Sayansi na Teknolojia (26)
Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika makala hii ambayo huangazia baadhi ya matukio muhimu ya kuhusu sayansi na teknolojia nchini Iran na maeneo mengine duniani.
Wakati idadi ya watu wanaotumia intaneti ikiongezeka duniani watu walio na ujuzi wa teknolojia, habari na mawasiliano yaani TEHAMA wanahitajika ili kuweza kuunganisha watu popote pale walipo. Hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya muungano wa kimataifa wa mawasiliano,ITU.
Ripoti hiyo yaenye anwani, “Kupima mawasiliano katika jamii 2018” inaonesha kuwa gharama ya TEHAMA imepungua kimataifa katika kipindi cha muongo mmoja. Huku sera na usimamizi wa TEHAMA vikitajwa kama vichochezi vya kutengeneza mazingira ya kupunguza bei na kuhakikisha kwamba faida za TEHAMA zinafikia wateja.
“Mwaka huu ripoti inaonesha jinsi kuwekeza katika teknolojia ya Broadband kunaleta mabadiliko ya kidijitali kimataifa na kuwezesha watu kufikia huduma mbalimbali kwa njia rahisi", amesema Mkurugenzi Mkuu wa ITU, Houlin Zhao wakati wa kufungwa kwa kongamano la Muungano wa Kimataifa wa mawasiliano ambalo limefanyika hivi karibuni mjini Dubai.
Kwa sasa, ripoti inaonesha kuwa kuna ongezeko la upatikanaji wa huduma na matumizi ya TEHAMA. Na kubwa zaidi takriban nusu ya watu duniani kote wanatumia TEHAMA ikiwa ni asilimia 51.2 ya watu duniani ifikapo mwisho huu wa 2018.

Hatahivyo ukosefu wa ujuzi wa teknolojia ya habari na mawasiliani kwa kifupi TEHAMA unakwamisha ufikaji wa intaneti kwa watu wengi huku takwimu zikionesha kuwa kuna pengo kubwa katika ujuzi unaohitajika na ambapo idadi ya watu wanakosa ujuzi muhimu kama vile kuhamisha mafaili na ni asilimia 41 tu walio na ujuzi wa wastani wa kuweka programu za kompyuta na kutumia programu mbalimbali; huku asilimia nne tu ndio wanatumia lugha mahsusi kuandika programu za kompyuta.
Mkutano wa biashara mtandaoni barani Afrika ulifanyika wiki iliyopita Nairobi Kenya kwa lengo la kuimarisha uwezo wa nchi za Afrika kushiriki na kunufaika na biashara mtandaoni na uchumi wa kidijitali.
Mkutano huo ulioratibiwa na Kamati ya Biashara na Maendeleo ya Umoja wa Mataifa, UNCTAD ulibeba kaulimbiu “Kuwezesha Uchumi wa nchi za Afrika katika zama za kidijitali".
Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano huo wa kwanza kabisa wa aina yake barani Afrika, Mkurugenzi Mtendaji wa UNCTAD, Dkt. Mukhisa Kituyi amesema kuwa sasa kuna ukuaji mkubwa wa biashara mtandaoni kote ulimwenguni na pia barani Afrika ikiwa ni asilimia 18 kwa mwaka lakini anahoji hali hii,“Huenda ni kweli kwamba watu milioni 21 wananunua huduma mtandaoni, huenda ni kweli kuwa watu milioni 134 wanatembelea mtandao wa Facebook lakini kweli kabisa kuwa hakuna kiwango cha maana cha huduma zinazouzwa kutoka Afrika mtandaoni, kwamba bidha kutoka Afrika zilizopo vijijini zinazouzwa na wanawake hazionekani popote katika soko ya kidijitali na hivyo tunahitaji mazungumzo ambapo walioweza wasaidie wengine.”
Ameongeza kuwa hawawezi kusherehekea kuwa Afrika imepiga hatua wakati asilimia 50 ya biashara mtandaoni inamilikiwa na Kenya, Afrika Kusini na Nigeria.
Kwa upande wake rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, katika ufunguzi huo amesema ili Afrika iweze kupata faida za biashara mtandaoni...“Sera zinapaswa kuwa zinaweka mazingira rafiki na hivyo ni muhimu kwamba sekta hii ikapewa umuhimu unaohitajika.

Makamu wa Rais wa Iran anayeshughulikia masuala ya Sayansi na Teknolojia Dkt. Sorena Sattari ametembelea Afrika Kusini wiki hii na kusema Iran itaipa Afrika Kusini uzoefu wake wa mafanikio katika uga wa sayansi.
Sattari aliyasema hayo Ijumaa akiwa nchini Afrika Kusini ambapo alisema Iran imepata mafanikio makubwa ya kisayansi katika nyuga za nanoteknolojia, bioteknolojia, seli shina, tekenolojia ya habari na mawasiliano n.k.
Amesema katika safari yake nchini Afrika Kusini, mafanikio ya Iran katika sekta za sayansi na teknolojia yameweza kuonyesha katika vituo mbali mbali. Aidha amebaini kuwa zile zamabo ambazo vikwazo vilikuwa na athari hasi zimepita na sasa fikra za kitenolojia na ubunivu zinaenea. Makamu wa Rais wa Iran anayeshughulikia masuala ya Sayansi na Teknolojia alifika mjini Johannesburg akiongoza ujumbe wa ngazia za juu wa wakurugenzi 48 wanaosimamia mashirika ya uwekezai katika nyuga za teknolojia ya habari na mawasiliano, afya, bioteknolojia, uchimbaji madini, mashine za kiviwanda na bidhaa za kielektroniki. Mkutano wa ujumbe huo wa Iran na wenzao wa Afrika Kusini ulifanyika Jumanne mjini Johannesburg.
@@@
Wiki hii hapa mjini Tehran kumefanyika Sherehe ya 19 ya Kuwaenzi Wanasayansi na Watafiti Bora Iran. Sherehe hizo zimehudhuriwa na Makamu wa Kwanza wa Rais Iran Ishaq Jahangiri, Makamu wa Rais anayeshughulikia masuala ya sayansi na teknolojia Dkt. Sorena Sattari, Waziri wa Afya Daktari Kadhi-Zadeh Hashemi na Waziri wa Sayansi, Utafiti na Teknolojia Profesa Mansour Gholami. Katika sherehe hizo wanasayansi na wataalamu wa teknolojia wapatao 24 walitunukiwa zawadi miongoni mwa 24 ambao walifika fainali.
Akizugumza katika sherehe hizo, Jahangiri amesema Marekani imefeli katika njama zake za kuudhuru uchumi wa Iran. Amesema sera za uchumi wa kimapambano ambazo Iran inatekeleza zimejikita pia katika masuala ya sayansi na teknolojia na kustawisah mashirika ambayo yana msingi wa kielimu yaani knowledge based. Amesema hivi sasa mashirika hayo ambayo yana msingi wa kielimu yamefanikiwa kuuza nje ya nchi bidhaa zenye thamani ya dola milioni 400 na kuongeza kuwa kuna mpango wa kuhakikisha kuwa kiwango hicho kinafika dola bilioni 100 kwa mwaka. Jahangiri amesema ustawi wa sayansi na teknolojia ni muhimu katika ustawi endelevu wa nchi na ni silaha ya kukabiliana na matatizo.

Na mapema mwezi wa Disemba 2018 Duru ya Pili ya Mashindano ya Kimataifa ya Roboti ya Asia na Pasifiki maarufu kama RoboCup Asia-Pacific 2018 yalifanyika katika Kisiwa cha Kish kusini mwa Iran katika Ghuba ya Uajemi. Mashindano hayo ya siku mbili yalikuwa na vitengo viwili vya roboti kamili na roboti za wanafunzi na yalihudhuriwa na washiriki kutoka nchi 15. Nchi zilizoshiriki ni pamoja na mwenyeji Iran, Russia, Australia, Japan, China, Korea Kusini, Singapore, Malaysia, Indonesia, Thailand, Turkey, Afghanistan na Umoja wa Falme za Kiarabu. Kati ya roboti zilizokuwa na mvuto ni roboti zenye kucheza mpira wa miguu na sababu imetakwa kuwa katika mwaka 2050, Jumuiya ya Kimataifa ya Roboti inapanga kuandaa mchezo wa soka baina ya timu ya wanadamu na timu ya roboti. Halikadhalika roboti za kiviwanda pia zilitia for a katika mashindano hayo ambapo roboti za Singapore na Ujerumani zilishindana na timu tano za Iran. Halikadhalika kuliwa na mashindano ya roboti za zima moto, roboti za kutekeleza shughuli za uokoaji, roboti za chini ya maji na pia roboti za kubeba mizigo bandarini.
@@@
Naam na kwa habari hiyo ya Duru ya Pili ya Mashindano ya Kimataifa ya Roboti ya Asia Pasifiki yaliyofanyika katika kisiwa cha Kish kusini mwa Iran ndio tunafika mwisho wa makala yetu ya Sayansi na teknolojia kwa leo. Ni matumaini yangu umeweza kunufaika kikamilifu. Hadi wakati mwingine panapo majaliwa yake Mola, Kwaherini.