Dec 24, 2019 04:28 UTC
  • Jumanne, tarehe 24 Disemba, 2019

Leo ni Jumanne tarehe 27 Rabiuthani 1441 Hijria sawa na Disemba 24 mwaka 2019.

Katika siku kama ya leo miaka 495 iliyopita, aliaga dunia Vasco da Gama baharia na mvumbuzi mashuhuri wa Kireno. Vasco da Gama alizaliwa mwaka 1460. Mwaka 1498, baharia huyo wa Kireno alifanya kazi muhimu ya kuvumbua njia ya majini kutoka Ulaya hadi bara la Asia na India.
Miaka 170 iliyopita wanajeshi wa Ufaransa waliivamia ardhi ya Guinea huko magharibi mwa Afrika. Uvamizi huo ulikuwa mwanzo wa nchi hiyo tajiri kwa madini ya dhahabu kudhibitiwa na Ufaransa. Kampuni ya Dhahabu ya Pwani iliundwa huko Guinea kabla ya uvamizi huo ili kuandaa mazingira ya kuingia kimabavu Ufaransa nchini humo.

Vasco da Gama

Miaka 170 iliyopita wanajeshi wa Ufaransa waliivamia ardhi ya Guinea huko magharibi mwa Afrika. Uvamizi huo ulikuwa mwanzo wa nchi hiyo tajiri kwa madini ya dhahabu kudhibitiwa na Ufaransa. Kampuni ya Dhahabu ya Pwani iliundwa huko Guinea kabla ya uvamizi huo ili kuandaa mazingira ya kuingia kimabavu Ufaransa nchini humo.

Bendera ya Guinea

Miaka 154 iliyopita katika siku kama ya leo, kundi la siri lililojulikana kwa jina la Ku-Klux-Klan ambalo liliitakidi kuwa watu weupe ni jamii ya watu bora na wa daraja la juu zaidi, liliasisiwa nchini Marekani kwa shabaha ya kupambana na watu wa jamii nyinginezo, hususan raia weusi. Japokuwa kundi hilo la Ku-Klux Klan lilipigwa marufuku miaka minne baada ya kuasisiwa kwake, lakini hadi kufikia sasa limefanya mauaji mengi dhidi ya raia weusi wa Marekani, kutesa, kuwaudhi, kuzusha hofu na kutoa vitisho dhidi yao. Kundi hilo linaua hata wazungu wanaotetea haki za makundi mengine. Pamoja na hayo hakujafanyika juhudi kubwa nchini Marekani kwa ajili ya kung'oa kabisa mizizi ya kundi hilo la kibaguzi na lenye misimamo ya kuchupa mipaka.

Ku-Klux-Klan

Siku kama ya leo miaka 68 iliyopita Libya ilijipatia tena uhuru wake baada ya kupasishwa azimio la Umoja wa Mataifa na Muhamad Idriss al Mahdi akateuliwa kuwa mfalme wa nchi hiyo. Huko nyuma Libya ilijulikana kwa jina la Tripoli na kwa miaka kadhaa ilikuwa chini ya himaya kubwa ya nchi za kigeni. Katika karne ya 16 Libya ilivamiwa na kukaliwa kwa mabavu na jeshi la Othmania. Aidha wakati wa kukaribia Vita vya Kwanza vya Dunia, nchi hiyo ilivamiwa na Italia lakini wananchi wa Libya wakapambana vikali na wavamizi hao wa Ulaya. Ilipofika katikati ya Vita vya Pili vya Dunia, Uingereza na Ufaransa zikaikalia kwa mabavu nchi hiyo, na hatimaye Libya ikajipatia uhuru wake mwaka 1951.

Bendera ya Libya

Na siku kama ya leo miaka 36 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Sayyid Ahmad Khansari, faqihi na marjaa mkubwa wa Kishia. Akiwa na umri wa miaka 20, Ayatullah Ahmad Khansari alielekea mjini Najaf, Iraq na kustafidi na elimu kutoka kwa wasomi wakubwa kama vile Muhaqqiq Khorasani, Sayyid Muhammad Kadhim Yazdi, Shariat Isfahani na Muhaqqiq Naaini. Ayatullah Sayyid Ahmad Khansari alielekea mjini Arak, Iran katika kipindi cha kuasisiwa chuo cha hauza cha mji huo na kujishughulisha na ukufunzi. Baadaye msomi huyo alishirikiana na Ayatullah Sheikh Abdul-Karim Hairi katika shughuli za tablighi na baada ya kuasisiwa hauza ya Qum, chini ya usimamizi wa Ayatullah Hairi Yazdi, Ayatullah Ahmad Khansari alikuwa imamu wa Swala ya jamaa katika chuo cha Faiziya mjini humo. Alishirikiana bega kwa bega na wanazuoni wa Kiislamu wakiongozwa na hayati Imam Ruhullah Khomeini katika harakati za Mapinduzi ya Kiislamu dhidi ya utawala muovu wa Shah. Msomi huyo amelea ma lufunza wasomi wakubwa kama Ayatullah Murtadha Mutahhari, Imam Musa Sadr na Sayyid Ridha Sadr. Mwaka 1370 Hijiria, Ayatullah Ahmad Khansari alielekea mjini Tehran na kuwa imamu wa swala ya jamaa katika msikiti maarufu wa ‘Sayyid Azizullah’. Ameandika vitabu vingi katika taaluma za sheria na teolojia ya Kiislamu.

Ayatullah Sayyid Ahmad Khansari

 

Tags