Jan 15, 2019 06:22 UTC
  • Mapinduzi ya Kiislamu Katika Nadharia za Sayansi ya Jamii (3)

Sehemu ya Pili: Mapinduzi ya Kiislamu yalivyojipambanua na mapinduzi mengine makubwa duniani. Msikilizaji mpenzi wa Radio Tehran, huku nikitumai kuwa hujambo popote pale ulipo wakati huu, nakukaribisha kusikiliza kipindi hiki kinachokujia kila wiki, siku na saa kama hii. Endelea kuwa nami basi hadi mwisho wa mazungumzo yetu, ili kuweza kufaidika na yale niliyokuandalia katika mfululizo huu wa pili.

Tukiendelea na pale yalipoishia mazungumzo yetu katika kipindi kilichopita, katika kueleza sifa zinazoyapambanua na kuyatafautisha Mapinduzi ya Kiislamu na mapinduzi mengine makubwa katika namna ya kutokea kwake, sifa nyingine ya kipekee ya mapinduzi hayo inahusu uongozi wa mapinduzi yenyewe. Uongozi wa vuguvugu la Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ulikuwa mikononi mwa viongozi wa dini; tabaka ambalo wachambuzi na wanasiasa hawakuwa na uwelewa nalo mkubwa pamoja na sifa zake maalumu za kifikra, kijamii, kiakhlaqi na kisiasa. Sambamba na hilo, uongozi wa Imam Khomeini (MA), ulikuwa ni nukta muhimu kwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran. Uongozi wa Mapinduzi ya Iran ulikuwa mikononi mwa mtu mwenye shakhsia ya kupendwa mno na watu, akiwa pia marjaa taqlidi, yaani faqihi mkuu anayefutu mas-ala yote ya dini. Wananchi wa Iran walikuwa na kiongozi mwenye shkhasia iliyokamilika pande zote; yaani mbali na kuwa mwanasiasa, alikuwa kiongozi wa kidini na kiakhlaqi pia.

Ervand Abrahamian, anaizungumzia nukta hiyo kwa kusema: "Kuna sababu mbili zinazoweza kubainisha nafasi muhimu na mapenzi makubwa ya watu kwa Ayatullah Khomeini. Sababu ya kwanza ni shakhsia yake, hususan maisha ya kawaida na yasiyo na makuu aliyokuwa akiishi Ayatullah Khomeini na kukataa kupatana na yule "dhalimu mwenye sifa za kishetani". Katika nchi ambayo wanasiasa wake wengi walikuwa wakiishi maisha ya raha na uneemevu, Ayatullah Khomeini alikuwa akiishi maisha ya kujihini; na kama walivyokuwa watu wengi wa kawaida hakuwa na hali ya uneemevu wa kimaada. Katika jamii ambayo viongozi wake wa kisiasa walikuwa na nyuso lukuki, wakiwa na maradhi yasiyotibika ya kufanyiana mambo kwa ujamaa, kulindana na kujuana, Ayatullah Khomeini alikuwa hakubaliani kwa namna yoyote ile na mwenendo huo na akiitakidi kwamba, atawahukumu adhabu ya kifo hata watoto wake mwenyewe, kama watastahiki kupewa adhabu hiyo. Ayatullah Khomeini, alifanya kama walivyo waja wateule wa Mwenyezi Mungu, ambao badala ya nguvu za kidhahiri za kimaada, wao wanatafuta na kupigania nguvu na uwezo wa kimaanawi.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Jambo la pili linalobainisha nafasi na hadhi ya aina yake aliyokuwa nayo Ayatullah Khomeini, ni shakhsia yake ya kukubalika mno kwa watu, hususan katika kuongoza umma mkubwa unaojumuisha makundi tofauti ya kisiasa na kijamii. Katika kuukosoa utawala, alikuwa akizungumzia zaidi mambo yanayonung'unikiwa na mirengo yote tofauti; kama upendeleo wa masualaa kadhaa uliotoa (utawala wa Shah) kwa Magharibi, mfungamano wake wa siri na usio wa moja kwa moja baina yake na Israel, matumizi yasiyo ya lazima ya kugharimia ununuzi wa silaha, ufisadi mkubwa uliokuwa umeenea miongoni mwa wakubwa serikalini, uzorotaji na hali isiyoridhisha katika sekta ya kilimo pamoja na ufa wa kitabaka uliokuwa ukizidi kupanuka. Ni kwa njia hiyo, Ayatullah Khomeini aliweza kuyavutia makundi mbali mbali ya kijamii na kuyafanya yaungane naye, kutokana na kuyapigania na kuyasemea mambo mengi yaliyokuwa yakinung'unikiwa na wananchi wengi."

Moja ya sifa nyingine muhimu zaidi inayoyapambanua na kuyatafautisha Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na mapinduzi mengine makubwa ni kwamba, mapinduzi hayo yaliutambulisha kwa walimwengu mfumo mpya wa utawala. Kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, dunia ilikuwa imebadilishwa na kugawanywa katika kambi mbili za Magharibi na Mashariki na mifumo miwili ya utawala wa Demokrasia ya Kiliberali na Ukomunisti, ambapo madola makuu mawili ya Marekani na Shirikisho la Kisovieti la Urusi ndiyo yaliyokuwa yakiongoza kambi hizo mbili na nchi zilizobaki zikiwa chini ya miamvuli ya kambi hizo. Hata kuundwa kwa Harakati Isiyofungamana na Upande Wowote, yaani Non-Aligned Movement, kwa kifupi NAM hakukuweza kuzifanya nchi wanachama wa vuguvugu hilo kujivua na utegemezi wa kambi hizo mbili za Magharibi na Mashariki. Iran ya kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu, ilikuwa kwenye kambi ya Magharibi iliyokuwa ikiongozwa na Marekani. Kutokea Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kulibadilisha hali hiyo iliyokuwepo, kwa kuutangaza na kuutambulisha mfumo mpya wa utawala ambao ni "Jamhuri ya Kiislamu". Mfumo huo mpya wa utawala, uligeuka kuwa mtindo na ubunifu mpya wa utawala, kiasi kwamba hata yalipojiri mapinduzi katika nchi za Kiarabu mnamo mwaka 2011, yalikuwa kigezo na kielelezo kilichoigwa na kufuatwa na nchi zilizokumbwa na mabadiliko ya utawala.

Iran imepiga hatua kubwa za kimaendelea katika kipindi hiki cha miaka 40 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu

 

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Khamenei, amekitaja kielezo hicho kuwa ni moja ya sifa pambanuzi za Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kulinganisha na mapinduzi mengine makubwa. Katika hotuba aliyotoa kwenye Sala ya Ijumaa iliyosaliwa tarehe 30 Machi mwaka 1990 (10 Farvardin 1369), aliizungumzia nukta hiyo kwa kusema: "Hadi kabla yake (Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran), kwa muda wa miaka mingi, dunia ilikuwa imepitia na kuzikubali aina mbili za utawala; moja ni demokrasia za Magharibi, na nyingine ni tawala za Kikomunisti. Katika zama za kale, walikuwepo wafalme, ambao walikuwa wakitawala kwa rai zao wao tu; pasi na kuwepo sheria yoyote ya wao kufuata; ni wao wenyewe ndio waliokuwa wakitunga sheria; na lile walilolitaka wao, ndilo pekee lililotekelezwa na kutumika kwa ajili ya kuwatawala watu. Huu ni utaratibu wa kale na uliopitwa na wakati katika utawala; japokuwa hata leo hii pia kuna nchi zinazoendeshwa kwa mtindo huu huu, lakini kwa kutumia sura na majina tofauti; na kabla ya Mapinduzi, nchi yetu pia ilikuwa ikiendeshwa kwa namna hiyo hiyo. Baada ya nchi za ulimwengu zilizopiga hatua kuweza kuondokana na tawala za aina hii za kiimla, zilipata uzoefu wa kupitia aina nyingine mbili za utawala: Moja ni demokrasia za Magharibi, zilizoenea katika nchi za Magharibi na zilizo chini yao; na aina nyingine ni tawala za Kikomunisti, ambazo zenyewe zilikuwa zimejipa jina la tawala za wafanyakazi za vibarua, lakini waliokuwa wakiongoza tawala hizo walikuwa ni makabaila na mabwanyenye, si vibarua. Na kileleni mwa tawala hizo, watu waliokuwa wakishika madaraka na kutawala hawakuwa na tofauti yoyote na wafalme na watawala walewale wenye mfumo wa utawala unaotafautiana na wao."

Mpenzi msikilizaji, sehemu ya pili ya kipindi cha Mapinduzi ya Kiislamu Katika Nadharia za Sayansi ya Jamii, imefikia tamati. Hivyo tusite hapa kwa leo hadi tutakapokutana tena wiki ijayo inshallah katika sehemu ya tatu ya kipindi hiki. Ahsante kwa kunisikiliza