Nov 02, 2019 04:15 UTC
  • Jumamosi, tarehe Pili Novemba, 2019

Leo ni Jumamosi tarehe Nne Mfunguo Sita Rabiul-Awwal 1441 Hijria mwafaka na tarehe Pili Novemba 2019 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 255 iliyopita alifariki dunia huko Karbala, Iraq faqihi, mpokezi wa hadithi, mhakiki na mwandishi maarufu wa Kiislamu katika karne ya 12 Hijria Sheikh Yusuf Bahrani. Alisoma masomo ya awali kwa baba yake na baadaye alielekea Bahrain na Makka kwa ajili ya kupata elimu ya juu. Baadaye alielekea katika mji wa Fasa kusini mwa Iran ambako alianza kufundisha na kuandika vitabu. Wakati huo alianza kuandika kitabu chake kikubwa zaidi cha fiqhi kinachoitwa "al Hadaiq al-Nadhirah". Mwanzuoni huyo ameandika vitabu 32 katika taaluma mbalimbali vikiwa ni pamoja na "Anisul Musafir" na "Jalisul Khawatwir.'' ***

Sheikh Yusuf Bahrani

 

Katika kama ya leo miaka 103 iliyopita, sawa na tarehe Pili Novemba 1916, Sharif Hussein mtawala wa Makka na Madina, alijitangaza kuwa mfalme wa tawala zote za Kiarabu. Mtawala huyo kuanzia tarehe 5 mwezi Juni mwaka huo huo na kwa ushawishi wa Uingerea alianzisha mapambano dhidi ya utawala wa Othmaniyah, wakati utawala huo ulikuwa na vita na waitifaki wake katika Vita vya Kwanza vya Dunia. Uingereza ilimuahidi Sharif Hussein kuwa baada ya vita hivyo, ingemtambua rasmi kama mfalme anayejitegemea wa Saudi Arabia. Hata hivyo Uingereza haikutekeleza ahadi yake hiyo na badala yake ikawaunga mkono watawala wa kizazi cha al-Saud dhidi ya Sharif Hussein. Aidha katika kusafisha sura yake chafu kati ya Waarabu, London iliamua kuwapatia ufalme watoto wa Sharif Hussein katika nchi za Iraq na Jordan, chini ya usimamizi wa Uingereza. ***

Sharif Hussein

 

Miaka 102 iliyopita inayosadifiana na tarehe Pili Novemba mwaka 1917, lilitolewa tangazo la James Balfour. Tangazo hilo lililotolewa na Arthur James Balfour Waziri wa Mambo ya Nje wa wakati huo wa Uingereza liliandaa uwanja wa kuasisiwa utawala haramu wa Israel huko katika ardhi za Palestina zilizokuwa chini ya wakoloni wa Uingereza. Tangazo hilo pia liliipa idhini serikali ya London kuunda utawala wa Kiyahudi katika ardhi za Palestina sanjari na kuitaka serikali hiyo kufanya kila iwezalo kufanikisha jambo hilo. Mwishowe miaka 30 baada ya kutolewa tangazo hilo la kikoloni mnamo mwaka 1948, utawala wa Kizayuni ulianzishwa kwa msaada wa Uingereza na Marekani na kwa kukanyagwa haki zote za wananchi wa Palestina. ***

Arthur James Balfour

 

Katika siku kama ya leo miaka 83 iliyopita, mtambo wa kwanza kabisa wa kurushia matangazo ya televisheni ulianza kazi mjini London, Uingereza. Mtambo wa kwanza wa kurusha matangazo ya redio ulianza kabla ya hapo yaani mwaka 1920. Ni vyema kuashiria hapa kuwa, mtambo wa kwanza wa kurusha matangazo ya redio nchini Iran ulianza kazi mwaka 1940 na wa matangazo ya televisheni ulifuatia mwaka 1958. Hii leo matangazo ya redio na televisheni ni sehemu isiyotenganishika na sehemu kubwa ya maisha ya wanadamu. ***

Mtambo wa kurushia matangazo ya televisheni

 

Siku kama ya leo miaka 70 iliyopita Indonesia ilijipatia uhuru baada ya kukoloniwa na Uholanzi kwa karne tatu na nusu. Kwa mujibu wa mkubaliano yaliyotiwa saini siku hiyo kati ya Uholanzi na wanamapinduzi wa Indonesia chini ya uongozi wa Dakta Ahmad Sukarno na Ahmad Hata, vikosi vya wakolozi wa Kiholanzi vilitakiwa kuondoka katika ardhi ya Indonesia. Makubaliano hayo yalitiwa saini baada ya miaka minne ya mapambano ya Waindonesia yaliyoanza mwezi Agosti mwaka 1945, ambapo baada ya uhuru wa Indonesia Dakta Sukarno alichaguliwa kuwa rais wa nchi hiyo, na kubakia madarakani hadi mwaka 1965 alipoondolewa madarakani kupitia mapinduzi ya kijeshi. ***

Bendera ya Indonesia

 

Miaka 56 iliyopita katika siku kama ya leo ya tarehe 11 Aban 1342 Hijria Shamsia Tayib Haj-Rezaei mmoja wa wapinzani mashuhuri wa utawala wa kidhalimu wa Kipahlavi hapa Iran alinyongwa. Alizaliwa mwaka 1280 Hijria Shamsia katika mji wa Tehran na kwa kipindi fulani alikuwa akihesabiwa kuwa mfuasi wa utawala wa kifalme wa Kipahlavi. Hata hivyo imani ya Tayib Haj-Rezaei kwa Uislamu hususan mapenzi yake makubwa kwa Imam Hussein AS ni mambo yaliyomfanya ajitenge na utawala huo wa Kifalme wa Shah na kujiunga na harakati ya mapinduzi ya Imam Ruhullah Khomeini MA. Hatimaye baada ya mateso mengi, alivyongwa katika siku kama ya leo. ***

Tayib Haj-Rezaei

 

Na miaka 55 iliyopita katika siku kama ya leo, Saud bin Abdulaziz Al Saud mfalme wa Saudi Arabia aliondolewa madarakani katika mapinduzi yaliyofanywa na ndugu yake, Faisal bin Abdul Aziz. Faisal alikuwa Waziri Mkuu wa Saud bin Abdul Aziz na alitumia ujanja kwa ajili ya kupata uungaji mkono wa idadi kadhaa ya wanafamilia wa kizazi cha Aal Saud na maulama wa Kiwahabi. Wakati Mfalme Saud alipokwenda nje ya nchi kwa ajili ya matibabu, Faisal aliwapa wafuasi wake ndani ya kizazi cha Aal Saud nyadhifa muhimu kama uongozi wa Gadi ya Taifa na kwa njia hiyo akawa amedhibiti nchi. Mapinduzi hayo yaliungwa mkono na wanasiasa na viongozi wa kidini wa Saudi Arabia na Faisal akawa mfalme mpya wa nchi hiyo. Miaka 11 baadaye Mfalme Faisal bin Abdul Aziz mwenyewe pia aliuawa na ndugu yake. Vita vya kuwania madaraka vimekuwepo siku zote ndani ya kizazi cha watawala wa Aal Saud huko Saudi Arabia ambapo baadhi ya wakati vita hivyo vimekuwa vikidhihirika wazi na tena kwa kutumia mabavu. ***

Saud bin Abdulaziz 

 

Tags