Jun 23, 2019 18:23 UTC

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu ya 21 ya kipindi hiki cha Katika Maktaba ya Imam Khomein (MA) ambacho kinakujieni kwa mnasaba wa miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran.

Katika kipindi kilichopita tulizungumzia nafasi chanya ya wanawake katika shughuli na kazi zote za ujenzi wa taifa kuanzia mwanzo wa Mapinduzi ya Kiislamu na baada yake, endeleeni kuwa pamoja nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

Ndugu wasikilizaji, Imam Khomeini (MA) kwa kuambatanisha siku ya mwanamke na siku aliyozaliwa Bibi Fatwimat Zahra (as) alijaribu kuwasilisha mfano bora wa mwanamke katika jamii ambapo mbali na kuashiria ustawi wake wa mtu binafsi na kijamii alisema pia kwamba mwanamke ni mlezi muhimu wa wanaume mashuhuri katika jamii. Alisema: “Siku ya kuzaliwa Bibi Fatwimat Zahra Mridhiwa (as) ambayo ni siku ya mwanamke, ni siku pia ya ushindi wa mwanamke. Mwanamke ni mtu mwenye nafasi muhimu katika jamii. Mwanamke ni dhihirisho la kufikiwa matumaini ya mwanadamu. Mwanamke ni mahala pa kulelea wanawake na wanaume watukufu.

Bibi Fatwimat Zahra pambo la wanawake duniani

 

Kupitia mwanamke, mwanaume anaweza kufikia kilele cha utukufu, na mikononi mwa mwanamke ni mahala pa malezi makubwa ya wanawake na wanaume. Hii siku ni siku kubwa, siku ambayo mwanamke mtukufu na kiigizo chema kwa wanadamu amezaliwa.” Hotuba ya Imam aliyoitoa mbele ya wanawake tarehe 27/2/1358.

******

Kadhalika Imam Khomeini alikuwa mmoja wa wakosoaji wakubwa wa hali mbaya ya wanawake katika kipindi cha utwawala wa kitwaghuti uliopita kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran. Akizungumzia hali mbaya ya wanawake katika kipindi hicho alisema: “Mwanamke amekuwa mwenye kudhulumiwa katika vipindi viwili, moja ni kipindi cha ujahili, ambapo baadaye Uislamu uliweka misingi ya kumuokoa mwanadamu na mwanamke kutokana na dhulma hiyo ya ujahili. Kipindi cha ujahili, kilikuwa kipindi  ambacho mwanamke si tu kwamba alikuwa sawa na mnyama, bali alikuwa chini zaidi ya kiumbe huyo. Hatua nyingine ambayo mwanamke alikumbwa na dhulma, ni kipindi cha utawala wa Shah wa zamani na Shah wa baada yake, ambao kwa kutumia jina la kile walichosema kuwa ni kutaka kumpa uhuru mwanamke, walitekeleza dhulma dhidi yao na kumteremshia mwanamke daraja yake ya utukufu. Aidha walimuondoa mwanamke katika daraja yake ya umaanawi kwa kisingizio cha uhuru na hivyo kuwapokonya wanawake na wanaume uhuru wao, matokeo yake yakiwa ni kuwasababishia uharibifu wa kimaadili wanawake na vijana wetu.” Hotuba ya tarehe 26/2/1358.

Wanawake kabla ya mapinduzi ya Iran walikuwa waliodhulumiwa sana na wanyonge

 

Kadhalika Imam Khomeini alielezea dhulma ya utawala wa kidikteta wa Shah kwa wanawake ikilinganishwa na matabaka ya watu wengine wa jamii kwa kusema: “Ninaweza kusema kuwa, katika kipindi cha Mfalme Shah wa kwanza na mtoto wake, wanawake wamedhulumiwa sana wakilinganishwa na watu wa matabaka mengine. Hamjui ni kitu gani waliwafanyia wanawake na ni msiba gani waliwasababishia wanawake kwa jina la kile walichodai kuwa wanataka kuifanya Iran kuwa kama Ulaya…..” Hotuba aliyoitoa mbele ya wanawake wa mkoa wa Ahvaz tarehe 10/4/1358.

*******

Kama kwanza ndio unafungulia redio yako, kipindi kilicho hewani ni sehemu ya 21 ya mfululizo wa vipindi vinavyofafanua nadharia ya Imam Khomeini (MA), kuhusu Mapinduzi ya Kiislamu kinachokujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Aidha Imam Khomeini (MA) sambamba na kukosoa mtazamo wa Magharibi na wa kipindi cha utawala wa kifalme humu nchini kuhusu haki za wanawake, alifichua hadaa zao za kuwalazimisha wanawake kuvua hijabu ambapo alikuwa akiwaasa wanawake wasihadaike na madai hayo yaliyolenga kuwanyang’anya uhuru wao kwa kusema: “Katika kipindi cha utawala wa Reza Shah Pahlavi ni matukio gani hatukuyashuhudia kwa wanawake wa mji wa Qum na miji mingine ya Iran! Mfalme huyo kwa kufuata watawala wengine na kuwavua wanawake vazi la hijabu, ni kwa kiasi gani aliuvunjia heshima Uislamu, matukufu ya waumini na matukufu ya wanawake! Vibaraka wake waliwafanyia mambo gani wanawake?! Ni kwa kiasi gani waliyachana mavazi yao ya kujistiri! Ni kwa kiasi gani waliwavua hijabu na shungi zao….! Mwenyezi Mungu anajua katika kadhia hiyo ya kuwavua hijabu wanawake ni mambo gani mabaya yaliwakumba watu wa Iran….Wanawake walikuwa wakilazimishwa na kupigwa ili kukubali uhuru (wa Magharibi), sambamba na polisi kuwavunjia heshima watu. Inawezekana vipi mtu Mwislamu akubali kirahisi kuvua hijabu yake? Na hapo ndipo wanawake wa Iran wakasimama kupambana na utawala huo katika kutetea matukufu yao......” Hotuba ya tarehe 29/10/1357.

******

Katika radiamali yake kuhusiana na hali hiyo aliwashajiisha wanawake waliokuwa bega kwa bega na wanaume au hata zaidi yao katika kusimama kishujaa katika safu ya mapambano dhidi ya utawala wa Shah, ambapo alikuwa na nafasi athirifu katika kuwapa moyo wananchi wa Iran. Bila shaka yoyote lau kama wanawake wasingekuwa safu moja na wanaume katika kupambana na utawala wa Shah, ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu usingefikiwa. Imam Khomein (MA) sambamba na kukiri juu ya nafasi muhimu na athirifu ya wanawake katika ushindi wa Mapinduzi, aliyataja mafanikio ya mwamke wa Kiislamu kuwa yaliyotegemea juhudi na ushujaa wa wanawake wenye ghera wa Iran kwa kusema: “Mwenyezi Mungu akuhifadhini nyinyi nyote. Ushindi huu tumeupata kutoka kwa wanawake hata kabla ya wanaume. Wanawake watukufu walikuwa katika safu ya mbele. Wanawake wetu walikuwa sababu ya wanaume kupata ushujaa na ujasiri. Mafanikio haya yanatokana na juhudi zenu nyinyi wanawake.” Hotuba aliyoitoa mbele ya wanafunzi wa kike wa Chuo Kikuu cha Shahid Beheshti na wanafunzi wa shule za sekondari wa mkoa wa Dezful na Qasr-e Shirin mkoa wa Kermanshah tarehe 23/1/1358. Katika sehemu nyingine kuhusiana na nafasi ya wanawake ndani ya Mapinduzi ya Kiislamu, Imam anasema: “Salamu zisizo na kikomo ziwaendee wanawake wa Iran.

Muda punde baada ya mapinduzi, wanawake wakaingia katika ulingo wa teknolojia na kushika nafasi mbalimbali za kielimu

 

Rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yenu nyinyi mashujaa ambao kwa azma yenu ya juu, mmeutoa Uislamu katika minyororo ya utumwa wa kiajenabi. Nyinyi wanawake mashujaa, kwa kuwa bega kwa bega na wanaume mmefanikisha ushindi wa Uislamu. Ninawashukuru wanawake wote wa Iran na ninatoa shukurani maalum kwa ajili ya wanawake wa mji wa Qum…..Ninyi mkiwa na watoto wenu wadogo mlimiminika mitaani kuutetea Uislamu. Kila nilipokuwa nikisikia habari za mji wa Qum na miji mingine ya Iran nilikuwa nikihisi ghera kutokana na ushujaa wa wanawake katika ushindi huu. Wanawake waliwashajiisha wanaume na kwa hakika wanaume wetu walitegemea ushujaa wenu nyinyi wanawake shujaa.” Hotuba ya Imam Khomeini (MA) alipokutana na wanawake wa Qum tarehe 5/2/1358.Ukweli ni kwamba nafasi chanya na ushujaa wa wanawake wa Iran, haukuishia tu kwenye ushindi wa Mapinduzi. Kwani hata baada ya ushiriki wao katika kuung'oa madarakani utawala wa kitwaghuti, waliendelea kutetea malengo mengi ya Mapinduzi hususan katika uga wa kufikiwa uadilifu wa kijamii na kadhalika katika kutetea ardhi ya Iran, mambo ambayo Mwenyezi Mungu akipenda tutayafafanua katika vipindi vinavyokuja.

Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji, sehemu ya 21 ya kipindi hiki cha Katika Maktaba ya Imam Khomeini (MA) ambacho kimekujieni kwa mnasaba wa kutimia miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, inaishia hapa kwa leo. Mimi ni Sudi Jafar, kwaherini.