Nov 03, 2018 10:41 UTC
  • Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu (70)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi la Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu. Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipitia hivi sasa umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya 70.

Mazungumzo yetu katika kipindi kilichopita yaliishia pale tulipoeleza kwamba ilikuwa imepita miezi mitatu tu tangu yalipotokea maafa ya Mina katika ibada ya Hija ya mwaka 2015, pale Wizara ya Mambo ya Nje ya Saudi Arabia ilipotoa taarifa ya kutekelezwa hukumu ya kunyongwa Sheikh Nimr Baqir An-Nimr, alimu na kiongozi wa Waislamu wa Kishia wa nchi hiyo. Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Saudia, kanali ya televisheni ya Al-Arabiyyah ilitangaza kwamba hukumu ya kunyongwa Sheikh Nimr pamoja na washtakiwa wengine 46 ambao aghalabu yao walidaiwa kuwa eti ni magaidi ilitekelezwa katika maeneo 12 ya nchi hiyo. Sheikh Nimr Baqir An-Nimr alizaliwa mwaka 1379 Hijria katika eneo la Al-‘Awamiyyah mashariki mwa Saudi Arabia. Mujtahidi huyo wa madhehebu ya Shia na mwanaharakati wa kutetea haki za binadamu nchini Saudi Arabia alitiwa nguvuni mwaka 2012 katika maandamano ya upinzani yaliyofanywa na Waislamu wa Kishia nchini humo.

Kongamano la Umoja wa Kiislamu mjini Tehran, Iran

Mahakama ya makosa ya jinai ya Saudi Arabia ilimhukumu Sheikh Nimr Baqir An-Nimr adhabu ya kifo ya kukatwa kichwa kwa upanga na kusulubiwa mbele ya hadhara ya watu kwa tuhuma eti za kuwa muhaarib, yaani mzusha vita vya uadui na mfanya vitendo vinavyohatarisha usalama wa taifa. Utekelezaji huo wa kishenzi na kinyama wa adhabu ya kifo wa zama za Enzi za Kati, kwa kimombo Middle Ages, ulifanyika katika hali ambayo mashirika mbalimbali ya kutetea haki za binadamu yalikuwa yamesha toa miito kadhaa ya kuutaka utawala wa Saudia usitekeleze hukumu hiyo dhidi ya Sheikh Nimr. Kutekelezwa hukumu hiyo ya kinyama ya adhabu ya kifo kulitoa mguso mkubwa katika nchi mbalimbali, na kwa sababu hiyo utawala wa Saudi Arabia ulikabiliwa na mashinikizo ya fikra za waliowengi na kutengwa duniani. Nchini Iran pia wananchi walibainisha hasira zao kwa kutekelezwa hukumu ya adhabu ya kifo dhidi ya Sheikh Nimr Baqir An-Nimr na wimbi la malalamiko likawaandama watawala wa Aal Saud. Malalamiko na manung'uniko ya wananchi wa Iran ya kulaani utekelezwaji wa hukumu hiyo yalikuwa makubwa kufika hadi ya baadhi ya walalamikaji kukusanyika mbele ya ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Mashhad na ubalozi wa nchi hiyo hapa mjini Tehran. Hatua hiyo ya walalamikaji ilidhibitiwa na vikosi vya askari polisi; na serikali ya Iran ikazuia kuchukuliwa hatua yoyote ya kusababisha madhara kwa wanadiplomasia wa nchi hiyo. Hata hivyo serikali ya Saudi Arabia, ambayo ilikuwa ikitafuta kisingizio cha kujivua na mashinikizo ya fikra za waliowengi duniani ilichukua msimamo mkali kuhusiana na kadhia hiyo kwa kuamua kuvunja uhusiano wake wa kidiplomasia na kisiasa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Katika juhudi za kujivua na hali ya kutengwa na kufifisha jinai inazotenda dhidi ya dini na dhidi ya binadamu, Saudi Arabia haikutosheka na kuvunja uhusiano wake wa kisiasa na Iran, lakini ilikwenda mbali zaidi na kutumia mbinu ya kurubuni na ya kutoa vitisho dhidi ya nchi nyingine za Kiislamu, ili kuuhamasisha Ulimwengu wa Kiislamu usimame dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kupitia kikao cha kumi na tatu cha viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) kilichofanyika mwezi Aprili mwaka 2016 mjini Istanbul, Uturuki. Katika kikao hicho, nchi ambazo zenyewe zinalihami na kuliunga mkono kundi la kitakfiri la Desh na magaidi wengine katika eneo, zilieneza sumu dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa lengo la kuibana isiendeleze sera zake za kuwaunga mkono watu wanaodhulumiwa, wa Palestina, Yemen na Bahrain. Katika taarifa ya kikao hicho cha 13 cha viongozi wa OIC, Saudia ilishinikiza kuongezwa kipengele cha kulaani matukio yaliyojiri katika ubalozi wake wa mjini Tehran na ubalozi wake mdogo wa mjini Mashhad. Lakini mbali na hilo, kulingana na matakwa ya viongozi wa Saudi Arabia, misimamo ya Iran kuhusiana na adhabu za vifo zilizotekelezwa nchini Saudia ilikosolewa vikali, na raia wa nchi hiyo walionyongwa kinyama, akiwemo kiongozi wa Waislamu wa Kishia Sheikh Nimr Baqir An-Nimr, walitajwa kuwa eti ni "magaidi".

 

Ijapokuwa taarifa hiyo ya kikao cha viongozi wa nchi wanachama wa OIC kilichofanyika mjini Istanbul ilipitishwa kutokana na mashinikizo ya Saudi Arabia lakini nchi nyingi za Kiislamu zilikuwa na uelewa kwamba madai ya nchi hiyo hayakuwa na ukweli, na tuhuma zake dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zilikuwa hewa na bandia; na hata baadhi ya nchi kama Lebanon na Iraq hazikuunga mkono misimamo hiyo ya utawala wa Riyadh. Hata hivyo kutolewa kwa taarifa hiyo kulionyesha wazi kwamba kwa kutumia wenzo wa vitisho na kurubuni, ikiwemo kutishia kukata misaada yao ya fedha kwa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League), Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi (P)GCC na jumuiya yenyewe ya ushirikiano wa Kiislamu, watawala wa Aal Saud walizilazimisha nchi wanachama wa jumuiya hizo zifuate siasa haribifu na za kihasama za nchi hiyo katika Ulimwengu wa Kiislamu hususan hatua zake za kiuadui dhidi ya Muqawama; na kudhihirisha pia kwamba Riyadh haisiti hata kufanya vyovyote vile iwezavyo ili kutoa pigo kwa Iran. Na hii ni katika hali ambayo, kuwa kitu kimoja nchi mbili za Iran na Saudi Arabia kunaufanya Ulimwengu wa Kiislamu uwe na nguvu na uwezo mkubwa mno katika uga wa kimataifa. La kusikitisha zaidi ni kwamba ili kuficha jinai za ukiukaji haki za binadamu unaofanyika nchini Saudia na kubadilisha mkondo wa lawama za fikra za waliowengi duniani kutoka upande wa Riyadh na kuuelekeza Tehran, watawala wa Aal Saud wamekuwa tayari kumkumbatia hata adui mkuu wa Waislamu, yaani Israel na kimsingi wanachofanya ni kufanikisha malengo ya kujipanua ya utawala huo haramu wa Kizayuni.

Wapenzi wasikilizaji inatupasa tukiri kwamba leo hii suala la umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu liko katika hali isiyoridhisha na ya kusikitisha mno, kwani baadhi ya nchi, badala ya kusaidia kutatua tatizo hilo zimeamua kuongezea uzito kwenye uzani wa adui; na ndiyo maana kila siku tunaendelea kushuhudia mifarakano katika Ulimwengu wa Kiislamu. Kutolewa taarifa ya Istanbul kulizima mwanga wa mwisho wa matumaini yaliyokuwemo ndani ya nyoyo za Waislamu ya kuletwa umoja na jumuiya hiyo. Pamoja na hayo tungali tuna matumaini ya kuja kushuhudia katika siku za usoni kuboreka hali ya umoja baina ya nchi za Kiislamu. Kutokana na kumalizika muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki, sina budi kukomea hapa kwa leo nikitumai kuwa mtakuja kujiunga nami tena wiki ijayo inshallah katika mfululizo mwengine wa kipindi hiki. Basi hadi wakati huo nakuageni, huku nikikutakieni kila la heri maishani.../

 

Tags