Nov 03, 2018 10:36 UTC
  • Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu (69)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi la Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu. Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipitia hivi sasa umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya 69.

Kwa wale wasikilizaji wetu wanaofuatilia kwa karibu kipindi hiki bila shaka mnakumbuka kuwa katika vipindi kadhaa vilivyopita tumezungumzia matukio na mabadiliko ya kisiasa na kimapinduzi yanayojulikana kama Mwamko wa Kiislamu yaliyojiri katika nchi za Yemen na Bahrain na tukaeleza kwamba Saudi Arabia imesababisha mpasuko na mfarakano katika Ulimwengu wa Kiislamu kwa hatua yake ya kuishambulia kijeshi Yemen kwa madhumuni ya kuiangusha serikali inayoungwa mkono na wananchi wa nchi hiyo na kwa kuyakandamiza maandamano ya amani ya kupinga utawala wa Aal Khalifa nchini Bahrain. Lakini badala ya utawala wa Aal Saud kuwajibika mbele ya fikra za waliowengi katika Ulimwengu wa Kiislamu, umekuwa kila mara ukizituhumu nchi nyingine kuwa zinaingilia masuala yake ya ndani na kuunga mkono wapinzani wake. Tukabainisha pia kwamba hatua za waziwazi za uingiliaji wa Saudia katika masuala ya ndani ya Yemen na Bahrain, ukiwemo uvamizi wake wa kijeshi, mbali na kukiuka dhahiri shahiri sheria za kimataifa umechangia sana pia kushadidisha mivutano na utengano katika Ulimwengu wa Kiislamu. Katika kipindi chetu cha leo tutachambua misimamo iliyochukuliwa na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) katika kikao cha mwisho cha viongozi wa nchi wanachama wa jumuiya hiyo kilichofanyika mjini Istanbul, Uturuki na nafasi ya Saudia katika kusababisha na kushadidisha utengano na mfarakano katika Ulimwengu wa Kiislamu.

Lakini kabla ya kuingia kwenye maudhui ya azimio lililopitishwa mwishoni mwa kikao cha 13 cha wakuu wa nchi wanachama wa OIC kilichofanyika mwezi Aprili mwaka 2016 mjini Istanbul Uturuki, ambapo kwa mashinikizo ya Saudi Arabia, kikao hicho kilitoa taarifa ya kuchochea mfarakano na iliyo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikiwa ni moja ya nchi wanachama wa jumuiya hiyo, inafaa tuyafanyie upembuzi kwanza mazingira ya kisiasa yaliyochochea kuibuka makabiliano kati ya Iran na Saudia katika kipindi cha karibu miaka mitatu nyuma ili tuweze kubaini malengo na makusudio ya utawala wa Riyadh ya kushinikiza kupitishwa azimio hilo dhidi ya Tehran.

Mwito wa Umoja

 

Baada ya kupinduliwa serikali ya Yemen na vikosi vya kimapinduzi na kushikwa hatamu za utawala na harakati ya Ansarullah, Saudi Arabia iliamua kukabiliana na nchi hiyo kwa kuivamia kijeshi; lakini kinyume na walivyodhani na walivyotabiri viongozi wa Saudia na wachambuzi wa masuala ya kisiasa na kijeshi wa eneo la Mashariki ya Kati, licha ya hatua hiyo kusababisha maafa makubwa ya kibindamu, mbali na kuteketeza maeneo mengi ya nchi hiyo, lakini hujuma na jinai zote hizo hazijawezesha Saudia kushinda vita hivyo na kuisambaratisha harakati ya Ansarullah. Katika wakati uleule vilipoanzishwa vita vamizi vya Saudi Arabia dhidi ya Yemen, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Khamenei alisisitiza msimamo wa Iran wa kutoingilia kwa namna yoyote katika masuala ya ndani ya Yemen na kutanabahisha pia kwamba ni jambo lisilowezekana kwa Saudia kushinda vita hivyo.

Kuendelea muqawama na kusimama imara wananchi na serikali ya Yemen kuliwahamakisha watawala wa Saudi Arabia; hivyo ili kufifisha fedheha na aibu waliyopata, watawala wa Riyadh wamekuwa kila mara wakiiandama Iran kwa vita vya kipropaganda na kisaikolojia.

Fedheha iliyofuatia iliyopata Saudia ilitokea katika msimu wa Hija wa mwaka 2015. Katika msimu huo wa Hija maelfu ya mahujaji kutoka nchi mbalimbali za Kiislamu walifariki dunia katika Masjidul-Haram, yaani msikiti mtukufu wa Makka na baadaye katika eneo la Mina kutokana na uzembe na usimamizi mbovu wa maafisa wa Saudia. Tukio hilo lililojulikana kama maafa makubwa zaidi ya Hija lilisababisha kupotea roho za mahujaji kutoka nchi 42 duniani. Afghanistan, Algeria, Bangladesh, Benin, Burkina Faso, Cameroon, Chad, China, Djibouti, Ethiopita, Gambia, Ghana, India, Indonesia, Iran, Iraq, Ivory Coast, Jordan, Kenya, Libya, Malaysia, Mali, Mauritius, Misri, Morocco, Myanmar, Niger, Nigeria, Oman, Pakistan, Senegal, Sri Lanka, Sudan, Tanzania, Tunisia, Ufilipino, Uganda, Uholanzi na Uturuki ni nchi ambazo mahujaji wao ama walifariki au kujeruhiwa katika maafa hayo.

 

Sababu ya kutokea maafa ya Mina ni moja ya mambo ambayo yamezusha mzozo na utesi kati ya Saudia na nchi zilizopata hasara kubwa zaidi ya roho za watu katika matukio hayo; na hadi sasa baada ya kupita zaidi ya miaka mitatu tangu yalipotokea maafa hasa ya Mina chanzo halisi cha matukio hayo bado hakijabainishwa na taasisi husika za nchi hiyo. Namna ya ufikishaji misaada kwa majeruhi na sababu ya kuchukua muda mrefu kabla ya kuanza kwake, ni masuali mengine yaliyoulizwa pia ambayo hayakupatiwa majibu ya maana. Lakini hata utaratibu wa kuhamisha na kutambua maiti za mahujaji waliouawa ni maudhui nyingine iliyozusha mjadala kati ya Saudi Arabia na nchi zilizotuma mahujaji katika msimu wa Hija wa mwaka 2015.

Mahujaji kutoka Iran waliofariki dunia katika maafa hayo walikuwa 464, ikiwa ni idadi kubwa zaidi kuliko nchi nyingine zote; na ndiyo maana Iran ilitoa wito mara kadhaa wa kuundwa tume ya kutafuta ukweli, lakini utawala wa Riyadh katu hauukujali wito huo bali ukafika mbali zaidi kwa kuwazuia mahujaji wa Kiirani wasishiriki kwenye ibada ya Hija ya mwaka uliofuatia wa 2016. Lakini haukuwa umepita muda mrefu tangu yalipotokea maafa ya Mina, utawala wa Saudia ukadhihirisha na kuonyesha upeo mpana zaidi wa chuki na uhasama wake kwa Waislamu  hususan wa madhehebu ya Shia ulipochukua hatua ya kumnyonga kiongozi wa Mashia wa nchi hiyo. Ilikuwa imepita miezi mitatu tu tangu yalipotokea maafa ya Mina, Wizara ya Mambo ya Nje ya Saudi Arabia ikatoa taarifa ya kutekelezwa hukumu ya kunyongwa Sheikh Nimr Baqir An-Nimr, alimu na kiongozi wa Waislamu wa Kishia wa nchi hiyo. Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Saudia, kanali ya televisheni ya Al-Arabiyyah ilitangaza kwamba hukumu ya kunyongwa Sheikh Nimr pamoja na washtakiwa wengine 46 ambao aghalabu yao walidaiwa kuwa eti ni magaidi ilitekelezwa katika maeneo 12 ya nchi hiyo. Sheikh Nimr Baqir An-Nimr alizaliwa mwaka 1379 Hijria katika eneo la Al-‘Awamiyyah mashariki mwa Saudi Arabia. Mujtahidi huyo wa madhehebu ya Shia na mwanaharakati wa kutetea haki za binadamu nchini Saudi Arabia alitiwa nguvuni mwaka 2012 katika maandamano ya upinzani yaliyofanywa na Waislamu wa Kishia nchini humo.

Wapenzi wasikilizaji, kutokana na kumalizika muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki sina budi kuishia hapa nikitumai kuwa mumenufaika na yale mliyoyasikia katika kipindi chetu cha leo. Basi hadi tutakapokutana tena wiki ijayo inshaallah, katika siku na saa kama ya leo katika sehemu ya 70 ya mfululizo huu, nakuageni, huku nikikutakieni usikilizaji mwema wa sehemu iliyosalia ya matangazo yetu…/

Tags