Leo tarehe 27 Septemba ni Siku ya Kimataifa ya Utalii Duniani. Utalii ni moja ya sekta muhimu za mabadilishano ya kiutamaduni baina ya watu wa mataifa mbalimbali. Aidha utalii unaweza kutimia kupitia safari na utalii wa ndani na nje ya nchi kwa madhumuni tofauti. Licha ya kwamba utalii umekuwa na historia ya muda mrefu katika maisha ya mwanadamu, lakini utalii wa mfumo wa kisasa ulianza mwanzoni mwa karne ya 16 Miladia, wakati yaliposhika kasi mapinduzi ya kiviwanda barani Ulaya na kuvumbuliwa aina mpya ya maisha barani humo. Ni kuanzia karne ya 17 ndipo istilahi ya utalii ikaenea zaidi hasa katika jamii ya watu wa Ufaransa.

Siku kama leo miaka 22 iliyopita, kundi la Taliban lilivamia na kutwaa mji mkuu wa Afghanistan, Kabul. Kundi la Taleban liliasisiwa mnamo mwaka 1994 na likateka hatua kwa hatua maeneo ya kusini na magharibi mwa Afghanistan kwa himaya ya Marekani, misaada ya kisiasa na kijeshi ya Pakistan pamoja na misaada ya kifedha ya Saudi Arabia. Jeshi la serikali ya Afghanistan lililokuwa likiongozwa na Ahmad Shah Mas'ud liliondoka mjini Kabul siku moja kabla ya Taliban kuuteka mji huo. Baada ya kuingia Kabul, kundi la Taliban lilianza kutekeleza sheria kali na zinazoshabihiana na zile za karne za kati dhidi ya wananchi.

Taliban

Siku kama ya leo miaka 34 iliyopita alifariki dunia Ayatullah Sayyid Abdullah Shirazi, mwasisi wa hauza ya kidini mjini Mash'had nchini Iran. Sayyid Abdullah Shirazi alizaliwa mjini Shirazi mwaka 1309 Hijiria na kuelekea mjini Najaf kwa ajili ya kuendelea na masomo ya juu ambapo alipata kusoma kwa Ayatullah Agha Dhiyaaud-Din Iraqi na wasomi wengine wa zama hizo. Baada ya kusalia kwa miaka 13 mjini Najaf na kufikia daraja ya ijtihadi alirejea mjini Shirazi na kuasisi hauza ya kidini sanjari na kuanzisha mapambano dhidi ya utawala wa Kipahlavi nchini hapa.

Ayatullah Sayyid Abdullah Shirazi

Siku kama ya leo miaka 37 iliyopita wapiganaji shujaa wa Iran walifanikiwa kuvunja mzingiro wa mji wa Abadan katika operesheni ya haraka na iliyokuwa imeratibiwa vyema dhidi ya ngome za jeshi la Saddam Hussein wa Iraq. Operesheni hiyo ilitekelezwa na wapiganaji wa Iran kufuatia agizo la kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Imam Khomeini, Mwenyezi Mungu Amrehemu. Mji wa Abadan ulikuwa umezingirwa na wanajeshi wa Iraq kwa karibu mwaka mmoja tangu kuanza vita vya kulazimishwa vya utawala wa dikteta Saddam dhidi ya Iran.

Askari wa Iran baada ya kuvunja mzingiro wa Abadan.

Siku kama ya leo miaka 69 iliyopita, mji wenye jamii kubwa ya watu Beijing ulichaguliwa rasmi kuwa mji mkuu wa Uchina. Mji wa kihistoria wa Beijing unapatikana mashariki kwa nchi hiyo na unahesabiwa kuwa moja ya vituo vikubwa vya kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni nchini China. Beijing ilichaguliwa kuwa mji mkuu wa China baada ya Mao Tse-tung kuchukua madaraka ya nchi na kiongozi wa wakati huo wa China Chiang Kai-shek kulazimika kukimbilia Taiwan.

Nembo ya mji wa Beijing